Menu
in

Morrison ni mkubwa kuzidi Yanga !

Morrison ni mkubwa kuzidi Yanga

Morrison ni mkubwa kuzidi Yanga

Tuanzie hapa, Bernard Morrison alikataa kusafiri na timu kwenda Shinyanga kucheza na Mwadui FC mechi ambayo Yanga ilishinda goli 1-0. Tuachane na matokeo ya mechi husika, wakati Yanga inasafiri kwenda Shinyanga wachezaji wote walitakiwa kusafiri na timu.

Lakini kuna baadhi ya wachezaji ambao hawakusafiri na timu, wapo wachezaji kama kina Papy Kabamba Tshishimbi ambao ilidaiwa kuwa ni majeruhi ndiyo maana hawakuweza kusafiri na timu. Lakini kuna baadhi ya wachezaji ambao hawakuwa na majeraha lakini hawakusafiri na timu.

Mmoja ya wachezaji hao ni Bernard Morrison ambaye alifikia hatua ya yeye kuzima simu , wakati anatafutwa na kocha wa Yanga hakupatikana, hata viongozi wa timu walipomtafuta hakupatikana pia.

Baadaye kulikuwepo na taarifa kuwa Simba walikuwa wanamhitaji Bernard Morrison na kuna makubaliano ya awali ambayo yalikuwa yameshafanyika kati ya Simba na Bernard Morrison. Yanga nao wakadai kuwa wana mkataba wa miaka miwili na Bernard Morrison.

Bernard Morrison kupitia Global TV alidai ana mkataba wa miezi sita na Yanga, mkataba ambao unamalizika mwezi huu wa saba na akaukana mkataba wa miaka miwili ambao Yanga walikuwa wanadai wako nao.  Sintofahamu ilianzia hapo, sintofahamu ambayo ilisababisha kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael kumsimamisha Bernard Morrison .

Adhabu ambayo ilibarikiwa na viongozi wa Yanga kutokana na utovu wa nidhamu wa Bernard Morrison.  Yote haya yalitokea kabla ya Yanga kucheza mechi ya robo fainali ya Azam Federation Cup, dhidi ya Kagera Sugar.

Yanga walifanikiwa kushinda mechi hiyo ya robo fainali dhidi ya Kagera Sugar, kitu ambacho kiliwapa tiketi ya wao kwenda nusu fainali ya kombe hili la Azam Federation Cup. Inshu siyo Yanga kufuzu nusu fainali ya Azam Federation Cup,  inshu hapa Yanga anaenda kukutana na nani kwenye mechi hii ya nusu fainali.

Yanga anaenda kukutana na Simba kwenye nusu fainali, mechi ambayo ni ya watani wa jadi, mechi ambayo ina ushindani kuanzia nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja, mechi ambayo imekuja kutuonesha kuwa Yanga ni ndogo mbele ya Bernard Morrison. 

Kumbuka Bernard Morrison alifungiwa na kocha wa Yanga  Luc Eymael lakini viongozi wa Yanga walimrudisha tena Bernard Morrison.  Picha inayokuja hapa ni kuwa Bernard Morrison amerudi Yanga kwa sababu ya mechi ya Simba.

Mechi ambayo viongozi wanaogopa kuipoteza kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza, hii mechi ni ya wapinzani wa jadi. Mechi ambayo kila timu hutaka kushinda ili kujitengenezea utulivu ndani ya klabu .

Sababu ya pili ni kuwa hii mechi inabeba hatima ya Yanga kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF. Ushindi wa mechi hii itawapa nafasi kucheza fainali ya kombe la Azam Federation Cup na kushinda fainali hii kutawapa nafasi ya wao kushiriki michuano ya CAF.

Uoga huu wa kutopeteza mchezo huu ndiyo umeifanya Yanga kumsamehe Bernard Morrison, msamaha ambao inaonesha dhahiri kuwa Yanga ni ndogo kuliko Bernard Morrison ndiyo maana Yanga imenyenyekea kwa kiasi kikubwa kuliko Bernard Morrison ambaye alikuwa ndiye mwenye kosa.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Leave a Reply

Exit mobile version