Unavyoweka rehani Kombe la Dunia la Vilabu
Kombe la Dunia la Vilabu ni mradi kipenzi wa rais wa FIFA, Gianni Infantino. Mashindano haya yanatarajiwa kufanyika nchini Marekani majira ya kiangazi mwaka ujao, lakini kabla ya kuanza yanaibuka maswali mengi yasiyo na majibu. Licha ya maswali hayo na hoja zinazoleta mzozo, FIFA inaonekana kuwa na nia ya kuendeleza mashindano haya yenye utata.
Baadhi ya vilabu vilivyofuzu kwa mashindano hayo vimeanza kuishinikiza FIFA itoe ahadi za kutumia akiba yake kugharamia zawadi za fedha kwa washindi, huku kiasi hicho cha zawadi kikiwa hakijathibitishwa na kuwekwa wazi. Vilabu vikubwa vinatarajia kuingiza hadi dola milioni 50 (£37m), kufuatia ahadi za awali kutoka kwa Infantino kwamba vingeweza kupata hadi dola milioni 80 (£60m). Hata hivyo, kama fedha hizo zitatoka kwenye mfuko wa akiba ya FIFA, hatua hiyo inatarajiwa kukosolewa vikali. Ukosoaji utajielekeza kwenye haki, kwamba sio haki kwa vyama wanachama kuvilipa vilabu tajiri zaidi. Kwa upande wake, FIFA imekuwa haiipi uzito hoja hiyo, ikiendelea na matararisho yake, huku tangazo rasmi la mashindano hayo likitarajiwa kutolewa ndani ya wiki chache zijazo.
Yapo matarajio kuwa FIFA itapata msaada wa kifedha kupitia uhusiano uliopo wa Infantino na Saudi Arabia pamoja na kampuni ya mafuta ya Aramco. Lakini, hilo bado halijathibitishwa rasmi. Wengine wanasema kuwa Saudi Arabia inaweza kuchelewa kufanya hivyo mpaka pale uamuzi kuhusu Kombe la Dunia la 2034 utakapofanyika na kuridhiwa.
Kwa hali ilivyo sasa, mjadala kuhusu namna Kombe la Dunia la Vilabu litakavyofadhiliwa ni miongoni mwa simulizi muhimu za msimu huu wa soka, licha ya kwamba suala hilo bado linaendelea kujadiliwa kwa siri ndani ya FIFA. Kama FIFA itathibitisha kutoa ama kuwepo kwa kiwango cha fedha kinachoweza kushawishi vilabu kuchukulia mashindano haya kwa uzito sawa na Ligi ya Mabingwa Ulaya, huenda mashindano haya yakawa yenye mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa soka. Na hiyo ndiyo nia na lengo la Infantino. Iwapo Saudi Arabia itajitokeza kuwa mfadhili, hilo linaweza kufanikiwa na kuifanya nchi hiyo kuwa sehemu muhimu ya miundombinu ya mchezo huo, kama ilivyoshuhudiwa kwenye michezo mingine ya masumbwi na gofu.
Hata hivyo, kwa sasa mashindano hayo ya Kombe la Dunia la vilabu yanakumbwa na changamoto lukuki hasa kuhusu muundo wake badala ya mabadiliko yake ya kuliboresha. Wakati vilabu vikitarajia pesa nyingi kwa upande mmoja, upande mwingine kuna shinikizo kutoka kwa mashirikisho ya ligi za Ulaya na vyama vya wachezaji, kukiwa na vitisho vya kuchukua hatua za kisheria kuhusu uwepo wa ongezeko la mechi kwenye kalenda ya soka.
Kwenye hili FIFA inaweza kusema mbona mashirika hayo hayakulalamika dhidi ya kupanuliwa na kuongezeka kwa mechi za Ligi ya Mabingwa ya UEFA, lakini hoja ni kwamba kwenye mabadiliko ya mfumo wa Ligi ya Mabingwa ya UEFA, wadau walishirikishwa kikamilifu katika hatua zote za mipango ya mabadiliko hayo. FIFA inatupiwa lawama nyingi kwenye hili kwa sababu imeonekana kufanya maamuzi haya “bila ushirikiano”, au kushirikisha wadau kwa upana wake, jambo linaloonekana kujirudiwa mara kwa mara.
Hata Miji inayotarajiwa kuwa wenyeji wa mashindano ya mwakani ilithibitishwa Ijumaa iliyopita, ikiwa ni miezi tisa tu kabla ya kuanza kwa mashindano hayo Juni 15 nchini Marekani. Bado hakuna uwazi zaidi kuhusu wadhamini, vituo vya kurushia matangazo au zawadi za fedha kwa washindi, ingawa FIFA inaonekana iko karibu kutangaza viwanja vitakavyochezewa mechi za mashindao hayo. Hayo yakiendelea, shughuli kuhusu ratiba ya mashindano hayo ya mwakani na kulionyesha kombe litakalowania inatarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.
Kwa FIFA, hili ni suala muhimu kwa ajili ya soka la kimataifa. Hata wakosoaji wa mashindano haya wanakubali kuwa wazo la kupanua Kombe la Dunia la Vilabu ni wazo jema, hasa kwa kuzingatia haja ya kunufaika kwa wengi kupitia utajiri mkubwa wa soka la Ulaya Magharibi. Mashindano haya yanaweza kuwa chombo muhimu cha kusukuma mbele mabadiliko hayo.
Hata hivyo, wakosoaji hao wanakosoa njia iliyotumika na inayotumika kuleta mabadiliko na kufanikisha mashindano haya, kwamba imeongeza maswali mengi zaidi kuhusu malengo ya Infantino. Kuna imani kwamba Infantino anataka FIFA iwe inashiriki kwa namna kubwa kwenye soko la vilabu ambalo linaonekana linavutia uwekezaji mkubwa wa kifedha, hasa kutokana na uzoefu wake akiwa UEFA na namna Ligi ya Mabingwa Ulaya ilivyo na thamani. Wengine wana mtazamo wa kukosoa zaidi, wakidai kuwa hizo ni njama ya Infantino kukusanya fedha zaidi ili kutimiza ahadi zake za uchaguzi kwa vyama vya wanachama wa FIFA.
Licha ya hayo, vilabu vikubwa vya Ulaya bado vinaunga mkono mpango huu na mabadiliko ya mashindano ya kombe la dunia kwa vilabu. Vilabu hivi vinaunga mkono vikiamini ni fursa ya kujitangaza zaidi duniani. Vilabu kama Chelsea, Manchester City, Atletico Madrid, Porto na Juventus vinaonekana kuunga mkono mashindano haya, huku viongozi wa City wakijipanga kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa tayari kwa ajili ya mashindano hayo. Rais wa Chama cha Vilabu vya Ulaya, Nasser Al Khelaifi, pia amesisitiza kuunga mkono.
Vilabu hivi havionyeshi wasiwasi na hofu kuhusu kalenda ya soka, kwani vinadhani mashindano haya ni mbadala wa baadhi ya michuano ya sasa, na yataongeza mechi chache tu kwa vilabu vichache kila baada ya miaka minne. Kuna mtazamo kwamba wakati wa mashindano hayo, timu shiriki hazitakuwa na wakati wa kufanya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, lakini uwepo wa zawadi ya dola milioni 50 ni kivutio na kikubwa kuliko kiasi cha dola kati ya milioni 20-30 zinazoingizwa na timu hizo hasa za ligi kuu England, zinapofanya ziara za maandalizi ya msimu wakati wa kiangazi huko Marekani
Lakini ili vilabu hivi viendelee kuunga mkono, mashindano lazima yaendeshwe vizuri, jambo ambalo halijaonekana bado. Wengi wanaona kuwa kuna ahadi ‘hewa’ licha ya kuwepo kwa miaka mingi ya mazungumzo na wengine wanasema ni siasa za soka. Kwa mfano awali FIFA ilitangaza mikataba ya haki za matangazo yenye thamani ya $5bn (£3.7bn), lakini sasa vilabu vinaonekana kuwa matarajio tofauti, ya kuingiza $1bn (£750m) tu. Warusha matangazo pia hawaoni kama mashindano ya Kombe la Dunia la Vilabu kama “bidhaa ya kuvutia” kuweza kuwekeza fedha nyingi kama vile ambavyo Infantino anataama. Yapo maoni kwamba soka la vilabu vikubwa limefikia ukomo wa mvuto. Na hoja nyingine timu zenye mvuto mkubwa na mashabiki wengin duniani kama Arsenal, Liverpool, na Manchester United kutokufuzu, kunapunguza mvuto.
Hoja nyingine zaidi inayoibuka ni kuhusu FIFA kuacha kuzingatia majukumu yake ya msingi na kuhangaika kutafuta fedha za kuendeshea mashindano haya. Hata kama fedha hizo zikipatikana, wasiwasi ni kwamba asilimia 75 ya mapato yataenda kwa wachezaji ambao tayari ni matajiri na wanalipwa vizuri, huku zawadi za fedha zikitarajiwa kuharibu ushindani kwenye ligi za ndani, kinyume na malengo ya mashindano haya. Kwa sababu timu tajiri, zitakazoshiriki zitaingiza fedha nyingi na itazitumia kwenye kujiimarisha hasa kwenye usajili wa wachezaji kwa misingi ya kanuni za kifedha za FIFA, na hilo kuendeleza kuathiri timu ndogo.
Kuna nadharia kwamba suluhisho hasa eneo la matangazo linaweza kutoka kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia kama itaweza kuipa fedha FIFA, kwa kushirikiana na kampuni binafsi ya uwekezaji binafsi. Kwa ufupi hili linapaswa kufanyika kwa ushirikishaji wa pande nyingi na zenye nguvu. Pamoja na yote na hofu zote zilizoko, ukweli unabaki kwamba mashindano haya hayatafutwa, yataendelea kuwepo kwa sababu athari za kuyafuta ni kubwa kuliko athari za kuyaacha, kwa mfumo na mtindo wowote unaodhaniwa.