*Hatimaye aliajiriwa na Bayern Munich atakayoiaga kuhamia Manchester City, mwezi Julai*
Mashabiki wa Chelsea na Manchester United wamo katika mtafaruku baada ya Jose Mourinho kuwaandikia barua Manchester United akiomba kazi. Sasa kutokana na uteuzi rasmi wa kocha mheshimika, Josep Gurdiola (Barcelona na Bayern Munich), kuja Manchester City, Julai, wapambe wameanza kukukubali kuwa huenda ombi hilo ni la maana.
Kawaida Mourinho alitakiwa kuiaga Uingereza kabisa, kama alivyoondoka klabu za Porto – (2002- 2004) alikoshinda vikombe sita, Chelsea (vikombe saba), Inter Milan –(vitano), na Real Madrid –vitatu- Copa El Rey 2011 na vingine viwili vya 2012. Ukiacha Porto alikosana na wenye klabu hizo.
Lakini baaada ya kutimuliwa Chelsea hakutaka kwenda kupumzika kama ilivyotegemewa. Licha ya vurugu , hamaki za karibu, kuwaita wachezaji wa Chelsea wazembe na malumbano na wanahabari kuhusu aliyomfanyia mganga wa timu, Dk Eva Carneiro mwaka jana, aliendelea na ukaidi na kiburi cha kutaka kazi. Aliandika barua ya kurasa sita kuelezea kwanini na vipi atauweza umeneja wa timu ya Man United. Mourinho alitegemewa akapumzike kama mwenzake Pep Gurdiola. Gurdiola alikuwa mchezaji wa hali ya juu sana katika timu ya taifa ya Hispania na Barcelona. Alifahamika zaidi kutokana na uongozi wa timu maarufu ya Barcelona na –akaamua kupumzika mwaka mzima New York, mwishoni wa mwaka 2011.
Lakini Mourinho si sawa na Pep Gurdiola…
Gurdiola alizaliwa 1971- Mourinho mwaka 1963. Gurdiola alikuwa mchezaji wa muda mrefu aliyetingisha viwanja vya Ulaya na Mashariki ya Kati, Mourinho hakuwa mchezaji mkubwa ila alisomea sayansi ya michezo.
Wote wawili wanaheshimiwa sana na wachezaji wakubwa wakubwa. Ila Mourinho hutafuta kushinda mechi na vikombe ambapo Gurdiola hushinda vikombe kama Mourinho na pia hubadili mtindo wa timu na klabu. Ndiyo maana ujio wake Uingereza umezungumziwa sana toka ulipotangazwa Jumatatu hii. Moja ya sababu ambazo baadhi ya viongozi wa Man United hawakumtaka Mourinho ni udhaifu wake kuendeleza wachezaji vijana kinyume na makocha Arsene Wenger, Alex Fergusson na Gurdiola. Cerc Fabregas na Lionel Messi ni mfano wa maendelezo ya vijana wa Barcelona.
Ingawa Mourinho alijigamba katika barua hiyo ya kurasa sita kuwa atageuza udhaifu wa Manchester United kuwa kama enzi za Mzee Alex Ferguson baadhi ya uongozi wa timu hiyo hawaipendi tabia yake ya kuzua mizozo na ugomvi kila anakokwenda. Mbinu kuu ya Mourinho ni kushinda mechi hata kama mpira haupendezi. Ni kama askari wa kulipwa anayechukua fedha ili mradi kazi inatimizwa.
Tabia hii ya kutaka vikombe tu huwa haijengi timu kama walivyofanya Arsene Wenger, (Arsenal) Pep Gurdiola (Barcelona) na Alex Ferguson (Man United). Mourinho hana timu maalum. Ndiyo sababu yuko tayari kuandika barua ya kurasa sita akitafuta kazi hata kama anapitia nyuma ya mgongo wa Van Gaal aliyekuwa zamani mwalimu wake.
Pamoja na haya yote makocha mbalimbali na wachezaji maarufu Uingereza wanaomfahamu Gurdiola wamesisitiza huenda Man United ikamhitaji Mourihno sasa. Mchezaji aliyekuwa Barcelona, Thiery Henry, alisisitiza kuwa kocha pekee atakayewaweza majirani hawa wasiopatana ni Jose Mourinho. Hii ni sababu Pep Gurdiola anategemea kuibadili kabisa Man City. Ligi ya England itatingishika. Na mtu pekee wakuwezana na ujirani huu wa kushindana mbinu ni Jose Mourinho.