Nyota wa Brazil , Neymar alidhani amepooza kutokana na alivyoumiwa uti wa mgongo, na ni moja ya mambo yaliyomfanya kulia sana.
Aligongwa kwa nguvu na goti la mchezaji wa Colombia, Juan Zuniga hivyo kwamba hakuweza kuhisi kama miguu yake inafanya kazi.
Aligaragara kisha kutulia akilia machozi kwa sauti uwanjani hapo, kabla ya mwamuzi kumwona na kuita matabibu, maana alikuwa akifuatilia mpira upande mwingine wa uwanja wa Arena Castelao, Fortaleza Ijumaa.
Kuumia huko kumemwondosha moja kwa moja kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazofanyika nchini mwake, lakini madaktari wanasema atapona baada ya wiki kadhaa.
Tayari Zuniga amemtumia salamu na kumwomba radhi kwa rafu hiyo anayosema hakukusudia. Neymar ndiye alikuwa tegemeo la Brazil katika mashambulizi na wapo wanaodhani Samba Boys hawana tena nafasi ya kusonga mbele.
“Alisema haoni mawasiliano kuanzia kwenye mgongo kwenda chini, akaogopa kwamba amepooza,” kocha Luiz Felipe Scolari anasema akimnukuu mchezaji wake mwingine, Marcelo.
Scolari anasema kwamba Marcelo alitishika sana kumwona Neymar katika hali ile hivyo kuamua kumwita daktari moja kwa moja, lakini daktari hangeweza kwenda bila kuruhusiwa na mwamuzi.
Neymar alitolewa nje kwa machela, kisha akapakiwa kwenye helikopta na kupelekwa hospitali ya jirani akiwa hajiwezi, akigugumia kwa maumivu huku akilia.
Watu wengi maarufu wamemtumia salamu za pole kupitia mitandao ya jamii na tayari amerejea kwenye kambi ya Brazil kuwapa wenzake moyo.
Brazil wamekata rufaa dhidi ya kadi ya njano kwa nahodha Thiago Silva ambayo inamkosesha mechi ijayo kwa kuwa amefikisha mbili na watapata jibu la rufaa yao kabla ya mechi hiyo.
Silva ametia moyo wenzake kucheza kwa nguvu ili watwae kombe kama zawadi kwa nyota wao Neymar.