Joseph-Desiré Mobutu alikuwa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka 1965 mpaka 1997. Aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Akajiita Mobutu Sese Seko na nchi akaiita Zaire. Alikuwa rais mashuhuri kwa udikteta uliopitiliza.
Jean-Pierre aliyekuwa askari wa jeshi la Zaire akaona aukimbie utawala wa mabavu wa dikteta Mobutu. Askari huyo akamchukua mke wake na mtoto wao mdogo wakahamia Ubelgiji mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mtoto akakulia Ubelgiji na akawa mwanasoka maarufu nchini Ubelgiji akicheza nafasi ya mshambuliaji.
Akazichezea klabu kubwa za Ubelgiji kama Standard Liège na Genk. Mwaka 2012 akahamia Aston Villa ya Uingereza kwa dau la paundi milioni 7 akitokea Genk. Huyo ni Christian Benteke. Wiki iliyopita alihamia Liverpool kwa dau la paundi milioni 32.5.
Anakuwa mchezaji ghali namba mbili kuwahi kusajiliwa na Liverpool baada ya Andy Carroll aliyasajiliwa kwa paundi milioni 35 akitokea Newcastle United 2011. Benteke ameifungia Aston Villa mabao 49 kwenye michezo 101 aliyoichezea. Usajili wake unapeleka matumaini Anfield. Huenda akainyanyua Liverpool.
Najaribu kujiuliza iwapo Benteke angepata nafasi ya kuichezea klabu kubwa kama Liverpool iwapo angekulia Kongo na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo. Mashaka yananijia nikiwatazama Trésor Mputu wa Kabuscorp SC ya Angola na Dioko Kaluyituka wa Al Gharafa ya Qatar.
Mputu akiwa nahodha wa TP Mazembe aliiwezesha kushinda kombe la Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo, 2009 na 2010. Akawemo kwenye orodha ya wachezaji watano waliowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika wa BBC 2009. Wengine wanne walikuwa Didier Drogba, Michael Essien, Samuel Eto’o, na Yaya Toure.
Kocha Claude Le Roy aliyekuwa kocha wa Cameroon kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 aliwahi kusema kuwa Mputu ni Eto’o wa baadae. Rekodi, umahiri wa Mputu na sifa zote hizi hazikumwezesha kuchezea klabu yoyote ya Ulaya.
Dioko Kaluyituka pia ni mshambuliaji wa kiwango cha juu. Mwaka 2009 alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika alipofunga mabao 8 na kutwaa ubingwa akiwa na TP Mazembe.
Kwenye michuano ya Klabu Bingwa Dunia mwaka 2010 alifunga bao safi kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Internacional ya Brazil na kuipeleka Mazembe fainali. Akatwaa tuzo ya mpira wa fedha ‘silver ball’ kwenye michuano hiyo. Amewahi pia kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Qatar akifunga mabao 22 msimu wa 2013/14. Bado hakupata nafasi ya kucheza Ulaya.
Ninavyoona kinachowakwamisha Mputu na Kaluyituka ni kukulia Kongo na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo. Nchi ambayo imewahi kushiriki kombe la dunia mara moja tu 1974 na ikapoteza michezo yote. Ni taifa changa kisoka.
Mawakala wa soka la Ulaya, makocha na viongozi wa klabu wanaonekana kutokuwa na imani kuwa nchi kama hiyo inaweza kutoa wachezaji wa viwango vya juu. Naamini Mputu na Kaluyituka wangekulia Ubelgiji na kuiwakilisha bendera ya nchi hiyo kama Benteke nao wangepata nafasi ya kucheza soka katika moja ya klabu kubwa Ulaya.
Ubelgiji ina historia nzuri kwenye soka. Kwa sasa inashikilia nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora vya FIFA. Imeshiriki Kombe la Dunia mara 12. Inafahamika kwa kutoa wanasoka mashuhuri waliowahi kutamba Ulaya kama Fernand Goyvaerts, Luc Nilis, Vincent Kompany na wengine.
Kukulia Ubelgiji kumemfanya Benteke awe mchezaji mahiri. Pia bendera ya Ubelgiji imemfanya aaminiwe na klabu za Ulaya na hatimaye kuwa tumaini la Liverpool. Shukrani zimwendee dikteta Mobutu aliyefanya Benteke kuhamishiwa Ubelgiji akiwa mdogo. Pasingekuwepo dikteta huyu Benteke angeishia kuichezea Motema Pembe ya Kinshasa. Mobutu amepeleka matumaini Anfield.
cassimbendera@gmail.com