Menu
in , ,

Mzambia alivunja rekodi ya Messi zamani

*Ni Chitalu aliyefunga mabao 107 mwaka 1972

*FA ya Zambia sasa yaikaba koo FIFA na CAF

 

Lionel Messi anatajwa kuwa mfungaji wa mabao mengi zaidi kwa mwaka katika historia ya soka, lakini Zambia inasema hapana.

Mshambuliaji huyo wa Barcelona ameshafunga mabao 86 msimu huu, ambapo wikiendi iliyopita alivunja rekodi ya Mjerumani Gerd Muller aliyekuwa na mabao 85.

Rekodi ya Muller ni ya mwaka 1972, ambapo rekodi zimekuwa zikidai kwamba kwa miaka 40 hakuna mchezaji aliyefanikiwa kufunga zaidi ya hayo.

Desemba inapoeleka katikati kabla mwaka haujamalizika, Messi anachukuliwa kuwa mfungaji bora zaidi, huenda akachaguliwa kuwa mchezaji bora pia kwa mwaka huu.

Lakini katikati ya sakata hilo, kimekuja Chama cha Soka cha Zambia na kusema yote hayo si kweli, kwa sababu Mzambia ndiye anashika rekodi kubwa zaidi.

Wanamtaja Godfrey Chitalu kuwa ndiye anashikilia rekodi ya dunia katika soka, kwa sababu alitikisa nyavu mara 107 kwa mwaka.

FA ya Zambia inasema kwamba mshambuliaji wao huyo alifanya mambo hayo mwaka 1972, wakati anachezea timu ya Kitwe United.

Chama hicho kinashangaa ni kwa vipi rekodi za Muller ndizo zimechukuliwa na za Chitalu ambaye sasa ni marehemu kuachwa. Hakikubali leo hii pia, kinaposikia Messi ndiye mfungaji aliyevunja rekodi.

Godfrey ‘Ucar’ Chitalu alifanya mambo makubwa uwanjani, na baada ya hapo alipewa tuzo maalumu na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kabla ya kuwa kocha wa timu ya taifa.

Chitalu alifariki dunia kwenye ajali ya ndege iliyotokea kwenye ufukwe wa Gabon na kuua kizazi cha wachezaji wote wa kikosi cha kwanza katika kizazi hicho, mwaka 1993

“Tunayo rekodi hii sisi, imerekodiwa na Chama cha Soka cha Zambia, lakini kwa bahati mbaya haijarekodiwa hivyo katika soka ya kimataifa.

“Hata dunia sasa inapomwangalia Lionel Messi katika rekodi yake kwamba amempita Gerd Muller, hapa kwetu mjadala ni kwamba kwa vipi rekodi ya Chitalu haitumiwi,” anasema msemaji wa tovuti ya Soka ya Laduma.

Zambia imeunda jopo la watu huru kutazama maktaba na kurekodi magoli yote hayo dakika kwa dakika na kukokotoa ni lini, kwenye mechi za mashindano gani na kuanika kila kitu wazi.

Baada ya kazi hiyo kukamilika, rekodi kamili zitatumwa FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kuwaonyesha kwamba rekodi ya Messi si chochote, kwa sababu Afrika ilishaiweka na kuipita miaka 40 iliyopita.

Tayari FA ya Zambia imewasiliana na FIFA kuhusu suala hilo, na FIFA wanasema kwamba nao wanalichunguza ndani kwa ndani.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version