Arsenal, Chelsea hapatoshi
Msimu wa soka wa England unaanza na Jumapili hii kwa ufunguzi wa mechi ya Ngao ya Jamii baina ya Arsenal na Chelsea.
Wakati Chelsea wanacheza mechi hii kwa sababu wao ni mabingwa wa England, Arsenal wanaingia kwa kuwa ndio mabingwa wa Kombe la FA.
Ni mechi kubwa kwa sababu ndiyo inafungua pazia kwa ajili ya Ligi Kuu ya England (EPL) kuanza lakini kwa maana nyingine kutwaa taji hili si kwamba ndiyo timu mashuhuri sana.
Huu ni mwanzo tu wa msimu wa aina yake wa soka kutokana na jinsi klabu zilivyojiandaa, ambapo Manchester City walioshika nafasi ya pili msimu uliopota, Arsenal wa tatu na Manchester United wa nne wanataka kuwakabili Chelsea.
Hakuna shaka kwamba Chelsea wana kikosi kizuri na hata pasipo kuongeza wachezaji wapya wanatarajiwa kuwa imara lakini nguvu za kujiimarisha kwa wapinzani wao zimepata kumtia hofu kocha Mourinho.
Mechi ya Jumapili hii ya Ngao ya Jamii, kama kawaida inafanyika kwenye Uwanja wa Wembley, unaochukuliwa kama wa taifa kwa England na unakuja siku 64 tangu Arsenal walipotwaa hapo Kombe la FA kwa mara ya mbili mfululizo baada ya kuwakong’ota Aston Villa 4-0.
Timu zote mbili hazijafanya usajili wa wachezaji wengi kiangazi hiki, lakini lao moja ni kwamba golikipa mkongwe wa Chelsea, Petr Cech amehamia Arsenal na anatarajiwa kwamba ataanza langoni.
Pengine Chelsea watamwanzisha mshambuliaji wa Monaco aliyefanya vibaya Manchester United msimu uliopita alikokuwa kwa mkopo, Radamel Falcao aliyechukuliwa kwa mkopo pia na Chelsea.
Falcao, 29, alifunga mabao manne tu katika mechi 29 msimu uliopita kwa Man U. Chelsea wamemsajili kipa Asmir Begovic wa Stoke kujaza pengo la Cech.
Hii ni mechi inayowakutanisha mahasimu wawili ambao kwa muda sasa wameonesha dhahiri kutoelewana kwao, Arsene Wenger wa Arsenal na Jose Mourinho wa Chelsea.
Wenger anaingia kwenye mechi hii akiwa bado kupata ushindi dhidi ya Mourinho katika mechi 13 na tayari kiangazi hiki Mourinho amedai kwamba Arsenal wametumia fedha nyingi zaidi yao katika miaka michache iliyopita kwenye usajili.
Wenger amejibu kwamba huwa hasikilizi kile watu wanachofikiri au kusema. Hata hivyo, Ijumaa hii Mourinho amedai kwamba anaamini kwa jinsi Arsenal walivyo, wanaweza kuwa washindani wakubwa kwenye ubingwa wa England.
Arsenal walishinda kwenye mechi kama hii msimu uliopita walipocheza dhidi ya Manchester City ambapo waliwacharaza 3-0. Arsenal pia wamekuwa wazuri kwenye mechi za kabla ya msimu huu, ambapo tayari wametwaa mataji mawili katika michuano ya kirafiki ya Barclays Asia na Kombe la Emirates.
Chelsea wametumia sehemu ya muda wao wa maandalizi ya msimu mpya barani Amerika na walipata kufungwa 4-2 na New York Red Bulls kabla ya kwenda sare na Paris St-Germain na Barcelona, lakini katika mechi zote mbili Chelsea walishinda kwenye mikwaju ya penati.
EPL inaanza Agosti 8 mwaka huu, ambapo mabingwa watetezi watakwaana na Swansea wakati Arsenal watawakabili West Ham siku inayofuata