MOTO wa soka umewaka barani Ulaya. Makumi ya timu wamekubaliana kuanzisha Ligi maalumu iitwayo European Super League ambayo inajumuisha vilabu vigogo vya soka batrani humo. mjadala wa kuanzishwa European Super League umekuwa mkubwa na kujikita kwenye masuala ya haki za televisheni na fedha. Makala haya yanakuletea masuala muhimu kuhusu European Super League.
Ni timu gani zimekubali kucheza European Super League?
Klabu 12 za Ligi mbalimbali barani Ulaya zimekubaliana kuanzisha Ligi yao ya Mabingwa. Klabu hizo ni; Manchester United, Tottenham Hotspurs, Real Madrid,Atletico Madrid, Juventus, AC Milan,Barcelona,Chelsea,Liverpool,Inter Milan, Man City na Arsenal. EPL inaongoza kuwa na timu nyingi ambazo ni Man City, Chelsea, Liverpool, Arsenal, Man United na Tottenham Hotspurs.
Je, timu za Ulaya hazitaki muundo mpya wa Ligi ya Mabingwa?
UEFA wanataka kupanua muundo wa mashindano hayo kutoka timu 32 hadi 36 kuania mwaka 2024 na kuendelea. Idadi ya mechi itaongezeka kwa asilimia 100 kutoka mechi 125 za sasa hadi 225 kwa muundo mpya. Pia wanataka mechi hizo kuchezwa kila mwezi wakati Ligi za ndani zikiendelea. Klabu zimekataa mpango mpya wa UEFA kwa sababu wanahofia endapo utakubaliwa na kutekelezwa maana yake utashusha thamani ya Ligi Kuu za ndani.
Chini ya muundo mpya wa UEFA, timu mbili kila msimu zitatoka Europa League na hatua za awali za nafasi za kufuzu Europa zitapelekwa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Utaratibu huo utatumika kote Ulaya, lakini ukweli ni kwamba utahusisha timu 400 zile zilizoko kwenye orodha ya ubora inayotolewa na UEFA.
Hilo litakuwa na maana timu zinazomaliza Ligi Kuu zikwa nafasi ya tano,sita au saba zitaingizwa daraja la timu za juu chini ya orodha ya timu bora zenye viwango vya UEFA. Nafasi mbili za Ligi ya Mabingwa zitaamuliwa namna hiyo kuanzia mwaka 2024 chini ya mapendekezo mapya ya UEFA.
Tanzaniasports imefanya uchambuzi wa mapendekezo hayo kulingana na viwango vya timu mbalimbali vilivyotolewa na UEFA kwa misimu ya 2019- 2020, 2018-2019 na 2017-2018. Kwa msingi huo timu zitakazonufaika na mapendekezo mapya ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zitakuwa kama ifuatavyo;
Msimu wa 2019-2020; timu za Tottenham Hotspurs (ilimaliza nafasi ya sita RPL) na AS Roma (ilimaliza nafasi ya tano Ligi Kuu Italia). Msimu wa 2018-2019; Timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya tano EPL, Sevilla ililazima nafasi ya sita La Liga. Msimu 2017-2018; timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya sita EPL na Sevilla ilimaliza nafasi ya saba La Liga.
Tatizo ni fedha za zawadi za mashindano
Tangu mwanzo European Super League imelenga kupata mapato makubwa kuliko ya sasa yanayotolewa na UEFA. Kwa waendeshaji wa European Super League wamepanga kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza anayetwaa ubingwa wa ligi yao kiasi cha pauni milioni 82. Msingi wa hoja hiyo ni kutokana na zawadi za UEFA, kwamba inatoa fedha ndogo kuanzisha zawadi za mashindano na mshindi wa kwanza, hadi haki za Televisheni na Streaming.
Je UEFA wamechukua hatua gani?
Shirikisho la,soka Ulaya nalo linatarajiwa kuziadhibu timu zote zilizokubaliana kuanzisha European Super League. Kwamba klabu zote 12 zitaadhibiwa kama ifuatavyo; zitaondolewa kwenye mashindano ya Ligi za ndani kuanzia msimu ujao, kila mchezaji atakayeshiriki European Super League atafungiwa kushiriki fainali za Kombe la dunia mwaka 2022, kila
kiongozi wa soka atakyejihusisha na European Super League atafungiwa kushiriki shughuli zozote za mashindano ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). UEFA itafungua mashtaka kudai fidia ya pauni bilioni 50 kwa kila klabu.
Je hofu ya UEFA ni nini?
Upo wasiwasi kuwa kupanuliwa kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa kutashusha thamani ya Ligi za ndani barani Ulaya kwa sababu mapato yanayotokana na matangazo yatakuwa makubwa zaidi hivyo kuwavutia wawekezaji zaidi. pia timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa huenda zikawa tajiri zaidi kuliko zingine zinazoshiriki Ligi ya ndani bila kufuzu mashindano hayo hivyo kuchangia mapato yao kuporomoka.
Majadiliano ya mapendekezo mapya yanahusisha vyama vya soka 55, Ligi Kuu za Ulaya na chama cha timu za soka. hata hivyo UEFA imepania kukamilisha mapendekezo hayo mapema kabla ya kufanikiwa mpango wa kuanzishwa kwa European Super League ambao unasimamiwa na Real Madrid.
Je ladha ya klabu zitakuwa zilezile kwenye soka?
Si jambo rahisi hadi sasa, kwa sababu sheria nyingi za Ligi za ndani zinawabana vilabu husika. Pia wapo makocha wanaopingana na wazo la kuanzisha European Super League, kwa mfano kocha wa Liverpool ambaye amesema, “Nategemea wazo hilo litakwama na halitotokea. Kwa mimi Super League tunayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kuna umuhimu gani kwa mfano Liverpool kupambana na Real Madrid kwa miaka 10 mfululizo? Hakuna mtu atakayetamani kuona hilo, linakinaisha,”
Kimsingi hoja ya Klopp ni sawa na kusema European League itakinaisha kuona Juventus na Madrid zinacheza mara kwa mara tena mfululizo kwa miaka 10 hivi. Hoja hiyo ni sawa na alivyowahi kusema Rais wa FIFA Giani
Infatino kuwa AFCON inakinaisha kwa sababu inachezwa kila baada ya miaka miwili badala ya kuwekwa miaka minne minne.
Je ni rahisi kuzifuta klabu zitakazojiunga European Super League?
Kimsingi miongoni mwa watu walioanzisha mpango huo ni rais wa Real Madrid, Florentino Perez, hivyo inaelekea wamejipanga vizuri. Fedha ndio kila kitu kwenye mashindano ya mpira wa miguu, kwa vyovyote vile walikuwa wanafahamu kuna vita kubwa itakuja na jinsi ya kukabiliana nayo. Haiwezekani vyama vya soka kuzifuta klabu hizo kwneye Ligi zao. Vilabu hivi vina mtaji mkubwa wa fedha na mashabiki hivyo kuwapa changamoto vyama vya soka.
Je tishio la UEFA na FIFA linatafsiriwa vipi?
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tmu zilizothibitisha kushiriki European Super League, Florentino Perez ameviambia vyombo vya habari kuwa hawaogopi vitisho vya mashiriko ya FIFA na UEFA, na tayari wamejipanga kuanzisha mashindano yao ya EURO kwa bara la Ulaya na Fainali za Kombe la Dunia.
Kwanini FIFA inakataa Ulaya na kutaka African Super League?
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, Giani Infatino anakumbukwa kwa kutoa wazo la kuanzisha mashindano ya African Super League, lakini ameungana na UEFA kukataa European Super League. Hii ina maana gani? Je FIFA walitaka kutumia African Super League kupima mambo katika uwanda wa soka?
Mchambuzi maarufu wa soka Afrika mashariki, Israel Saria anasema, “Mashindano ya soka huanzishwa yapate baraka za FIFA. Kwa bara la Afrika bado haliwezi kusimama peke yake bila kusaidiwa, hivyo kwa klabu za Ulaya zinataka kupandisha dau la mashindano ya Ligi ya Mabingwa, Michuano ya Euro na Kombe la Dunia,”