`Mzimu` ulioifanya Yanga ishindwe kuitoa timu ya kiarabu katika historia yake ya ushiriki wa michuano ya klabu ya Afrika jana uliendelea kuwatesa mabingwa mara 22 hao wa Bara, baada ya kutupwa nje ya Ligi ya Klabu Bingwa na Zamalek ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1.
Ikiwa ilitoka sare ya bao 1-1 na Zamalek katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita hapa nyumbani, habari kutoka Cairo, Misri zilisema Yanga iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani jana ililala 1-0. Kwa matokeo hayo, Yanga imetupwa nje ya mashindano kwa jumla ya magoli 2-1.
Katika mchezo wa jana uliochezwa kwenye uwanja wa wa kituo cha jeshi nchini humo bila ya kuwa na mashabiki, Zamalek walipata goli lao katika dakika ya 30 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji Ahmed Hossam ‘Mido’ na hivyo kuifungulia Yanga ‘mlango wa kutokea’ kwenye mashindano hayo makubwa zaidi barani Afrika kwa kwa ngazi ya klabu.
Taarifa kutoka Misri zinasema katika mchezo huo kiungo wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili cha mchezo huku pia Zamalek wakipata penalti katika kipindi hicho lakini wakakosa.
Katika mchezo huo, Yanga walijitahidi kuwabana wenyeji wao mpaka dakika hiyo ya 30 ambapo mchezaji aliyekuwa akicheza soka kwenye ligi kuu nchini Uingereza, Mido alipoipatia timu yake goli pekee na kuivusha hatua inayofuata.
Yanga wanatarajiwa kurejea nchini kesho kuwekeza nguvu zote zilizobaki kwenye ligi kuu ya Bara.