Sakata la ununuzi wa klabu ya Newcastle linaloendelea, wanunuzi wakiwa jamaa wa Saudi Arabia, linazidi kushika kasi na upinzani unakuwa mkali.
Wadau kadhaa wanataka kuona kwamba Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL), Chama cha Soka (FA) na kwa ujumla wake – Serikali wanaingilia na kuzuia dili hilo ili Wasaudia wasiichukue klabu hiyo.
Upinzani dhidi ya Wasaudia kuchukua klabu hiyo unatokana na madai na tuhuma nzito dhidi ya taifa hilo juu ya haki za binadamu, lakini pia madai kwamba serikali hiyo ya kisultani imekuwa ikilinda mtandao wa kampuni zinazorusha matangazo ya mechi za EPL kiharamia.
Sasa wadau wanasema kwamba, ikiwa serikali haiingilii kati sakata hilo na kuzuia kwa sababu za kimaadili, basi ichukue hatua kwa sababu ya uharamia unaofanywa ambapo EPL hawapati haki yao kwa kurushwa mechi za ligi yake nchini Saudi ana kwingineko Mashariki ya Kati.
Inadaiwa kwamba Wasaudia wamekuwa wezi wa muda mrefu wa hakimiliki za matangazo ya mpira, kitu kinachowafaidisha Wasaudia, lakini kuwapokonya haki Waingereza na pia kushusha hadhi ya ligi na taifa kwa ujumla.
Serikali ya Saudia inaunga mkono kundi linalotaka kuichukua Newcastle chini ya Mwana Mfalme Mohamed bin Salman, wakati pia imekuwa ikiwalinda na kuzuia hatua za kisheria dhidi ya mtandao unaoiba matangazo ya mpira wa England kupitia beoutQ.
Waziri wa Nchi (Dijiti, Utamaduni, Habari na Michezo), Oliven Dowden, ametakiwa kuchukua hatua kwa kuingilia kati dili hilo linalotarajiwa kuwa la pauni milioni 300 au zaidi, Mike Ashley akiamua kuiuza klabu hiyo.
Hata hivyo, hivi karibuni waziri huyo alisema kwamba haingekuwa rahisi kwa serikali kuingilia kati suala hilo – kuzuia Wasaudia kuchukua umiliki na uendeshaji wa moja ya klabu zinazojulikana zaidi katika Uingereza. Waingereza wanataka kuona klabu ikibaki mikononi mwao, ikiwa ni ishara ya kuenzi utamaduni wao wa muda mrefu.
Hatua kadhaa zilishachukuliwa katika mchakato wa kuiuza klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kutiliana saini nyaraka muhimu, lakini inasemwa kwamba kwa Ashley, hadi kitu kikamilike kabisa ndio mmoja anaweza kusema kwamba ni kweli, kutokana na utata wake.
Ashley amekuwa akilalamikiwa sana na washabiki wa Newcastle kutokana na ubahili wake, akikataa kusajili wachezaji wakubwa kiasi cha kuwachanganya makocha, na ndiyo sababu Rafa Benitez aliamua kuondoka klabuni hapo. Katika siku za karibuni, Newcastle wamekuwa wakifanya vizuri katika soka hadi mechi zilipositishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Kutokana na tabia za Wasaudia hao, wadau wa soka wanataka kuona kwamba nguvu zinaunganishwa kupambana na uharamia na ukiukaji wa haki za binadamu, na njia inayoonekana kufaa ni kuwazuia kuichukua klabu hiyo kongwe.
beautQ wamekuwa, kwa miaka mitatu hivi sasa, wakiiba haki za matangazo ya mechi kuanzia kwenye EPL hadi Planet Earth; The Nest na hata kwenye mechi za Uskochi. Wanarusha matangazo hayo nchini mwao, Mashariki ya Kati na hata Afrika Kaskazini kupitia satelaiti na kutengeneza faida kubwa.
Hatua kadhaa zimechukuliwa, zikiwamo za kisheria, kwa ajili ya kuzuia matangazo hayo, lakini kampuni kadhaa za uwakili zilizopewa kazi hizo zimekuwa zikiishia katika hatua za awali na kujitoa, ikidhaniwa kwamba zimekuwa zikipewa mlungula na serikali ya Saudia haitoi ushirikiano unaofaa kwa ajili ya haki husika kupatikana.
Juni mwaka jana, vyama vya rugby na kriketi vilibaki bila kuwa na washirika halali wa kurusha matangazo yao huko Mashariki ya Kati, baada ya shirika kubwa zaidi – OSN kutangaza kwamba halingenunua tena haki za matangazo hayo kutokana na uharamia wa beautQ. Hii imevisababishia vyama husika kukosa mapato tarajiwa.
Formula 1 tayari wamesalimu amri kutokana na kashfa hiyo, huku beIN Sports wakikiri kwamba uharamia umewagharimu sana, hivyo hawakuwa na mbadala zaidi ya kujtoa kwenye mkataba wa kurusha matangazo, ikimaanisha mapato kupungua huku beautQ wakizidi kutamba kijinai.