Nyota wa Yanga, Simon Msuva ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania.
Pamoja na kupewa tuzo hiyo, Msuva amepata pia kiatu cha dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora kwenye ligi iliyomalizika karibuni, ambapo Yanga walitwaa ubingwa.
Msuva amewazidi kete mchezaji mwenzake aliyekipiga Yanga msimu uliopita, Mrisho Ngasa aliyehamia klabu ya Free State ya Afrika Kusinina beki wa Simba, Mohamed Hussein. Ngasa ametimkia Afrika Kusini.
Msuva anayetakiwa na klabu ya Bidvest ya Afrika Kusini pia, amejinyakulia zawadi ya Sh milioni 11.4, ambapo Sh milioni 5.7 ni kwa tuzo ya uchezaji bira na nyingine kama hizo kwa ufungaji bora.
Msuva alikuwa nchini Ethiopia kwa mazoezi na Timu ya Taifa ya Tanzania na anatarajiwa kuwa safarini nchini Misri kwa ajili ya mechi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika wikiendi hii.
Katika hafla hiyo, hata hivyo, alipata uwakilishi mnono kutoka kwa baba yake mzazi, Happygod Msuva na mamaye Suzan Msuva.
Katika hafla ambayo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, kipa bora alitajwa kuwa Shaaban Kado wa Coastal Union.
Huyo aliwazidi wengine ambao ni Mohamed Yusuph wa Prisons na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar. Kado alipata zawadi ya Sh milioni 5.7.
Kocha bora amekuwa Mbwana Makatta aliyewapiku kocha wa Yanga, Hans De Pluijm na yule wa Simba kwa msimu uliopita, Goran Kopunovic.
Makatta ametwaa zawadi ya Sh milioni 8.6 kutokana na kazi kubwa aliyofanya ya kuwanusuru Prisons kushuka daraja msimu huu.
Kwa upande wa waamuzi, Israel Nkongo amechukua tuzo akiwa amewaacha Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu na kujizolea Sh milioni 8.6.
Upande wa nidhamu klabu iliyoibuka vyema ni Mtibwa Sugar. Walikuwa wakiwania tuzo hiyo na Mgambo JKT na Simba. Kwa nidhamu yao, Mtibwa wamepewa Sh milioni 17.2.
Itakumbukwa kwamba Mtibwa walianza vyema sana Ligi Kuu lakini wakateleza baadaye kiasi cha kukaribia eneo la kushuka daraja.