*Real Madrid, Dortmund nusu fainali Ulaya
Ulikuwa usiku wa mabao matano matano katika viwanja viwili kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakiingia uwanjani Uturuki na faida ya mabao matatu waliyopata nyumbani, Real Madrid walianza vyema kwa bao la Cristiano Ronaldo dakika ya saba.
Hata hivyo, Galatasaray walizinduka na kusawazisha katika dakika ya 57 kupitia kwa Emmanuel Eboue, kabla ya Wesley Sneider na Didier Drogba kusababisha tetemeko kwa mabao yao dakika za 71 na 72.
Drogba alifumani tena nyavu akielekeza kiama kwa bosi wake wa zamani Chelsea, Jose Mourinho, lakini waamuzi walishasema kwamba alikuwa ameotea.
Mechi hiyo ya robo fainali ilitokea kuwa ya mvuto mkubwa kwa washabiki 52,000 waliohudhuria na wale waliofuatilia kutoka mbali.
Galatasaray waliendeleza shinikizo kubwa dhidi ya Real, lakini dakika za majeruhi alikuwa Ronaldo tena aliyecheka na nyavu za wapinzani wao, na kumaliza ubishi wa mechi, Real wakishinda kwa uwiano wa mabao 5-3.
Nchini Ujerumani, palikuwa na usiku mwingine wa aina yake, ambapo mabao matano – matatu kwa wenyeji na mawili kwa wageni.
Borussia Dortmund na Malaga waliingia uwanjani Dortmund wakiwa na mtaji sawa, kwani hakuna kati yao aliyekuwa na goli, hivyo ni kama walikuwa wakianza upya.
Malaga walionekana kuwaelemea wenyeji wao, lakini walikuwa Dortmund waliojikusanya na katika dakika za majeruhi wakapata mabao yaliyowavusha, baada ya Malaga kuwa mbele kwa mabao mawili.
Mashujaa wa Dortmund walikuwa Marco Reus na Felipe Santana waliopigana na kufunga dakika za majeruhi, japokuwa lile la ushindi la Santana ilionekana mfungaji akiwa kama ameotea, walau kwa inchi chache.
Malaga walipata bao lao la kwanza kupitia kwa
Joaquin kabla ya nyota anayewaniwa na timu za England, Robert Lewandowski kusawazisha.
Piga nikupige iliendelea kwa mchezaji aliyeingia kipindi cha pili kwa Malaga, Eliseu alifunga bao ambalo wengi walishachukulia lingekuwa la ushindi kwa Malaga, kabla ya ‘wauaji’ wawili wale kutokea na kuwanyamazisha Wahispania hao.
Kwa msingi huo, Real Madrid na Borussia Dortmund wameingia nusu fainali, wakisubiri mechi za Jumatano hii kujua wengine wawili watakaoungana nao.
Katika robo fainali ya pili, Barcelona wasiokuwa na Lionel Messi wanawakaribisha Paris Saint-Germain ambao wote wanafungana kwa 2-2 wakati Juventus watawakaribisha Bayern Munich. Wajerumani hao wana faida ya mabao 2-0 waliyopata mechi ya awali nchini Ujerumani.