Menu
in , ,

Msituletee Siasa Kwenye Soka

viwanja

Katika jamii nyingi ulimwenguni, michezo, hususani soka, imejengeka kuwa zaidi ya burudani. Soka limekuwa na nguvu ya kushawishi na kuunganisha watu kutoka tabaka na mitazamo mbalimbali. Hii inafanya soka kuwa na mvuto maalum si tu kwa mashabiki bali pia kwa wanasiasa. 

Kwa Tanzania tuko katika kipindi ambacho tunaelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ambapo wananchi watachagua wawakilishi wao ambao ni Madiwani ,Wabunge na Rais. 

Ni wazi kuwa hiki ndio kipindi ambacho mechi za soka zitaonekana ni za muhimu Sana Kwa wanasiasa katika ngazi mbalimbali kwani zitatumika kama jukwaa la kujipatia umaarufu wa kisiasa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Utajiuliza wanakua wapi kipindi ambacho vijana wapo vijiweni tu hakuna ajira na Wala hakuna Ligi ambazo zinachangamsha maeneo ambayo wanayaongoza au wana mpango wa kugombea? katika miaka yote tangu nakua mpaka sasa nimekua nikiona wanasiasa na vyama vyao wakitumia matukio haya kwa ajili ya kujiimarisha na kuvutia uungwaji mkono. Hii inadhihirisha uhusiano wa karibu kati ya siasa na soka, ambao umekua na kuimarika kadri kampeni zinavyoendelea.

Tanzania ni taifa ambalo wananchi wake wanaipenda soka kwa dhati. Mechi za soka zinavutia na haishangazi kuona idadi kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi wakija kushuhudia vipaji vya wachezaji na kusherehekea mchezo huu maarufu. Soka kwa Tanzania limekuwa ni sehemu muhimu ya burudani, na vilevile limechangia kujenga mshikamano na umoja.

Wanasiasa wamegundua umuhimu huu wa soka, na wanatumia fursa hii kuvutia watu wengi kwa nia ya kujijenga na kujitangaza kwangu sio shida lakini swali kubwa ni kwamba huwa wanajiandaaje baada ya kupata umaarufu wanaotafuta kwenye soka kwa ajili ya kuandaa sera ambazo zitavutia vijana kuwachagua wakati mwingine bila kuwa na maswali mengi ya utatufanyia nini tukikuchagua?

Kwa utafiti wangu mdogo tu na hata wewe msomaji utaniambia kipindi hiki ndio kile ambacho utakuta kunaandaliwa zile Ligi za Madiwani au za Wabunge katika majimbo ya uchaguzi kwa sababu wanasiasa wa Tanzania hutumia mechi za soka kama njia ya kufikia wapiga kura wengi kwa wakati mmoja. 

Katika mikusanyiko ya mechi hizi, ambapo mashabiki wa timu mbalimbali hukusanyika, wanasiasa hupata nafasi ya kutangaza ajenda zao na kusikiliza kero za wananchi. Mara nyingi, hutumia mechi hizi kwa kupeleka salamu za kuwatakia mashabiki na timu zao kila la kheri, jambo ambalo linaonekana kama njia ya kujionesha kuwa karibu na wananchi.

Ukiachana na jambo hilo tu hiki ni kipindi ambacho watajitokeza watu ambao Kwa namna Moja au nyingine wana lengo la kugombea kwa kutoa michango ya fedha, mavazi ya timu, au hata kutoa zawadi kwa wachezaji au mashabiki. Hatua hizi za kutoa msaada na kujitokeza kwa mashabiki hujenga taswira ya viongozi wanaojali na kufuatilia maslahi ya wananchi wao jambo ambalo baada ya uchaguzi wengi wao hupotea.

Kutumia mechi za soka kama njia ya kampeni kunaleta athari mbalimbali. Kwanza, mechi hizi hutoa fursa ya kuwaunganisha watu kutoka mitazamo tofauti na kujenga mshikamano. Hata hivyo, kuna changamoto pia, kwani baadhi ya mashabiki wanaweza kuona juhudi hizi za kisiasa kama juhudi za kinafiki au kunufaisha maslahi binafsi ya wanasiasa ndio Yale ambayo unakuta wapo watu ambao hawapendi kwenda viwanjani kutazama mechi Kwa sababu unakutana na picha na mabango ya wanasiasa yakitembezwa kuunga mkono kuhusu jambo fulani.

Kwangu mimi mambo kama haya naona kabisa kama kuna hatari ya kushuka kwa imani ya wananchi kwa siasa na michezo. Wakati ambapo wanasiasa wanatumia nguvu zao kujipenyeza kwenye mechi za soka, wananchi wanaweza kuona kwamba michezo hiyo imepoteza maana yake ya asili. Mashabiki wanaweza kupoteza imani kwa viongozi ambao wanaonekana kuwa wanatumia soka kwa maslahi yao binafsi badala ya kusaidia jamii kwa dhati.

Hatukatai kwamba katika ulimwengu wa kisasa, soka na siasa vinazidi kuunganishwa kwa njia mbalimbali. Kwa hapa Tanzania, mechi za soka zinaendelea kuwa jukwaa muhimu la kampeni, ambapo wanasiasa hutumia matukio haya kujenga jina lao na kuvutia wapiga kura. Hata hivyo, ingawa hatua hizi zinaweza kuongeza umaarufu wao kwa muda, wanasiasa wanapaswa kuwa waangalifu ili wasijenge taswira ya kutumia mchezo huu kwa maslahi yao binafsi.

Wananchi wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, itakuwa vyema iwapo wanasiasa watatumia mechi za soka kwa namna ambayo inalenga kusaidia jamii na kukuza umoja. Soka linaweza kuwa jukwaa zuri la kuwafikia wapiga kura, lakini inahitaji busara na maadili kuhakikisha kuwa linabaki kuwa burudani ya watu na nyenzo ya kujenga mshikamano badala ya kuwa uwanja wa migawanyiko na maslahi binafsi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version