TAMBO za Kocha Jose Mourinho ‘The Happy One’ zimezidi baada ya kufanikiwa kuvunja rekodi ya Manchester City.
Chelsea wakicheza ugenini katika dimba la Etihad usiku wa Jumatatu walivunja mwiko wa vijana hao wa Manuel Pellegrini kutofungwa kwao msimu huu.
Kama kawaida, City walianza kwa nguvu japokuwa walimkosa kiungo Fernandinho na mpachika mabao wao namba moja, Sergio Aguero.
Hata hivyo, kasi ilikuwa kubwakutoka kwa Alvaro Negredo, David Silva, Edin Dzeko na kiungo Yaya Toure lakini kasi hiyo ilivunjwa na Chelsea.
Mourinho alionesha soka ya kweli ya karne ya 21, akiwachezesha vijana wake uwanja mzima pasipo kupaki basi kama alivyodai West Ham walimlazimisha kwenda nao suluhu kwa mtindo wa kujihami tu, akisema ni soka ya karne ya 19.
Alikuwa ni beki Branislav Ivanovic aliyepanda na kusukuma kombora kali la kima cha nyoka wakati wa mashambulizi langoni mwa City na kumwacha kipa Joe Hart akiwa hana la kufanya.
Chelsea wangeweza kupata mabao mengine lakini mara tatu mipira iligonga nguzo ya goli, huku wachezaji wake Samuel Eto’o, Eden Hazard na wengine wakiwachachafya Man City.
Negredo alitolewa nje kwani ilionekana sio siku yake akaingia Stevan Jovetic ambaye hata hivyo hakuweza kuing’arisha siku yao na washabiki wakachukia kwa rekodi kuvunjwa.
Kwa matokeo hayo, Arsenal ndio wamecheka zaidi kwani wamebaki kileleni kwa alama zao 55 huku Man City wakifuatia kwa alama 53 sawa na Chelsea lakini Man wana mabao mengi ya kufunga kuliko timu yoyote ile.
Hata hivyo, Mourinho amesema bado hana wazo la kutwaa ubingwa kwa sababu ni mapema mno bali akawasifu vijana wake.