IKIWA zinakutana kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi Kuu msimu huu kwa timu za Simba na Yanga, imebainika kuwa mwamuzi wa mpambano huo atakuwa Victor Mwandike, imebainika.
Simba na Yanga zitapambana Oktoba 26 kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa ni miezi mitatu baada ya Yanga kuichaka Simba katika michuano ya Kombe la Kagame. Pambano la Simba na Yanga lilikuwa lifanyike Julai 27.
Pambano hilo lilikuwa la kutafuta mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame baada ya timu hizo kufanya vibaya katika nusu fainali. Tusker ya Kenya ndiyo iliyotwaa ubingwa.
Uchunguzi uliofanywa jijini Dar es Salaam umebaini kuwa mwamuzi huyo ambaye sehemu kubwa amekuwa akiminiwa kwa mechi hizo za watani, atasaidiwa na John Kanyenye wa Mbeya na Jesse Erasmus kutoka Morogoro.
Hii ni mara ya kwanza kwa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kupanga waamuzi tofauti katika mechi moja, mara nyingi mwamuzi wa kati hutoka mkoa mwingine lakini waliosalia huwa ni kutoka katika mkoa husika.
Hata hivyo, mchezo huo wa Oktoba 26, Jumapili hautakuwa wa kwanza kuchezeshwa na Mwandike ambaye amewahi kucheza mechi mbalimbali za watani zao hao ikiwa ni pamoja na ile ya Februari mwaka 2001, mchezo wa Ngao ya Hisani ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1.
Mwandike, kutoka Dar es Salaam pia alichezesha mchezo wa watani hao, Novemba 2002 na matokeo kutoka suluhu ya bila kufungana.
Hata hivyo, Simba imekuwa ikiinyanyasa Yanga kwa kuifunga mfululizo katika miaka ya hivi karibuni zinapokutana kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mwaka 2000, Simba iliifunga Yanga mabao 2-1 wakati mwaka 2002 pia iliifunga timu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani mabao 4-1 katika fainali za michuano ya Kombe la Tusker.
Mwandike amekuwa kinara wa mechi hizo kama ilivyokuwa kwa waamuzi wa enzi hizo Omar Abdulrasul wa Morogoro. Waamuzi wengine waliochezesha mechi nyingi za Simba na Yanga ni Omar Abdulkadir wa Dar es Salaam na Nassor Hamduni wa Kigoma.
Waliochezesha mara chache na waliokuwa na maamuzi thabiti katika mechi ya watani ni pamoja na Paschal Chiganga wa Musoma, David Nyandwi wa Rukwa ambao ni waamuzi wenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA.