Msimu mpya wa soka wa 2019/2020 unaanza, huku klabu zikiwa zimefanya usajili tofauti.
Wakati Arsenal wamewasajili wachezaji kadhaa kama David Luiz wa Chelsea na Kieran Tierney kutoka Celtic ya Uskochi, Everton wamemchukua Alex Iwobi kutoka Emirates.
Arsenal walikuwa wanamtaka pia mshambuliaji wa Crystal Palace, Wilfried Zaha lakini imeshindikana. Alhamisi hii Kocha wa Crystal Palace, Roy Hodgson alimwondoa mchezaji huyo mazoezini, akisema hakuwa katika hali nzuri kiakili.
Tottenham Hotspur walishindwa kumchukua mchezaji Paulo Dybala kutoka Juventus tkutokana na masuala ya haki za mchezaji. Spurs waliwaomba Juve kumlipia mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina haki hizo lakini mabingwa hao wa Italia hawakuwa tayari.
Spurs walidhani kwamba dili hilo lingekuwa limekamilika wakati ambapo mshambuliaji wa Manchester United kutoka Ubelgiji, Romelu Lukaku akienda zake Inter Milan baada ya kupungua kwa kiwango chake cha uchezaji hapo Old Trafford.
Paul Pogba sasa anatarajiwa kubaki Old Trafford kwa sababu United hawakusajili mbadala wake, nah ii ni habari mbaya kwa Real Madrid waliokuwa wakimhitaji mno. Sasa wanadaiwa kujielekeza katika kumpata Neymar wa PSG.
Inter Milan wamempata Lukaku kwa pauni milioni 74, ikiwa ni rekodi mpya kwa klabu hiyo kutoa kiasi kikubwa hivyo cha fedha.
Lukaku amefunga mabao 42 katika mechi 96 kwa United, akiondoka miaka miwili tu baada ya kujiunga na miamba hao akitoka Everton kwa kiasi cha pauni milioni 75 kwa mkataba wa miaka mitano.
Sasa anakuwa mchezaji wa tatu kwa ughali huko Serie A baada ya wale wawili wa Juventus, Cristiano Ronaldo (£99.2m) na Gonzalo Higuain (£75.3m). Lukaku amedai kwamba Inter ndio klabu pekee aliokuwa akiwataka.
Manchester wametoa taarifa wakisema kwamba wanamshukuru Lukaku kwa muda aliokuwa nao na jitihada zake za kuwaimarisha. Alionekan akushuka kiwango na kuachwa kwenye uteuzi katika timu kwa muda sasa.