Menu
in , , ,

MOURINHO NA MZIMU WA MSIMU WA TATU

Tanzania Sports

Jose Felix Mourinho, Mreno mwenye mafanikio makubwa sana katika ngazi ya ukocha.

Mafanikio ambayo yalianza kama kitu cha kushangaza kwa sababu aliwashangaza wengi kupata mafanikio makubwa akiwa na klabu ya FC Porto.

Timu ambayo ilikuwa haidhaniwi kama inaweza kutoa ushindani kwa timu kubwa kama Real madrid, Bayern Munich, Barcelona, Manchester United.

Lakini ilifanikiwa kuchukua kikombe cha ligi ya mabingwa barani ulaya chini ya Jose Mourinho.

Hapo ndipo ukarasa wa Jose Mourinho ulivyopendeza kwa maandishi ya kumsifia. Maandishi ambayo yalizifanya klabu nyingi zimtamani.

Maandishi ambayo yalimfanya Jose Mourinho kupata thamani. Thamani yake ikawa kubwa mno!.

Ilikuwa ngumu kumpeleka klabu yoyote tu kwa pesa ya kawaida. Ilikuwa ni ngumu sana kumpeleka kwenye klabu ambayo haina malengo makubwa.

Itawezekana vipi kwake yeye kulinda heshima yake aliyoipata FC Porto kwa kwenda klabu isiyo kuwa na misingi bora ya kulinda mafanikio yake?

Ndiyo ikawa rahisi sana kwake yeye kwenda katika klabu ya Chelsea. Klabu ambayo haikuwa na historia kubwa ukilinganisha na vilabu vingine, lakini ilikuwa ni klabu ambayo ilijaza mipango yenye macho.

Mipango ambayo ilikuwa kama ndoano bora ya kumnasa Jose Mourinho. Ikawa virahisi kwake yeye kukanyaga jiji la London, macho ya wana Chelsea yalitokwa na machozi ya furaha, hata Jose Mourinho alipowataka mashabiki wa Chelsea wamwiite “The Special one” hakuna kichwa cha mwana Chelsea yoyote kilichokataa.

Vinywa vyote vilimtambua Jose Mourinho kama “The Special One”. Jose Mourinho alibeba matumaini makubwa sana ndani ya mioyo ya mashabiki wengi wa Chelsea.

Hawakukosea kumwamini, hata tumaini lao lilikuwa sahihi kuliweka kwa Jose Mourinho kwa sababu aliwapa kombe la ligi ya England kwa mara ya kwanza baada ya kukaa miaka hamsini (50) bila kuchukua.

Furaha ilijaa kwenye nyuso za mashabiki wa Chelsea. Jose Mourinho akawa kipenzi kipya kwa mashabiki wa Chelsea. Walimwamini sana!, walimwelewa sana!, na kikubwa zaidi hata cheo cha “The Special One” hawakumtolea.

Jose Mourinho alirudisha fadhila kwa kuwapa kombe la pili la ligi kuu ya England katika msimu wake wa pili.

Hakuweza kuendelea na msimu wa tatu, miguu yake iliwasha kuondoka. Italy ndiyo ilikuwa nyumba ambayo alichagua kwenda kuishi tena kwenye jiji la Milan kwenye timu ya Intermilan.

Aliwapa furaha isiyo ya kifani mashabiki wa Intermilan. Kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya ilikuwa zawadi kubwa kutoka kwa Jose Mourinho kwenda kwa mashabiki wa Intermilan.

Na inawezekana kombe hili la ligi ya mabingwa ndilo kombe ambalo lilikuwa chachu kubwa kwa RealMadrid kumchukua.

Realmadri walikaa muda mrefu bila kuchukua kombe hili, walitaka mtu ambaye angeweza kuwapa, na kwa kuwa Jose Mourinho alifanikiwa kufanya hivo akiwa na FC Porto pamoja na Intermilan ilikuwa imani kubwa sana kwa Realmadrid kupata kombe la ligi ya mabingwa chini ya Jose Mourinho.

Misimu mitatu ilimkuta Jose Mourinho akiwa katika ardhi ya jiji la Madrid. Maisha yake yalianza mwaka 2010 mpaka mwaka 2013 ndipo ikawa mwisho wa Jose Mourinho katika timu ya Realmadrid.

Msimu wake wa tatu ndiyo msimu ambayo ulikuwa msimu wa mwisho kwake , na ndiyo msimu ambao ulikuwa na matokeo mabaya kwake kwenye kila michuano ambayo alishiriki.

Alifungwa na Borrusia Dortmund magoli 4-1 kwenye mechi ya ligi ya mabingwa tena kwenye mechi ya mkondo wa kwanza. Mechi ambayo iliwakatisha tamaa Realmadrid kusonga mbele.

Ndiyo mechi ambayo iliwafanya Realmadrid kwa msimu huo wabaki hawana kitu chochote kwa sababu hata kwenye ligi kuu ya Hispania (La Liga) walimaliza ligi wakiwa nyuma ya alama 15 dhdi ya Barcelona.

Ulikuwa ni ukweli ambao unauma, kwa sababu hata Copa De Ley walifungwa kwenye fainali na wapinzani wao Atletico Madrid.

Msimu ukawa umemalizika kwa Jose Mourinho kutobeba kikombe chochote. Ndiyo msimu ambayo aligombana na watu wengi.

Hali ulikuwa mbaya kwenye vyumba vya kubadilishia nguo. Hakuwa na maelewano mazuri na wachezaji nyota.

Yalianza kutofautiana na Iker Casillas, golikipa na mchezaji wa kuheshimika katika timu ya Realmadrid.

Kutolewana kwa Jose Mourinho na Iker kulimfanya Pepe kumwambia Jose Mourinho ampe heshima inayostahiki Iker.

Hapo ndipo ugomvi mwingine mpya ulipoanzia. Akawa haelewani na Pepe, migogoro ikaendelea mpaka kwa kina Cristiano Ronaldo na Sergio Ramos.

Kwa kifupi alijikuta wachezaji nyota wote amegombana nao. Vyombo vya habari vikaingilia kati, likawa kosa kubwa sana kwao!, Jose Mourinho anapenda vita , hawezi kuishi bila vita kwa sababu anajivunia na kujiamini kupitia mafanikio yake.

Ugomvi na waandishi wa habari ukawa mpya, akawa na uadui na waandishi wa habari. Mashabiki akawagawa mara mbili, wakabaki ambao wanamwamini na ambao hawamwamini.

Waliokuwa hawamwamini walimfanya apate hamu ya kuondoka na kurudi England.

Sehemu ambayo aliamini anapendwa na mashabiki, wachezaji na vyombo vya habari.

Mwaka 2013 alirudi rasmi katika ardhi ambayo yeye alikuwa anaamini anapendwa sana kupitiliza. Sehemu ambayo aliweka alama kubwa.

Msimu wa kwanza haukuwa mzuri sana lakini msimu wake wa pili ulikuwa wenye mafanikio makubwa sana. Aliwapa Chelsea kombe la ligi kuu ya England tena kwa mara ya tatu.

Mwisho wa msimu wa pili, ukawa mwanzo wa msimu wa tatu katika uwanja wa Stamford Bridge. Mzimu wa msimu wa tatu ukaendelea tena kuzifuata nyao za Jose Mourinho.

Aligombana na kila mtu, alikwaruzana na wachezaji, akatofautiana na viongozi na akawa anakaripiana na vyombo vya habari na mwisho wa siku msimu wa tatu ukawa msimu wa mwisho kwake.

Leo hii yupo msimu wa tatu na klabu ya Manchester United. Msimu ambao alitembea nao katika klabu ya Realmadrid na Chelsea tayari umeshafika katika klabu ya Manchester United.

Mashabiki wamegawanika wapo wanaomwamini na kutomwamini mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo Ed Edewood. na wapo ambao hawamwamini Jose Mourinho.

Ametofautiana na baadhi ya wachezaji, kila kukicha anarushiana maneno na vyombo vya habari na hii ni dalili tosha kuwa mzimu wa msimu wa tatu unamfuata Jose Mourinho kila anapokanyaga.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version