Kwa historia ya mchezo wa soka la ufukweni nchini Tanzania haikuwepo kabisa bali wapenzi wake wachache walikuwa wakiangalia mchezo huo kupitia Runinga kwa nchi ambazo mchezo huo upo kwa miaka mingi.
Siwezi kukupa historia ya mchezo wa soka la ufukweni Tanzania zaidi ya kusema tusubiri miaka ijayo ndio tutakuwa na historia ya mchezo huo kwani tutakuwa tumepata kujua mbivu na mbichi kwa mchezo wa soka la ufukweni,ambalo ndio kwanza limebisha hodi nchini Tanzania.
Hivi karibuni Tanzania ilijitosa katika soka la ufukweni kimataifa ambapo tumeona matunda ya awali baada ya timu hiyo ya Tanzania katika mchezo huo ikiwa chini ya mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars John Mwasasu ikiitupa nje ya mashindano hayo timu ya taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12-9 ambapo Tanzania ilishinda 5-3 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Mombasa Kenya na marudio iliibuka kwa ushindi wa 7-6 na kuweza kufuzu katika hatua ya pili kwa jumla ya 12-9 na itapambana na timu ya taifa ya Misri.
Nionavyo ni mwanzo mzuri sana kwa mchezo huo tena ukiwa ni mgeni sana kwa nchi yetu kwani nilishuhudia pale escape 1 Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano kati ya Tanzania na Kenya ambapo idadi ya mashabiki waliojitokeza walikuwa ni wengi sana na kutoa sapoti kubwa ambapo pengine ilikuwa ndio chachu ya ushindi kwa Tanzania.
Lakini kwa yote hayo napata kujiuliza je kuwepo kwa mashabiki wengi pale escape 1 katika mchezo wa Tanzania na Kenya je ni ugeni wa mchezo huo?,kwa vile hakuna kiingilio? au ni muonekano na mfanano wa soka linalopendwa?,lakini bado nina imani na kuamini kuwa mchezo wa soka la ufukweni una nafasi ya kupenya na kuwa mchezo mkubwa na wenye kupendwa kama kila kitu kitakwenda vile kilivyopangwa.
Pia vyombo vya habari ndio wakati wake kuupa nafasi mchezo huo ili kufahamika kwa wadau na watanzania kwa ujumla kwa kutoa historia yake kwa nchi zingine ambazo mchezo huo umepewa nafasi.
Aidha ukiacha vyombo vya habari pia ni wakati wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF,kujikita katika mchezo huo kwa kuusimamia na kuuongoza ili upate mashiko na kuwa na ramani nzuri kwa Tanzania,mfano mzuri nchi ya Afrika Kusini kupitia shirikisho la soka la nchi hiyo SAFA wenyewe wamejikita kuusimamia mchezo huo pamoja pia wakisimamia soka la nchi hiyo.
Sasa basi shirikisho la soka Tanzania,Baraza la Michezo na wadau wengine pasi kuchelewa itazameni timu hii ya taifa ya soka la ufukweni na kuipa sapoti kwani siku za hivi karibuni tumemsikia Kocha mkuu John Mwasasu akisema kambi yake ina uchache wa mipira ya mazoezi ambapo kwa mchezo huo katika mazoezi yake kila mchezaji anatakiwa awe na mpira wake.
Vilevile suala lingine Kocha Mwasasu alililosema ni kuwa na baadhi ya wachezaji waajiriwa na wanatumikia timu hiyo hivyo amewaomba waajiri wa wachezaji hao wawape nafasi ili kulitumikia taifa pale watakapohitajika.
Kwa wakati huu timu hiyo inajiandaa na hatua ya pili ya mashindano ya soka la ufukweni kwa kuvaana na timu ya taifa ya Misri kuwania kombe la mataifa ya afrika ambapo fainali zake zitafanyika shelisheli.