*Rio Ferdinand ajiunga QPR
*Khedira, Remy bado utata
WAKATI Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani, Philip Lahm (30) ameamua kuachia ngazi baada ya kulipatia taifa ubingwa wa dunia, beki wa kati wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand (35) amejiunga na Queen Park Rangers (QPR).
Lahm wa Bayern Munich anayecheza nafasi ya beki na kiungo, ametumikia taifa lake mara 113 na sasa ataelekeza nguvu kwa klabu yake, ambako muda mfupi kabla ya kuanza fainaliz a Kombe la Dunia nchini Brazil alisajili mkataba mpya hadi 2018.
Ferdinand kwa upande wake, anaungana na mwalimu wake wa kwanza akiwa West Ham, Harry Redknapp na anasema anatak kuhakikisha QPR wanajiweka barabara kwenye Ligi Kuu, walikorejea msimu huu baada ya kushuka msimu uliopita.
Ferdinand alianzia soka ya kulipwa West Ham kabla ya kwenda Bournemouth kwa mkopo 1996 akakaa hadi mwaka uliofuata aliposajiliwa na Leeds United. Man United walimsajili kwa dau lililovunja rekodi 2002 alikocheza hadi mwaka huu.
Alichezea pia Timu ya Taifa ya England tangu 1997 na ameichezea mara 81. Alikuwa pia mchezaji wa timu za vijana tangu 1996.
QPR pia wamesajili beki mwingine wa kati kutoka Cardiff, Steven Caulker (22) aliyewika sana msimu uliopita na sasa atafanya kazi sambamba na Ferdinand kuipa ngome yao uhai. Caulker amepata kuchezea timu ya taifa ya England.
Demba Ba wa Chelsea (29) amejiunga rasmi na Besiktas ya Uturuki kutoka Chelsea huku Mathieu Debuchy (25) wa Newcastle akikamilisha usajili wake Arsenal, ambako atakuwa beki wa kulia badala ya Bacary Sagna aliyehamia Manchester City.
Debuchy ni mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa anayepewa kipaumbele kabla ya Sagna. Newcastle nao wamejiimarisha wakiziba pengo la Debuchy kwa kumsajili Daryl Janmaat (24) wa Feyenoord na Timu ya Uholanzi.
Real Madrid wamekamilisha usajili wa Toni Kroos kutoka Bayern Munich, huku Yaya Toure akikataa maombi ya Manchester United kumsajili baada ya kudai wamesikia hataki tena kubaki kwa jirani zao, Manchester City.
Hata hivyo, ManCity wanadaiwa kuhangaika kumsajili kiungo Ross Barkley wa Everton ili kuziba nafasi ya Toure iwapo ataendelea kutikisa kibiriti na kuondoka, kwani inadaiwa anaweza kwenda Paris Saint-Germain (PSG) ila mwenyewe amesema anabaki Man City.
Arsenal inadaiwa kusitisha mbio za kumsajili kiungo wa Real Madrid, Sami Khedira baada ya kudai mshahara mkubwa mno, na sasa Chelsea wanatafakari, japokuwa inadaiwa Monaco wanaomilikiwa na tajiri wanataka kumtwaa. Khedira (27) yupo katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake Bernabeu.
Arsene Wenger sasa anaelekeza macho yake kwa kiungo wa Southampton, Morgan Schneiderlin, huku Redknapp wa QPR akidokeza kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa Arsenal kumpata mshambuliaji wake, Loic Remy, kwani anataka kucheza soka ya ubingwa wa Ulaya.