Makosa ya golikipa wa Mtibwa Sugar Said Mohamed Nduda yainyima Mtibwa Sugar kuondoka na alama tatu muhimu uwanja wa Jamhuri Morogoro dhidi ya Yanga.
Yanga imeambulia alama moja baada ya kulazimishwa sare ya kufungana goli 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hii tunaweza kusema kuwa dua ya Kifaru imedunda baada ya sare hiyo.
Kabla ya mchezo huo Msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kuomba dua ili wapate ushindi katika mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kupata alama tatu ili kujihakikishia kubaki ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Mtibwa Sugar ilikuwa ya kwanza kupata goli dakika ya 28 ya mchezo baada ya beki wa Yanga Juma Makapu kufanya makosa na Haruna Chanongo kufunga goli .
Goli la kurudisha la Yanga limepatikana dakika ya 83 baada ya Adeyun Saleh kupiga shuti nje kidogo ya eneo la hatari lililomshinda kipa Said Nduda.
Mtibwa Sugar sasa imefikisha alama 42 nafasi ya 14 ikiwa sawa na Mbao FC ikipishana kwa magoli ya kufunga na kufungwa.
Matokeo ya mechi nyingine, KMC imepoteza goli 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons huku Mbao FC ikiichakaza Namungo FC magoli 3-0.
Mwadui FC imeicharaza goli 1-0 timu ya soka ya Biashara United wakati Singida United imeambulia kichapo cha magoli 2-1 dhidi ya Kagera Sugar.