*Manchester United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Southampton zinavyopigana vikumbo na Arsenal kuwania nafasi hizo muhimu.
*right down to the wire.
IMEKUWA kama kawaida sasa kwa Arsenal kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) hivyo kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Kwa misimu 17 mfululizo, chini ya kocha Arsene Wenger, Arsenal wamefuzu michuano hiyo mikubwa zaidi kwa klabu barani.
Walikuwa timu ya kwanza ya London kutokea kwenye fainali ya UEFA, nayo ilikuwa 2006. Tangu msimu wa 1998/99 hadi 2014/15, Arsenal wamekuwa wakicheza michuano hiyo.
Kwa England, ili timu ifuzu wanatakiwa kuwa katika nafasi nne za juu, na ni falsafa ya Wenger kwamba moja ya ‘makombe’ timu yake inayohitaji ni huko kufuzu tu.
Rekodi hiyo ya kufuzu miaka mingi imepitwa na Manchester United na Real Madrid pekee katika Ulaya katika zama hizi.
Arsenal wamekuwa timu ambayo kuna wakati wanatarajiwa na kila mmoja kushinda lakini hupoteza mechi na wanapofikiriwa wanapoteza hushinda.
Mwaka jana walikatisha kiu yao ya miaka mingi bila kikombe walipotwaa ubingwa wa Kombe la FA, wanaoendelea kuutetea msimu huu baada ya kuvuka kihunzi cha robo fainali kwa kuwafunga Man United 2-1 wiki jana.
Kwa upande wa kufuzu nafasi nne za juu ili kucheza UCL msimu ujao, inaelekea kwamba kuna ushindani mkubwa zaidi mwaka huu.
Wakati Chelsea wakiongoza ligi huku wakikimbiliwa na mabingwa watetezi, Manchester City, kuna uwezekano nafasi mbili za juu zikawa zimekwenda tayari, au zinakaribia kwenda, japokuwa bado kuna mechi kama tisa za kuchezwa kukamilisha EPL.
Ugumu wa msimu huu unaompa Wenger na vijana wake mtihani ni jinsi timu za Manchester United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Southampton zinavyopigana vikumbo na Arsenal kuwania nafasi hizo muhimu.
Kwa maneno mengine ni kwamba huenda nafasi hizo mbili zilizobaki zikawa zinagombewa na timu tano, na ili kufuzu, Arsenal hawatakiwi kuteleza kwenye mechi zijazo, hasa watakapokabiliana na baadhi ya washindani wao wanaofukuzia nafasi hizo.
Baada ya kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la FA kutetea taji lao, lazima wafikirie juu ya mechi tisa za EPL zilizobaki, kuhakikisha wananyakua pointi nyingi kadiri iwezekanavyo.
Jingine ni kuomba pia ili wasipate majeruhi wengine zaidi, maana kama ilivyokuwa msimu uliopita, wamegubikwa na matatizo ya kuumia wachezaji, tena muhimu.
Ninavyoona Liverpool wanatia ushindani mkubwa, tena ukiwa umeanza mwaka huu wa 2015 baada ya kuwa wameanza ligi kwa kusuasua, wakiwindwa na jinamizi la kukosekana Luis Suarez waliyemuuza Barcelona.
Hawa wamefanya vyema kwa kuwanyuka timu nzuri katika mechi zao za karibuni, zikiwamo Spurs, Southampton na mabingwa watetezi City.
Katika mechi ya kwanza pale Anfield, Arsenal walikwenda sare ya 2-2 na Liverpool, tena wakati ule vijana wa Brendan Rodgers wakiwa si imara kama sasa.
Kwa msingi huo, Wenger ana mtihani mgumu hapo, maan Daniel Sturridge aliyekuwa majeruhi sasa yu timamu wa mwili na kwenye kiwango kizuri na Liver nao wanataka washike nafasi nne za juu.
Mei 16 kutakuwa na mechi ya kisasi, ambapo Manchester United watawaalika tena Arsenal Old Trafford na wangependa kuona wakishinda, ili kufuta aibu ya kufungwa hapo kwenye robo fainali ya Kombe la FA Machi 9.
Louis van Gaal atawaingiza vijana wake wakiwa kama faru aliyejeruhiwa, mwenyewe akitaka kuanza na rekodi nzuri kwa kufuzu kucheza UCL waliyoikosa msimu huu baada ya kumaliza ligi wakiwa nafasi ya saba.
Arsenal wakishinda hapo tena, wanaweza kuwa wamepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mashetani Wekundu na wakifungwa watajitia matatani kuvuruga rekodi ya misimu 17 ndani ya UCL.
Lakini pia Mei 24 kuna mechi dhidi ya wagumu West Bromwich Albion. Si ajabu vita ya kuwania nafasi nne za juu ikaenda hadi siku hii ya mwisho ya msimu wa EPL. Waingereza wanasema right down to the wire.
Kwa mawazo hayo, mechi hiyo ya mwisho ni muhimu kwa Arsenal kwa minajili hiyo, lakini pia kulinda heshima ya Washika Bunduki wa London.
Hii haitakuwa mara kwa kwanza kwa Wenger kukabiliana na Baggies hawa wakati akitaka kujihakikishia nafasi ligi kubwa ya Ulaya.
Mwaka 2012 walikuwa nao, ambapo hatimaye Arsenal walipigana kufa na kupona wakapata ushindi wa 3-2 na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Katika dakika za mwisho kabla ya kipenga kupulizwa, Wenger alionekana mwenye hofu kubwa, na alikuwa amemshika msaidizi wake wa wakati ule, Pat Rice, kana kwamba alidhani dunia ilikaribia kuanguka.
Wakicheza vyema, Arsenal wataepuka mechi zenye shinikizo kubwa ambazo huwa tabu kushinda katika siku za mwisho.
Arsenal wana rekodi za aina yake, ambapo 2006 wakiwa na kipa Jens Lehman walipata kuweka rekodi ya kutofungwa hata bao moja katika mechi 10 mfululizo kuelekea michuano ya UEFA.
Walikuwa na ngome nzuri, iliyokwenda dakika 995 bila kuruhusu bao. Ni wakati waliopo wajifunze na wajijenge hivyo, pengine ndiyo maana Wenger anafikiria kuongeza wachezaji majira yajayo ya kiangazi, kuanzia kipa, beki na kiungo. Kwa sasa ushindani kwa nafasi nne za juu ndio kama vile umeanza.