Menu
in , , ,

MWILI WA CONTE UNAONESHA KESHO YAKE

Tanzania Sports

Jana Antonio Conte alirudi kwenye mfumo wake wa msimu uliopita wa
3-4-3, mfumo ambao ulimpa ubingwa lakini msimu huu akawa anautumia
mara chache kwa kuhamia katika mfumo wa 3-5-2.

Jana wakati anautumia mfumo wa 3-4-3, kwenye karatasi ulionekana mfumo
ambao unafanana na mfumo uliompa ubingwa msimu jana, lakini kiuhalisia
kulikuwa na tofauti kubwa sana.

Moja ya sababu ni aina ya wachezaji ambao walikuwepo msimu jana kwenye
mfumo wa 3-4-3 na wachezaji waliokuwepo jana kwenye mfumo wa 3-4-3.

Msimu jana Matic alicheza kama Box to Box midfielder akishirikiana na
Kante katika eneo la katikati mwa uwanja, lakini jana alikuwepo
Bakayoko katika eneo ambalo Matic alikuwepo msimu jana.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya Matic na Bakayoko kwenye kutimiza
majukumu ya Box to box midfielder.

Msimu jana katika ligi kuu ya England , Matic alifanikiwa kutoa pasi
za mwisho saba (7). Matic alikuwa mtulivu kimaamuzi, majukumu yake
alikuwa anayatimiza kwa utulivu, kuanzia jukumu la kukaba alipokuwa
anashuka mpaka chini katika eneo la Chelsea kumsaidia Kante majukumu
ya kukaba mpaka alipokuwa anaenda kwenye box la timu pinzani
kushambulia ambapo alikuwa na uwezo wa kutoa pasi za mwisho na
kutengeneza nafasi za magoli vizuri.

Hii ni tofauti sana na Bakayoko, kwenye kujilinda anatimiza vizuri
majukumu yake, tatizo linakuja pindi timu inaposhambulia, ameshindwa
kuwa mtulivu kama alivyokuwa Matic. Hatengenezi nafasi za magoli kwa
wingi, hana utulivu katika umaliziaji ndiyo maana anakosa nafasi
nyingi za magoli.

Hata mipira mingi anapoteza pindi timu inapohitaji kuwa na mipira,
mfano jana kabla ya kupigwa kadi nyekundu alikuwa amecheza dakika 30,
ndani ya dakika hizo 30 alipoteza mipira mara 7.

Hii ndiyo tofauti ya kwanza ya mfumo wa 3-4-3 wa msimu jana na 3-4-3
ya mechi ya jana, pili jana Hazard kacheza kama false 9, msimu jana
mtu aliyesimama mbele alikuwa Diego Costa ambaye alikuwa mshambuliaji
halisi wa kati ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga pamoja na
kutengeneza nafasi za kufunga.

Jana Hazard alikuwa amezungukwa na kina Pedro pamoja na Willian,
wachezaji ambao walikuwepo hata msimu jana kwenye mfumo wa 3-4-3
lakini tofauti yao ni kwamba msimu jana walikuwa kwenye kiwango
kizuri, msimu jana Pedro alifanikiwa kufunga magoli 9 kwenye ligi kuu
ila mpaka sasa hivi ukijumuisha magoli ya Pedro na Willian ya msimu
huu kwenye ligi kuu ya England, kwa pamoja wote wawili hawafikishi
idadi ya magoli aliyofunga Pedro msimu jana.

Jana Hazard alikuwa anaonekana peke yake akipambana kule mbele huku
akipata msaada hafifu kutoka kwa Pedro na Willian.

Je kulikuwa na ulazima kwa Conte kumwanzisha Olivier Giroud?

Hapana shaka kulikuwa na ulazima, Olivier Giroud anahitaji muda
kutendea haki ya krosi za Chelsea.

Msimu huu Chelsea ni timu ya pili ambayo imepiga krosi nyingi ikiwa
imepiga krosi 393 nyuma ya Manchester United iliyopiga krosi nyingi.

Kati ya huduma ambayo Olivier Giroud huifurahia ni mipira ya juu,
ambapo mpaka sasa katika miaka yake mitano katika ligi kuu ya England
amefanikiwa kufunga magoli 27 kwa kichwa.

Kulikuwa na ulazima wa kumwanzisha mapema ili kupokea huduma hii
ambayo Chelsea inaonesha wako vizuri kwenye utoaji.

Je, Zappacosta alistahili kuanza eneo la Marcus Alonso?

Hapana shaka jana upande wa kushoto kulikuwa na upungufu wa krosi
nyingi kutokana na Zappacosta kucheza kama wingback left, eneo ambalo
tumezoea kumuona Marcus Alonso akilitumikia kwa ufasaha mkubwa na jana
alikosekana kwa kiasi kikubwa na Chelsea walihitaji huduma yake katika
mchezo wa jana.

Andreas Christensen jana kaanzia benchi, je David Luiz alifanikiwa
kukaa vizuri katika eneo la nyuma?

mara ya mwisho kwa David Luiz kuanza katika kikosi cha Chelsea kwenye
ligi kuu ya England ilikuwa October mwaka jana. Jana alionekana
kukosa sharpness kwenye timu kiasi kilichopelekea Chelsea kutengeneza
space eneo la nyuma.

Space ambazo kina Gerard Deulofeu kuzitumia vizuri na kuiadhibu Chelsea.

Eneo la nyuma la Chelsea jana lilikuwa linauwazi sana walipokuwa wanashambuliwa.

Jana Antonio Conte hakuonesha kuhamasisha kama ilivyokawaida yake,
hakuwa anashangilia pindi timu ilipofunga goli, lugha ya mwili wake
ilikuwa inaonesha kuwa muda wowote anaweza asiwe kocha wa Chelsea
tena.

Katika mechi 10 zilizopita Antonio Conte amefanikiwa kushinda mechi
mbili tu, matokeo ambayo yanaonesha kabisa Antonio Conte hali yake ni
mbaya katika timu ya Chelsea.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version