*Lukasz Fabianski ajiunga Swansea
*Arsenal watoa ‘posa’ kwa Di Maria
Bilionea Malcolm Glazer aliyenunua Klabu ya Manchester United na kuimilikisha familia yake ameafariki dunia.
Glazer (85) aliyezaliwa New York Marekani ameaga dunia katika msimu mbaya kuliko yote tangu ainunue klabu hiyo, na ingawa hajapata kukanyaga Old Trafford alikuwa akishughulikia shughuli zote hadi alipopatwa kiharusi.
Watoto wake, Joe na Avram ndio wamekuwa wakishughulika na klabu hiyo ambayo baba yao aliinunua kwa pauni milioni 790 mwaka 2005 katika dili tata lililopingwa sana na washabiki wa klabu hiyo nchini Uingereza.
Hata hivyo, tangu manunuzi hayo, Man U wametwaa ubingwa wa England mara tano na ubingwa wa Ulaya mara moja wakifundishwa na Alex Ferguson. Msimu uliomalizika chini ya David Moyes umekwua wa aibu, kwani wamemaliza ligi katika nafasi ya saba na kukosa ushiriki wa mashindano yoyote ya Ulaya.
Familia ya Glazer inamiliki asilimia 90 ya hisa za klabu hiyo ambazo zimegawanywa sawa sawa kwa watoto sita wa mzee Glazer huku asilimia 10 zikiwa zimewekwa kwenye Soko la Hisa la New York. Tangu kuanguka hadhi klabu hiyo biashara imekuwa haiendi vizuri na pia chapa ya United imeanguka.
LUKASZ FABIANSKI AJIUNGA SWANSEA
Kipa aliyemaliza mkataba wake Arsenal, Lukasz Fabianski amesaini mkataba wa muda mrefu na klabu ya Swansea iliyo Ligi Kuu ya England.
Fabianski (29) alikataa nyongeza ya mkataba Emirates kwa sababu kwa muda mrefu amekuwa kipa namba mbili, akisugua benchi licha ya kuwa kwenye kiwango cha juu na kuwsaidia Arsenal wakati kipa namba moja akiwa hayupo.
Raia huyo wa Poland amesema kilichomfanya aondoke ni kwamba anataka acheze kila wiki na anataka kuwa kipa namba moja, jambo linaloonesha uwezekano wa kipa namba moja wa Swansea, Michael Vorm kuhamia Liverpool ambao wamekuwa wakimsaka.
Vorm akihamia huko ataungana na kocha wake wa zamani, Brendan Rodgers lakini Swansea wanadai kwamba Liverpool hawajawasiliana nao juu ya suala hilo. Rodgers ndiye alimsajili Vorm hapo Liberty Stadium na sasa anataka ampeleke Anfield ili awe namba mbili wa Simon Mignolet.
ARSENAL WAPELEKA MAOMBI KUMSAJILI DI MARIA
Arsenal wameanza mchakamchaka wa usajili baada ya kupeleka maombi rasmi kwa Real Madrid ili kumsajili mchezaji wao, Angel Di Maria.
Hii ni mara ya pili kwa Arsenal kupeleka ‘posa’ kwani msimu uliopita walipeleka maombi ya kumsajili pamoja na Mesut Ozil na Karim Benzema, wakafanikiwa kumpata Ozil pekee. Arsenal wanataka kuimarisha eneo la ushambuliaji ambalo linaonekana kuwapa shida.
Di Maria, raia wa Argentina amesema anataka kuondoka Santiago Bernabeu licha ya kuwa na msimu mzuri na kutokea kuwa nyota wa mchezo kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wikiendi iliyopita, ambapo Real waliwafunga Atletico Madrid 4-1 na kutwaa kombe hilo.
Arsenal wanaelezwa kuwa mbele ya Manchester United na Manchester City wanaomtaka winga huyo wakati pia klabu ya Monaco ya Ufaransa imeelezwa kwamba inamtaka mchezaji huyo kama ilivyo kwa Juventus ya Italia.