Mtandao wa klabu ya Manchester City na nyingine duniani zenye mmiliki mmoja umeanza kuzua maswali katika ulimwengu wa soka.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekuwa wa kwanza kuhoji, ambapo ametupa swali lake juu ya usajili wa kiungo wa kimataifa wa England, Frank Lampard aliyesajiliwa wiki iliyopita tu kutocha Chelsea kwenda New York City.
Lampard (36) sasa ametolewa na klabu hiyo ya Marekani kwa Man City kwa mkopo acheze michuano ya Ligi Kuu ya England na ile ya Mabingwa Ulaya hadi katikati ya Januari mwakani ligi ya Marekani itakapoanza.
Mabilionea wanaohusishwa na klabu na kampuni za mafuta Mashariki ya Kati wana mtandao wa klabu tatu kubwa duniani – Manchester City, New York City na Melbourne City ya Australia ambayo imemchukua kwa mkopo David Villa aliyesajiliwa majuzi kutoka Atletico Madrid ya Hispania.
New York City pia wanahusiana na New York Yankees tangu 2013 lakini pia kuna Yokohama F Marinos. Mwaka huu Man City wamewekewa ukomo wa kusajili wachezaji 21 tu, ambapo katika Ligi Kuu wanatakiwa kuwa na wanane wa England.
“Je, hii ni njia ya kujinasua kwenye kibano cha kanuni za uungwana wa matumizi ya fedha? Sijui, lakini inaelekea kwamba hizi klabu za ‘City’ zitakuwa zikiilisha klabu yao mama ya Manchester City – nasikia wanataka kununua klabu tano maeneo mbalimbali duniani,” akasema Wenger.
Mfaransa huyo anasema kwamba inashangaza kuwa walifanikiwa kununua timu hiyo ya Marekani kwa dola milioni 59.4 na sasa watacheza kwenye Ligi Kuu ya Marekani msimu ujao na kwamba mwelekeo sasa ni kuwa rangi ya bluu itasambaa kote duniani.
Wenger alisema Arsenal hawawezi kutumia mbinu kama hizo maana si uungwana. Wenger amekuwa akipinga matumizi kupita kiasi ya fedha kwa kununua wachezaji, na alikuwa ametabiri kwamba sheria ya Uefa ingezikaba koo timu pinzani na Arsenal.
Alisema kwamba wanafurahia kwamba fedha ambazo Arsenal wanazalisha zinatosha kuendesha klabu hiyo na zinabaki kidogo, si kama Man City wenye nyingi za kuendesha klabu nyingine nje ya nchi.