Kabla ya kuwa kocha mkuu wa muda wa Forest Green Rovers mwanamke huyo alikuwa bosi wa Akademi ya klabu hiyo…..
WALIANZA Waamuzi wanawake wa mchezo wa soka. Wakapewa nafasi kupuliza filimbi katikati ya dimba na wengine wakawa Waamuzi wasaidizi. Waamuzi wanawake wamepiga hatua katika soka na hawajaachwa nyuma. Chelsea waliwahi kuwa na daktari mwanamke, ambaye alivunja vikwazo vyote vya wanawake kukosekana katika klabu za EPL.
Sasa yupo mwanamke wa kwanza kufundisha mpira wa miguu England katika timu ya wanawake. Ingawa ni ngazi ya chini ya Ligi lakini inabaki kuwa rekodi ya Aina yake.
Klabu ya daraja la pili Forest Green Rovers imemteua Hannah Dingley kuwa kocha wao. Uteuzi wa Hannah umekuwa gumzo Ingawaje anakuwa kocha wa muda wakati timu hiyo ikiwa inajiandaa kupata kocha wa kudumu.
TANZANIASPORTS inafahamu kuwa kibarua alichokabidhiwa Hannah kinamweka katika rekodi kwa klabu hiyo, kwa Ligi hiyo pamoja na soka kwa ujumla wake. Anakuwa kocha wa kwanza klabuni hapo kuongoza kikosi Cha wanaume.
Hannah Dingley amepewa jukumu hilo kuwa kocha wa kikosi Cha kwanza. Vilevile katika Ligi zote za England, yeye ndiye Mwalimu wa kwanza mwanamke kuteuliwa kunoa kikosi cha wanaume.
Umekuwa uamuzi wa kushangaza uliofanywa baada ya aliyekuwa kocha wao Duncan Ferguson kuachana na Forest Green ambako alidumu kwa kipindi cha miezi sita.
Kabla ya kuwa kocha mkuu wa muda wa Forest Green Rovers mwanamke huyo alikuwa bosi wa Akademi ya klabu hiyo.
Kwa Mara ya kwanza Hannah alisimamia mazoezi ya klabu hiyo mapema wiki hii baada ya mpango wa kuondoka wa Duncan Ferguson kukamilika.
Hannah Dingley ana leseni ya ukocha kutoka Shirikisho la Soka Ulaya ( UEFA Pro Licence), ni Kati ya wanawake wenye ushawishi katika mchezo wa soka.
Kocha anatarajiwa kuendelea na kibarua chake ikiwemo kukiandaa kikosi kwa ajili ya msimu ujao. Maandalizi ya msimu ujao yaliyotakiwa kufanywa na Ferguson, sasa yapo mikononi mwa mwanamke huyo.
Forest Green inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Melksham Town katika maandalizi yao ya msimu ujao. Katika mchezo huo Hannah ndiye atakiongoza kikosi Cha Forest Green Rovers.
Mmiliki wa Forest Green Rovers, Dale Vince huenda akawa tajiri wa kwanza kuchukua uamuzi unaotarajiwa kutikisa soka England, kwani huwa haufanywi na wengi wanaomiliki timu.
WANAWAKE KATIKA MCHEZO WA SOKA
Mwake 1991: Fainali za kwanza za Kombe la Dunia kwa wanawake zilifanyika China. Timu 12 zilishiriki fainali hizo ambapo Marekani iliibuka kuwa bingwa.
Mwaka 1994: Wendy Toms alikuwa mwanamke wa kwanza katika kipindi cha miaka 106 na kuweka rekodi ya kihistoria kuwa refa msaidizi katika mchezo kati ya Torquay v Carlisle mwezi Agosti na ilikuwa mechi yake ya kwanza.
Miaka miwili baadaye akawa mwanamke wa kwanza kuchezesha mchezo wa wanaume.
Mwaka 1996: mwaka mmoja baafa ya kufanyika fainali za pili za Kombe la Dunia kwa wanawake, timu za wanawake zilishiriki michezo ya mpira wa miguu katika mashindano ya Olimpiki kwa Mara ya kwanza. Katika fainali Marekani walishinda medali ya dhahabu baada ya kuwafunga China huko jijini Athens, Georgia.
Mwaka 1997: Wendy Toms alikuwa mwamuzi msaidizi wa kwanza wa Ligi Kuu England. Alishika kibendera chake Cha kwanza EPL katika mchezo Southampton vs Crystal Palace.
Miaka mitatu baadae alikuwa mshika kibendera katika mchezo wa fainali Carabao.
Mwaka 2021: Rebecca Welch alitajwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha mchezo wa mpira wa miguu wa wanaume uliozikutanisha Harrogate vs Port Vale kwenye daraja la Pili. Tukio hilo lilikuja miaka 11 baada ya Amy Fearn kuchukua jukumu la kuchezesha mechi ili kumalizia dakika dakika 20 za mchezo zilizobaki kutokana na mwamuzi wa Kati kuumia.
Katika mahojiano fulani aliyowahi kufanya mapema mwaka huu, Hannah Dingley aliulizwa ikiwa itatokea siku za usoni timu za wanaume kufundishwa na kocha mwanamke. Kocha huyo alisema ” inawezekana, na itakuja hivi karibuni kuliko wengi wanavyodhani. Mafanikio ambayo wamepata timu ya Taifa ya wanawake, pamoja ubora wa kocha Emma Hayes unavyoipa mafanikio Chelsea ni dhahiri kuwa wapo wanawake wenye uwezo kuwa makocha wazuri. Muhimu ni kuwa na Imani nao na wanaweza kufundisha timu za wanaume. Siku si nyingi tutaona wanawake kwenye mabenchi ya timu za wanaume.”