*Van Gaal, Klopp, Simeone wafikiriwa
Hatimaye David Moyes amefukuzwa kazi ya ukocha kwenye klabu ya Manchester United walioshindwa kutetea ubingwa wao.
Hatua hiyo imekuja baada ya uvumilivu mkubwa wa wamiliki wa klabu hiyo, Familia ya Glazer ya Marekani, lakini sasa wameona maji yamezidi unga.
Taarifa ya United ilisema mapema Jumanne hii kwamba Moyes ameondoka klabuni hapo, kocha mchezaji Ryan Giggs atashikilia kwa muda mikoba yake hadi uteuzi wa kocha wa kudumu utakapofanyika.
Moyes amekuwa na wakati mgumu katika miezi 10 aliyokaa United, ikiwa ni pamoja na kufungwa mechi 16 na kuvunja rekodi nyingi za United kwa kufanya vibaya.
Tayari wanaelekea kukosa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na wasipogangamala kwenye mechi zilizobaki na kuomba huruma ya timu pinzani kufungwa, watakosa hata Ligi ya Europa kwa mara ya kwanza tangu miaka ya mwanzo ya ’90.
Sumu iliwaingia wana United vya kutosha wikiendi iliyopita, pale Moyes aliporudi kwenye klabu aliyofundisha kwa miaka 11 ya Everton na wakafyatuliwa mabao 2-0, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1969 kuoga kichapo jinsi hiyo hapo.
Walichezea vichapo vingi, kiwa ni pamoja na kutoka kwa mahasimu wa mji wao Manchester City waliowakung’uta 4-1 kisha wakachapwa mfululizo kwenye mzunguko wa kwanza na Everton na Newcastle.
Haali ya hewa ilizidi kuhafuka Old Trafford kwani Mashetani Wekundu walikuwa wakikubali vipigo mfululizo ikiwa ni pamoja na cha kwanza kihistoria kutoka kwa timu ya Swansea.
Kana kwamba haitoshi, walitolewa kwenye Kombe la Ligi na Kombe la FA kabla ya kubanduliwa pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa hawawezi tena kutwaa ubingwa wa England.
Takwimu zimewashitua washabiki wa United na wadau wengine wa soka, kwa sababu katika miaka 27 ya ukocha wa Ferguson ni mara moja tu United walitolewa katika raundi ya tatu ya Kombe la FA lakini Moyes katika miezi yake sita ametolewa haraka tayari katika raundi hiyo.
Moyes mwenyewe amekuwa akijitetea kwamba hata angekuwa Alex Ferguson aliyempendekeza kuwa kocha angepata wakati mgumu na kikosi alicho nacho, lakini ndicho kilichotwaa ubingwa msimu uliopita.
Baada ya kufungwa wiki iliyopita, alidai kwamba anajiandaa kukisuka upya kikosi hicho, ambapo inadaiwa kwamba zimetengwa pauni milioni 150 kununua wachezaji wapya.
Hata hivyo, Moyes amekuwa akipondwa na baadhi ya wachezaji wake kwa mfumo wa mazoezi na jinsi anavyopanga kikosi chake kwa kushitukiza, lakini pia kuwaweka benchi wachezaji muhimu au kuwachezesha kwenye nafasi tofauti na wanazowezea au kupenda.
Baadhi ya wanaodaiwa kupata kulalamika ni pamoja na Giggs, Danny Wellbeck, Rio Ferdinand, Robin van Persie aliyedaiwa kukosana na kocha wake huyo lakini pia Javier Hernandez, Wilfred Zaha na Anderson aliyetolewa kwa mkopo Fiorentina.
Makocha wanaotajwa kuweza kuchukua nafasi hiyo ni pamoja na yule wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal, Kocha wa Borussia Dortmud, Jurgen Klopp ambaye tayari amekana kukubali mpango kama huo na hata wengine wanamfikiria kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone wa Bayern Munich, Pep Guardiola na Laurent Blanc wa Paris Saint Germain.