Menu
in , , ,

MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU BARA

 

 

SIMBA, YANGA, AZAM ZAENDELEA KUPETA

 

Vigogo watatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara wameendelea kushinda michezo yao kwa mara ya pili mfululizo. Simba SC wameendeleza ubabe wao msimu huu kwenye dimba la Mkwakwani baada ya kuwafunga Mgambo JKT mabao mawili kwa sifuri.

Wekundu hao wa Msimbazi waliuanza mchezo huo kwa mashambulizi ya hatari ambapo kiungo chipukizi Said Ndemla alihusika zaidi na mashambulizi hayo ya mapema. Kwenye dakika ya pili ya mchezo Ndemla alipiga krosi nzuri ambayo iliokolewa kwa kichwa na walinzi wa Mgambo na kuzaa kona.

Kona hiyo ya mapema ilipigwa na Mohamed Hussein lakini haikuweza kutengeneza nafasi ya bao. Dakika chache baadae nahodha Mussa Hassan Mgosi alipolea pasi kutoka kwa Peter Mwalyanzi na kupiga shuti lililogonga mwamba na kurudi ndani ya uwanja.

Kwenye dakika ya 27 ndipo mashambulizi ya Simba yalipoweza kuzaa bao baada ya Mohamed Hussein kupiga krosi iliyotiwa wavuni na Justice Majabvi. Simba waliendelea kuonyesha makali lakini hawakuweza kupata bao lingine na kipindi cha mapumziko kikafika Simba wakiongoza kwa bao moja kwa sifuri.

Kwenye kipindi cha pili cha mchezo Mgambo JKT walionekana kuamka kwa kiasi fulani lakini jitihada zao hazikuweza kuzaa matunda. Hamis Kiiza akafumania nyavu za dimba la Mkwakwani kwenye dakika ya 73 kwa mara ya pili msimu huu na kuipatia Simba bao la pili.

Jijini Dar-es-salaam ndani ya Uwanja wa Taifa mabingwa watetezi Yanga waliwaadhibu Tanzania Prisons kwa mabao matatu kwa sifuri na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Vijana hao wa Jangwani waliuanza mchezo wao kwa kasi kwenye dakika kumi za mwanzoni lakini waliendelea kufifia kadri muda ulivyozidi kwenda.  Hata hivyo halikupita nusu saa baada ya mchezo kuanza Mbuyu Twite akawapatia bao la kuongoza.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mapumziko hakijapulizwa mshambuliaji Amis Tambwe aliipatia Yanga bao la pili. Dakika ya 58 ya kipindi cha pili ikamshuhudia James Josephat wa Prisons akilimwa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi Simon Msuva kwenye eneo la hatari na Yanga wakapewa penati ambayo iliwekwa wavuni na Donald Ngoma.

Azam nao katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Kambarage jijini Shinyanga waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Stand United. Mabao hayo yalifungwa na mshambuliaji kutoka Kenya, Allan Wanga na kiungo wa zamani wa Yanga Frank Domayo.

Matokeo ya michezo mingine yalikuwa; Mwadui 2 – African Sports 0, Mbeya City 3 – JKT Ruvu 0, Majimaji 1 – Kagera Sugar 0, Ndanda FC 1 – Coastal Union 0 na Mtibwa Sugar waliiadhibu Toto Africans 2-1 jijini Mwanza.

Written by Kassim

Exit mobile version