Menu
in , , ,

NANI ATAKUWA MENEJA WA KWANZA KUTIMULIWA EPL MSIMU HUU?

Tanzania Sports

Ligi Kuu ya England inaendelea kupamba moto ikiwa inaingia kwenye mzunguko wa tano wikiendi hii. Baadhi ya timu tayari zimejikuta zikipata matokeo mabaya mapema kinyume na malengo ya timu husika kwa msimu huu.

Pengine hili linaweza kuwaweka mameneja wa timu hizo kwenye hatari ya kutimuliwa ndani ya wiki chache zijazo kama mienendo ya timu hizo haitabadilika na kuziridhisha bodi za timu husika.

Msimu uliopita Neil Warnock ndiye aliyekuwa meneja wa kwanza kutimuliwa baada ya Crystal Palace kumfungashia virago Desemba 27 mwaka jana baada ya kupokea kipigo cha 3-1 kutoka kwa Southampton na kujikuta akiiacha timu kwenye ukanda wa kushuka daraja.

Hii hapa chini ni orodha ya mameneja wanne ambao wameuanza vibaya msimu huu wa EPL. Timu zao zipo katika nafasi mbaya kulingana na hadhi au/na malengo ya timu husika msimu huu. Huenda tayari wapo kwenye hatari ya kutimuliwa wakati wowote.

DICK ADVOCAAT – Advocaat aliingia kwenye kibarua katika klabu ya Sunderland kama kocha wa muda Machi mwaka huu baada ya Gus Poyet kutimuliwa kutokana na matokeo mabaya. Mwezi Juni akateuliwa kama kocha wa kudumu. Huenda na yeye yakamtokea kama ya huyo meneja wa kabla yake msimu huu. Sunderland yenye alama 2 ipo chini kabisa ya msimamo wa EPL baada ya kufungwa michezo miwili kati ya minne na kuambulia sare mbili. Ni wazi kuwa kibarua cha meneja huyo kinaweza kuota nyasi wakati wowote ingawa alikuwa shujaa wa timu hiyo msimu uliopita kwa kuiepusha kushuka daraja baada ya kuichukua alipotimuliwa Poyet.

JOSE MOURINHO – Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Mourinho hana rekodi ya kutimuliwa. Lakini msimu huu mwenendo wa Chelsea, timu anayoifundisha si mzuri kiasi cha kupelekea wengi kutabiri kuwa huenda atatimuliwa msimu huu. Chelsea ipo katika nafasi ya 13 ya msimamo wa EPL ikiwa na alama 4. Imeshinda mchezo mmoja tu na kutoa sare moja kati ya michezo minne iliyocheza mbaka sasa. Unaweza kudhani kuwa hawezi kutimuliwa kwa kuwa aliipatia timu hii taji la EPL kwa kishindo msimu uliopita. Lakini ikumbukwe kuwa Roberto Di Matteo alitimuliwa miezi sita baada ya kuiwezesha timu hii kushinda taji la Ligi ya Mabingwa 2012.

LOUIS VAN GAAL – Imepita misimu miwili Manchester United ikijikuta inashindwa angalau kuukaribia ubingwa wa EPL. Msimu huu ni wazi kuwa mwenyekiti, bodi wanachama na washabiki wa Manchester United hawapo tayari kushuhudia wakiukosa ubingwa wa EPL kwa msimu wa tatu mfululizo. Kiuhalisia kikosi cha United chini ya Van Gaal bado hakijaonyesha ubora unaotosha kushinda taji la EPL. Wiki iliyopita timu hii ilipewa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Bafetimbi Gomis na wenzie. Pengine kesho watakutana na kipigo kingine kutoka kwa Liverpool. Hilo likitokea nafikiri Luis Van Gaal atakuwa anahesabiwa siku Old Trafford.

BRENDAN RODGERS – Rodgers ametumia zaidi ya paundi milioni 65 kusajili wachezaji saba msimu huu pekee. Wiki iliyopita aliishuhudia timu yake Liverpool ikikutana na kichapo cha 3-0 nyumbani dhidi ya West Ham. Kwa sasa timu yake ipo kwenye nafasi ya 7 ikiwa na alama 7. Kesho Jumamosi atakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Manchester United ya Luis Van Gaal ambayo ilimfunga michezo yote miwili aliyocheza nayo msimu uliopita. Msimu uliopita alishindwa kuipeleka timu hii kwenye nafasi nne za juu lakini hakutimuliwa. Nafikiri ni kutokana na mafanikio aliyokuwa ameyapata msimu wa nyuma alipomaliza kwenye nafasi ya pili.

Je unadhani kuna watakaotimuliwa kutoka kwenye orodha hii?. Je nani atakuwa wa kwanza kufungashiwa virago?!

Written by Kassim

Exit mobile version