Mshambuliaji wa pembeni wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa (Pichani), ameanza majaribio yake juzi kwenye klabu ya West Ham United ya Uingereza akiwa na hofu kutokana na kukutana na idadi kubwa ya wachezaji waliokwenda kufanya majaribio kwenye klabu hiyo.
Ngassa, ambaye alitua nchini Uingereza mwanzoni mwa wiki hii, alianza rasmi mazoezi akiwa na kikosi cha pili cha timu hiyo kilichochanganywa na wachezaji hao wanaojaribiwa, ambapo hali hiyo ilimfanya Ngassa kucheza kwa kutojiamini hali iliyosababisha wakala wake Yusuph Bakhresa kumtuliza presha.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Nipashe imezipata kutoka kwa Bakhresa, imeelezwa kuwa siku ya kwanza ya majaribio yake Ngassa, hakuonyesha uwezo wake kutokana na kuwa na hofu hasa baada ya kuona idadi ya wanaofanyiwa majaribio ni kubwa.
Imeleezwa kuwa baada ya hali ile Bakhresa, alimtaka mchezaji huyo kucheza soka lake la kawaida na kuondoa hofu ushauri ambao aliutekeleza, ambapo jana alifanya mazoezi ya pamoja na kikosi cha kwanza cha West Ham.
Taarifa hiyo imeweka wazi kuwa baada ya ushauri huo Ngassa, alitulia na kucheza mpira wake wa kawaida, ambapo juzi alionyesha uwezo uliompa nafasi ya kujumuika na kikosi cha kwanza cha West Ham.
“Kidogo alipata wasiwasi katika siku ya kwanza ya majaribio yake, lakini aliwekwa sawa na sasa anaendelea vizuri na anaonyesha mchezo wake wa kawaida,”alisema Bakhresa.
Mchezaji huyo ataendelea kufanya majaribio na kikosi cha kwanza hadi pale atakapomaliza muda uliopangwa kwa ajili ya majaribio hayo.