Moja ya hadithi ambayo kila siku hizi unatakiwa kuisoma kwa kuizingatia ni hadithi ya Mrisho Ngassa. Moja ya wanasoka bora kuwahi kutokea kwenye nchi yetu ya Tanzania.
Uzuri wa Mrisho Ngassa alikuja wakati ambao dunia inahitaji wachezaji wa aina yake. Wakati ambao mshambuliaji halisi wa kati alikuwa anapotea kwenye ulimwengu wa soka na mshambuliaji aliyekuwa anatokea pembeni mwa uwanja ndiye alikuwa anahitajika kwenye soko.
Ndiyo wakati ambao Ronaldo De Lima alikuwa anaenda kupumzika na Cristiano Ronaldo alikuwa anakuja kuchukua nafasi yake. Ndiyo wakati ambao dunia ilikuwa na uhaba wa washambuliaji wa kati.
Uhaba ambao ulisababisha tupate kutambulishwa kwa false 9 “namba 9 muongo” , mchezaji ambaye alikuwa anacheza eneo la mbele kama mshambuliaji wa kati muongo.
Huyu alikuwa na uwezo wa kushuka chini katikati ya uwanja, kwenda pembeni mwa uwanja ili mradi tu atengeneze uwazi eneo la nyuma, uwazi ambao ulikuwa unatumiwa na wachezaji wenzake wanaotokea pembeni mwa uwanja.
Huu ndiyo wakati ambao wachezaji kama Mrisho Ngassa walikuwa wanahitajika sana kwa sababu kuna dunia mpya ilikuwa imeshatengenezwa kwa ajili ya wao kukaa na kufanya wanachotaka.
Dunia ambayo ilikuwa inahitaji mchezaji anayetokea pembeni mwa uwanja mwenye uwezo wa kufunga magoli mengi ndani ya msimu mmoja na kutoa pasi nyingi za mwisho za magoli ndani ya msimu mmoja.
Mrisho Ngassa alikuwa anaishi kwenye hii dunia. Alikuwa anafunga sana magoli akitokea pembeni mwa uwanja, alikuwa anashindana na washambuliaji halisi wa kati kwa yeye kuwa na uwezo wa kucheza kama false 9 (namba tisa muongo).
Huyu ndiye aliwahi kuwa mfungaji bora wa ligi ya mabingwa barani Afrika mwaka 2014 akiwa na magoli 5, huyu ndiye aliwahi kuwa mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania bara mwaka 2011 na mwaka 2008 alikuwa mfungaji bora wa CECAFA.
Mrisho Ngassa ndiye mfungaji bora wa pili wa muda wote wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars ) akiwa na magoli 25 nyuma ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara mwenye magoli 28.
Vyote hivi Mrisho Ngassa kavifanya akiwa anacheza akiwa anatokea pembeni mwa uwanja na kuna wakati mwingine aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars”, Marcio Maximo aliwahi kuwa anamchezesha kama false 9 (namba tisa muongo ).
Hii inatosha kukuonesha kuwa Mrisho Ngassa alikuja kipindi ambacho dunia inageuza shingo kuwatazama wachezaji ambao wana sifa kama zake. Dunia ilikuwa inahitaji wachezaji kama yeye.
Ndiyo maana leo hii tuna Cristiano Ronaldo, Raheem Sterling Alexis Sanchez, Lionel Messi, Neymar Jr, hawa wote ndiyo wamebeba msisimko wa soka kwa sababu mahitaji ya soka kwa sasa yanawahitaji aina ya wachezaji kama hawa.
Uchezaji wa hawa watu hautofautiani sana na uchezaji wa Mrisho Ngassa, Mrisho Ngassa alitakiwa kuongeza juhudi sana, juhudi ambazo zingemwezesha yeye kufika sehemu ambayo ingekuwa kubwa kwake na muda huu angekuwa anamalizia maisha yake ya mpira huko China kwa kutunukiwa utajiri wa pesa.