Menu
in

Ndoto za Olimpiki Tanzania imezimwa, tunahitaji mabadiliko ya haraka kwenye uongozi wa michezo….

*Ubinafsi wa viongozi kikwazo cha kukuza michezo
*Watoto wenye vipaji waishia kwenye ulevi na ngono
Michezo ya 30 ya Olimpiki imeanza kutimua vumbi jijini London, ikikusanya vipaji vya aina ya juu.
Michuano hii mikubwa kuliko yote duniani, inashirikisha nchi 205, ambapo Tanzania nayo imejitupa kujaribu bahati yake.
Pamoja na kwamba ni mashindano yanayofanyika kila baada ya miaka minne, yakitoa nafasi kubwa kwa wadau kujiandaa, Tanzania haiwezi kusema imejiandaa vyema.
Idadi ndogo ya washiriki ni ishara ya kwanza ya maandalizi duni na ama mwamko mdogo, kutojituma ipasavyo kwa wahusika, au kutekwa kwa fursa husika na kupotezewa malengo kwa kizazi cha sasa.
Tanzania kuwa na washiriki wasiofika hata kumi kwenye mashindano makubwa kama haya, ambayo ratiba yake inajulikana siku zote ni udhaifu mkubwa.
Wingi wa wachezaji kwa nchi ni moja ya njia za kujitangaza, kwa sababu kwenye maandamano ya kuingia kila moja inaoneshwa na wachezaji wake nyuma ya bendera na ngao yenye jina la nchi.
Kujituma kwenye mashindano yenyewe, kila wachezaji katika michezo mbalimbali waliyokuja kuwakilisha ni hatua ya pili.
Kilele chake ni kwa mshindi wa kwanza kwa kila mchezo kupata medali ya dhahabu, wa pili fedha na wa tatu shaba.
Siku njema huonekana asubuhi, Waswahili husema, ni wazi kwamba wingi wa washiriki hutoa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa kufuata sayansi ya uwiano.
Maana uchache wa wanamichezo wetu, japo walipendeza na suti zao za kibuluu na upeperushaji bendera kubwa na ndogo, ni kujifunga tayari.
Huko ni kujifunga kwa sababu kwanza hakuna uhakika iwapo wote watapata medali, na mazoea yamekuwa wengi kuzikosa, kwa hiyo timu inakuwa kimsingi imeshakosa nafasi nyingi za awali.
Badala ya timu kuingia na ndoto ya kushika nafasi ya kwanza, ya pili, ya tatu na nyingine zinazokaribia hapo, inakuwa na mawazo ya kuwa ya 100 au nyuma ya hapo.
Hapo n kwa kutumia kigezo cha idadi ya wachezaji wake tu, ikizingatiwa kwamba timu zote 205 zimetoa karibu wachezaji 11,000.
Ile tu kushiriki michezo yote iliyopo ni sifa kubwa, na msingi wa kuweza kutwaa medali zaidi. Kwa Tanzania ni kinyume, maana michezo iliyopo ni zaidi ya mara tatu ya washiriki wake.
Zipo nchi ndogo kijiografia na kiuchumi, zenye idadi ndogo ya watu zinazostahili kutuma mtu mmoja, watano au 10 lakini si Tanzania kubwa na yenye watu milioni 46.
Mfano wa karibu kuonesha Tanzania inavyokwenda isivyotakiwa ni jirani zetu Uganda yenye eneo dogo zaidi, uchumi mdogo zaidi, watu wachache zaidi (milioni 34) lakini imetuzidi wanamichezo wa Olimpiki mara dufu.
Kwamba medali ya mwisho ya fedha (si dhahabu) katika Olimpiki kwa Tanzania ilipatikana mwaka 1980 halijawa jambo la kuwasukuma Watanzania kujiandaa vyema.
Ndoto zlizojengeka kwamba baada ya akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kutwaa medali hizo za fedha, Tanzania ingetwaa medali nyingi zaidi za fedha na hata dhahabu ziliyeyuka.
Wakati ikidhaniwa matumaini yangerejea, kadiri miaka ilivyokwenda ndivyo ndoto zilifutika kabisa, zikazikwa kwenye kilindi kikubwa cha bahari, maana hadi leo, miaka 32 hakuna kitu.
Je, nini kinatukwaza? Yawezekana ni ukosefu wa mipango na kujituma katika kuitekeleza, tukiachia tu kila mmoja kwenye nyanja yake aoneshe nguvu zake.
Ukubwa wa nchi kijiografia na wingi wa watu uliozungumziwa awali ndiyo hazina ya vipaji, ndiyo maana nchi kubwa kama Marekani ina wachezaji 525 Olimpiki.
Hakuna anayesema Tanzania nayo ipeleke wengi kiasi hicho, lakini hata wakiachwa hao 500, inashindwa kupeleka walau 25?
Je, katika wingi wa vipaji vilivyosambaa kote mikoani Bara na Visiwani, wanakosekana wanamichezo 100 wa kufuzu?
Ili yote haya yafanikishwe lazima kuwe na dira ambayo inaweza tu kuwekwa Watanzania wakiwa na ndoto moja itakayowaongoza mwelekeo mmoja.
Uzuri wa Tanzania ni kwamba inavyo vitu vyote vya msingi kwa ajili ya maendeleo katika nyanja zote, michezo ikiwamo. Wapo watu waelewa wanaoweza kutoa uongozi mzuri na wamebarikiwa kwa rasilimali nyingi.
Katika vijiji vingi Tanzania kuna vipaji vya ajabu kwenye michezo karibu yote 25 ya Olimpiki. Ni jinsi tu ya kuvikuza na kufungua fikra za wachezaji na kuwaingiza kwenye hali ya kisasa ya sayansi kiutandawazi.
Katika Olimpiki hakuna michezo ya kutoka sayari nyingine, ni michezo ya kawaida tu – kuogelea, kulenga shahaba, soka ya wanawake na wanaume, tenisi, vishale, mpira wa pete, kikapu…yote inachezeka.
Kwa msingi huo, ndoto ya kuweza, ikichanganywa na uwezeshaji wa uongozi katika vipaji anuwai ambavyo vimekuwa vikichipuka kila wakati kote nchini, Tanzania ingekuwa mbali.
Nchi hii ya asali na maziwa, yenye eneo kubwa kuliko nchi nyingi za Afrika Mashariki na Kati (ukiondoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), ingeweza kuwika sana michezoni.
Kwa kufanya hivyo, lingekuwa tangazo kubwa sana kwa utalii wake usio kifani. Kukuzwa utalii kungeisaidia nchi kuingiza mabilioni ya shilingi kwa mapato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Lakini ndoto imeuawa na kuzikwa, wameachwa wachache wenye vipaji kujaribu bahati yao pembezoni walipo, hivyo kwamba ni shida kupanda hadi kufuzu kwa Olimpiki.
Ndoto nzuri ya Olimpiki inauawa na watu wenyewe – kwa ubinafsi wao, uroho na kutoridhika na walicho nacho, wanachochuma au hata wanachokipata kutokana na kodi za wananchi.
Wachache waliopewa dhamana wameshindwa kuwasaidia wananchi kuvuna asali na maziwa. wanakwama kubadili umasikini wao kuwa utajiri, hivyo ama kuzikalia rasilimali au kuacha zitafunwe na wachache kwa kushirikiana na wageni.
Tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi leo Tanzania ikiwa awamu ya nne, ni medali mbili tu za fedha.
Pengine wapo viongozi wanaoona ni matunda ya kutosha ya uhuru na ya kujivunia. Ndiyo maana hawaoni haja ya kuibua na kukuza vipaji vilivyotapakaa kila kona.
Naam, ndiyo maana wanaona ni sawa kupeleka wanamichezo saba kati ya 11,000 wanaoshiriki michezo mitatu kati ya 205.
Wanaona ni sawa kwa viongozi au watu wasio wachezaji kuwa wengi kuliko wachezaji kwenye msafara. Wanaweza kujitetea kwamba kila mchezo unahitaji kocha wake, daktari na nafasi nyingine watakazoamua kubuni.
Lakini ukweli pia utawaumbua, kwamba ni ukosefu wa uongozi bora kwenye michezo unaosababisha, kwani ikiwa kila mchezo ungekuwa na washiriki walau wawili, basi wachezaji wangezidi viongozi. Hilo ni doa tayari na ni vigumu kulifuta.
Kama bado hawapo tayari, je, wanaweza kuacha kushiriki ili wajiandae? Ikiwa ni hivyo, wanaweza kutoa ratiba na mipango yenyewe badala ya kutetea kwenda viongozi wengi kuliko wachezaji?
Si ajabu inalazimu kushiriki michezo hii na mingine inayokuja kila mwaka au kila baada ya miaka kadhaa kwa ajili ya posho za viongozi.
Bahati mbaya wachezaji wengi hutolewa hatua za mwanzo, wangefanikiwa kusonga mbele na viongozi wangezidi kujikusanyia kitita cha posho kila wakati. Huu ndio muda wa kujirudi, kukaa chini na kutafakari kama taifa, ili ndoto ile izaliwe upya.
Mafanikio wenye Olimpiki hayatakuja kwa kushangilia watu saba tu London, ambao pia hawakupata maandalizi ya kutosha.
Haikushangaza kumsikia na kumsoma Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui akisema hawatarajii wachezaji kufanya vizuri.
Katika uchache wao, wakifanya vizuri ingekuwa faraja, lakini bado ujumbe muhimu wa kufikisha na kufanyiwa kazi ni wa kujenga upya misingi na zaidi kujenga utamaduni safi.
Mazingira yamechafuka sasa Tanzania, kwa sababu watoto hawakuzwi tena katika maadili na miiko inayotakiwa ili wafanikiwe.
Sinema za uzalendo zimechukuliwa na ‘visinema’ vingi vya mambo machafu kwenye mikahawa ya mitandao ya jamii, televisheni majumbani na sasa katika simu za mkononi.
Picha za mambo ya ngono, muziki uliojaa maneno yasiyo na maadili ndivyo vinawalevya watoto waliotakiwa kukuzwa ili leo watambe Stratford, London na kwingineko.
Imekuwa vigumu kupata zaidi ya wanamichezo saba kwa sababu ya mchanganyiko wa mambo haya – viongozi hawana muda wa kuvikuza vipaji vya wengi walio pembezoni, hivyo wameishia kwenye mambo machafu.
Ile ari ya Ujamaa na Kujitegemea imetibuliwa na ubepari na uhuria wa soko ambao umesambaza kila aina ya bidhaa chafu na kupasua mtandao wa umoja chini ya utamaduni wa kweli wa mwana wa Kitanzania.
Utukufu wa mafanikio ya Mtanzania katika michezo na utamaduni hauonekani tena katika medali za Olimpiki ya Athens, Beijing, Stratford wala hakuna anayeifikiria Rio de Janeiro miaka minne ijayo.
Ni fahari ya waliopewa dhamana kuongeza utajiri wao, kumalizia majumba yao, kutunisha akaunti zao kwa fedha za kukuzia vipaji.
Hakuna tena soni katika kuuza viwanja vya kuchezea watoto kwenye miji na vijiji vya Tanzania, kwa sababu imegeuka fursa ya walioaminiwa kujipatia fedha.
Nani ataitangaza tena fahari ya Mlima Kilimanjaro, visiwa vya karafuu vya Zanzibar na hifadhi za Ngorongoro na Serengeti ikiwa hakuna anayeona uchungu na idadi hii ndogo ya washiriki wetu Olimpiki?
Miaka 50 baada ya uhuru ambayo Watanzania wameitambia kuwa na mafanikio, ni wachache mno wanaotumia nafasi zao, ubunifu na jitihada za wengine kufanikisha michezo.
Lakini pia, ni muhimu kutambua kwamba, mchezaji mzuri si lazima aje kuwa kocha bora, na hii imethibitika kisayansi kwenye ndani na nje ya nchi.
Ni katika msingi huo, naona kwamba kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kuiletea Tanzania medali za fedha kutoka Olimpiki, si tiketi ya wawili hao kuwa viongozi wa michezo.
Ndiyo kusema kwamba pamoja na medali zao, wao ni sehemu ya udhaifu wa uongozi unaopigiwa kelele. Bayi ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania wakati Nyambui ni Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania.
Ipo haja kwa wadau kutafakari zaidi maana ya uongozi, kupima na kuchagua kwa uangalifu zaidi, badala ya kuchukulia kirahisi tu kwamba wote waliofanya vyema kwenye mchezo fulani wanafaa kuongoza.
Katika lile suala zito kuchukua maamuzi magumu, nadhani hakuna haja ya kupoteza muda, ambapo wawili hao binafsi wakiamua kujitazama wataona wamewakwaza Watanzania.
Hii ni kwa sababu wameshindwa kuwarithisha wengine vipaji vyao vya riadha. Ingekuwa mchezaji mzuri anageuka kiongozi mzuri, tangu washike nafasi hizo Tanzania ingepata medali nyingi za dhahabu kwenye Olimpiki.
Kwa kuwa uongozi ni kupokezana kijiti na lazima anayepokea awe na uwezo, utashi wa kufanya kazi husika, nguvu ya kuhimili mitikisiko na kasi ya kuwashinda wengine na kupata medali, watoe vijiti kwa wengine.
Ieleweke kwamba lazima viongozi wa kweli wafanye maamuzi magumu, iwe ni katika kuleta mafanikio wakiwa madarakani au kung’atuka wanapoona hawaleti matunda yanayotakiwa.
Nakumbuka nikiwa mwajiriwa wa Idara ya Mifugo mkoani Dodoma, Ofisa Elimu wa Mkoa wakati huo, Mama Cecelia Shirima alinitumia kutafuta vipaji, kuvikuza na kuviendeleza.
Mama Shirima alichukua hatua hiyo kwa kutambua mchango wangu  katika  maendeleo ya Mpira wa Wavu (Volleyball).
Ulikuwa uamuzi mgumu, kwa sababu alifanya kile ambacho hakuna aliyekuwa amejaribu, na hakujua athari zake, lakini alihisi mafanikio na utimilifu wa ndoto ya mkoa kimichezo.
Kwa kwenda kinyume na utaratibu wa kawaida wa kazi ambao umegeuka na kuwa kituko cha business as usual, alihatarisha nafasi yake, maana ilitakiwa wakufunzi wawe waajiriwa wa wizara.
Uamuzi huo mgumu haukuwa bure, ulilipa, kwa sababu hatimaye Mkoa wa Dodoma ulikuwa Bingwa wa Umitashumta kwa miaka sita mfululizo.
Tena sehemu kubwa ya timu iliundwa na wachezaji kutoka shule moja ya msingi ya wilayani Kondoa, ikiitwa Mirambo! Je, nani amerudi Kondoa kujua siri ya mafanikio haya?
 Mkoa ulipata sifa kubwa kwa mafanikio yale, na vijana nao wakapata nafasi ya kuijua nchi yao, kwa maana ya kusafiri mikoani, walipopelekwa kwenye mashindano kama ya Bonite.
Tunahitaji Viongozi wenye uwezo na uthubutu wa kutoa maamuzi magumu hata kama yatawagharimu, lakini kwa faida ya wananchi na Tanzania yao.
Endapo Kenya wanafanya vizuri kwenye michezo mingi, kwa nini tusiwatumie Wakenya kutusaidia kutengeneza mfumo mzuri wa michezo utakaokuwa endelevu na kutupatia mafanikio, hasa kwenye riadha?
Tunahitaji viongozi wa aina ya akina Mama Shirima wengi, vinginevyo Tanzania haitafanikiwa kwenye michezo, bali itabaki imesinzia.
 Medali za Olimpiki zitabaki ndoto ikiwa Tanzania haitasafisha nyumba yake – kwa wadau kuondoa woga, ubinafsi na kuacha kula vilivyotengwa kwa ajili ya watoto wa Olimpiki.
Uozo unaongezeka kwa sababu kadiri watoto wanavyoongezeka katika ardhi kubwa ya Tanzania, ndivyo wanavyoachwa kuogelea kwenye uchafu wa pombe na ngono.
Mbaya zaidi ni kwamba vipo vyombo vya habari ambavyo msingi wa kuanzishwa kwake duniani ni kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha.
Ndivyo vinashiriki kuwatumbukiza wana wa Tanzania kwenye shimo la kina kirefu kwa ukosefu wa maadili. Wanazeeka kabla ya muda wao, hivyo ni ndoto za mchana kuwaona wakikuza vipaji vyao na kutamba ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Wataendelea kuachwa katika hali hiyo hadi pale viongozi watakapoona busara ya kutokimbilia Beijing, London na Rio de Janeiro kwa mashindano huku wanamichezo wenyewe wakiwa bado Bagamoyo.
Olimpiki iliyozinduliwa Ijumaa kwa sherehe ya Pauni milioni 27 inayotarajiwa kukuza uchumi wa nchi mwenyeji kwa kiasi kikubwa ni kitu tofauti kwa Tanzania.
Fashifashi zilizowaka angani usiku ule na kupokewa kwa vifijo na wakazi wa London na wageni wake ziliizamisha Tanzania kwenye deni kubwa zaidi, maana miaka inaongezeka tangu ing’are.
Nani atahangaika tena kukuza kipaji chake cha michezo ikiwa watoto wanashuhudia sasa wasiofanya kazi wakifaidi maisha? Wanafuata mkumbo na tabia hiyo isipokomeshwa isiwe ajabu ushindani wa nchi kupungua zaidi.
Mazoea yanayojengeka yanaharibu picha ya Tanzania, fahari ya waasisi wake waliorithisha kabla ya kuondoka. Tanzania iseme wazi ‘basi’ kwa waporaji wa watoto hawa.
Vipaji visidumazwe kwa uchu wa fedha walio nao viongozi wachache wanaofikia hatua ya kutafuna fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya kukuza vipaji na kuandaa timu.
Hizi ni zama za kurejea kwenye ndoto nzuri ya Tanzania. Kuiona fahari yake kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki na kutwaa medali kwenye Olimpiki na mashindano mengine.
Hakuna tena muda wa kupoteza, hivyo basi, ujenzi wa ndoto hiyo uanze sasa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version