Menu
in , , ,

Mzunguko wa 14 wa epl, mtamu..

*Chelsea waua Man City

*Aguero, Fernandinho wala kadi nyekundu

*Arsenal wagawa kichapo kwa West Ham

*Liverpool washindwa kwa Bournemouth

Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeleta makubwa kwenye
ulimwengu wa soka kwa Chelsea kuwafunga Manchester City katika mechi
iliyokuwa kama vita na kushuhudia wachezaji wawili muhimu wa City
wakipewa kadi nyekundu, huku Arsenal wakiwapiga West Ham mabao matano.

Ilikuwa mechi ya nane kwa Chelsea kushinda mfululizo katika msimu huu,
wakiwa walianza kuamka baada ya kutunguliwa 3-0 na Arsenal. Man City
walifungwa 3-1 na kudhalilishwa nyumbani kwao Etihad kwenye mechi
iliyomalizika kwa fujo huku Sergio Aguero na Fernandinho wakipewa kadi
nyekundu kwenye muda wa majeruhi.

Vijana wa Antonio Conte walionesha dhamira ya wazi ya kutaka
kulichukua kombe msimu huu licha ya kwamba City ndio walianza kupata
bao kwa Gary Cahil kujifunga bao kwa mpira wa mkengeuko uliompiga
kutokana na majalo ya Jesus Navas na kumshinda Thibaut Courtois.

City walitawala mpira kwa asilimia kubwa na dakika ya 56 Kevin de
Bruyne alikosa bao akiwa ndani ya yadi sita kwenye goli kwa
kuugongesha mpira wa Navas kwenye mtambaa wa panya. Diego Costa
alisawazisha bao dakika ya 60 baada ya kumzidi nguvu Nicolas Otamendi
na wakaongoza dakika 10 baadaye pale Willian alipomzidi maarifa kipa
Claudio Bravo.

Eden Hazard alifunga kitabu cha mabao kwa bao zuri baada ya kumshinda
kasi Aleksandar Kolarov na kuwahakikishia Chelsea pointi tatu muhimu.
Hayo ndiyo majibu kutoka kwa Conte aliyemwacha Pep Guardiola wa City
akiwa na maswali. Guardiola aliomba radhi kwa wachezaji wake kufanya
rabsha.

City sasa wanajiandaa kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi
ya Celtic Jumanne hii kisha wakifuatiwa na mechi ya EPL dhidi ya
mabingwa watetezi, Leicester Desemba 10. Mechi ijayo kwa Chelsea ni
dhidi ya West Bromwich Albion Desemba 11. Kwa ushindi huo Chelsea
wamefikisha pointi 34 huku City wakiwa nazo 30.

ARSENAL WATOA MAUAJI YA SHARUBELA
Mtu hatari sana, huyu....

Arsenal wameonesha nia yao ya kutwaa ubingwa wa England kwa ushindi
mnono wa mabao 5-1 dhidi ya West Ham, ambapo wamepanda hadi nafasi ya
pili kwa kufikisha pointi 31.

Alexis Sanchez alionesha kiwango kizuri kwa kufunga mabao matatu – hat
trick kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa London, nyumbani kwa West Ham
ambako wenyeji wamekuwa hawafanyi vyema.

Alikuwa kiungo Mjerumani, Mesut Ozil aliyeanza kufunga bao kwa shuti
la kwanza la timu yake kulenga goli kwenye mchezo huo baada ya kosa la
Angelo Ogbonna na kumwezesha Sanchez kumiliki mpira na kumpasia Ozil.

Hammers walitishia kuwasawazisha The Gunners baada ya kipindi cha
kwanza kabla ya Sanchez kuibuka tena na kutikisa kamba, akipita
kiufundi Darren Randolph. Raia huyo wa Chile aliongeza bao la pili
dakika nane baadaye kwa mpira wa kima cha nyoka.

Hiyo ilikuwa muda mfupi kabla ya Andy Carroll kuingia akitokea benchi,
ikiwa ni mechi yake ya kwanza tangu Agosti 18 kutokana na kuwa
majeruhi. Alikaribia kufuna akipokea mpira wa adhabu ndogo wa Dimitri
Payet lakini akagonga mwamba wa goli. Arsene Wenger aliogopa tisho la
kurejea kwa mchezaji huyo hivyo kumpumzisha beki wa kulia, Carl
Jenkinson na kumhamishia hapo Gabriel.

Matumaini yoyote ya West Ham kurudi mchezoni yalikwisha baada ya Alex
Oxlade-Chamberlain kufanya kazi nzuri na kufunga bao Kabla ya Sanchez
tena kufunga na kuhitimisha karamu ya mabao.


LIVERPOOL WAZIDIWA, MAN U SARE TENA

Liverpool wameshindwa kujisogeza katika nafasi ya pili baada ya
kukubali kufungwa 4-3 na Bournemouth kwenye mechi ambayo Liver
walikuwa wakiongoza kwa 2-0 hadi nusu ya kwanza ya mchezo na ilifika
dakika 15 Kabla ya mechi kumalizika wakiwa mbele kwa 3-1.

Hii ilikuwa moja ya mechi ambazo timu zimepambana kweli kweli kuondoka
kutoka nyuma kwa mabao na kuja kuibuka kwa ushindi, ambapo bao la
ushindi la Cherries lilipatikana katika dakika ya 93 kupitoa kwa
Nathan Ake.

Sadio Mane aliwafungia Liverpool bao la kuongoza baada ya kudhibiti
vyema mpira wa Emre Can kisha Divock Origi akampita kipa Artur Boruc
na kutikisa kamba. Bournemouth walimwingiza Ryan Fraser dakika ya 55
na kubadili mchezo, kwani sekunde kadhaa baadaye James Milner
alimwangusha kwenye eneo la penati na Callum Wilson akafunga penati
iliyotolewa. Can aliweka bao la tatu kwa mkwaju wa umbali wa yadi 20
lakini Fraser akafunga bao lake la kwanza EPL dakika ya 76.

Beki wa kati wa Bournemouth, Steve Cook aliwasawazishia Cherries Kabla
ya Ake kucheka na nyavu kutokana na kipa Loris Karius alipoutema mpira
wa Cook. Kwa matokeo hayo Liverpool wanabaki nafasi ya tatu wakiwa na
pointi 30 wakati Bournemouth wamepanda hadi ya 10 wakiwa na pointi 18.

Kwa upande wa mechi baina ya Everton na Manchester United, Leighton
Baines aliwanusuru wenyeji kukosa pointi zote kwa kufunga penati
dakika za lala salama kutokana na Marouane Fellaini, kucheza rafu.

Fellaini, mchezaji wa zamani wa Everton, aliingia akitoka benchi
dakika ya 85 ikiwa ni mechi yake ya 100 hapo United, lakini kitu pekee
cha kwanza alichokifanya na cha kukumbukwa ni rafu dhidi ya Idrissa
Gueye na ikawagharimu United.

Kocha Jose Mourinho alitetea kumwingiza, akisema aliamua hivyo
kutokana na urefu wake ili awakabili Everton ambao wamebadili mbinu na
badala ya mchezo wa pasi sasa ni kubwatua mpira moja kwa moja golini,
akilalamika kwamba baadhi ya timu zimekuwa zikijihami na wachezaji
wote 11 na kutegea tu kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

Bao la United lilifungwa na Zlatan Ibrahimovic dakika ya 42. Kwa sare
hiyo United wamepanda hadi nafasi ya sita baada ya kufikisha pointi 21
huku Everton wakiwa wa nane na pointi zao 20.

MATOKEO MENGINE EPL WIKIENDI HII

Katika matokeo mengine wikiendi hii, Crystal Palace wa Alan Pardew
aliyekuwa akihofia kibarua chake walifufuka kwa kuwafunga Southampton
3-0 katika matokeo ya kushangaza. Stoke waliwalalia Burnley 2-0,
Sunderland wakaondoka mkiani kwa kuwanyuka mabingwa watetezi,
Leicester 2-1, Tottenham Hotspur wakawakandika Swansea 5-0 na West
Bromwich Albion wakawazidi nguvu Watford kwa 3-1.

Liverpool wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 30 wakati Spurs
wanashika nafasi ya tano kwa pointi 27 nyuma ya Man City. Mkiani wapo
Swansea wenye pointi tisa tu, Hull na Sunderland wenye 11 kila mmoja.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version