Mkandarasi aliyepewa kazi ya kuufanyia ukarabati uwanja wa zamani wa Taifa ameutupia lawama uongozi wa uwanja huo kuwa wao ndio chanzo cha matatizo ya sasa ya uwanja huo.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya EKIKA iliyofanya kazi hiyo, Joseph Mushi, alisema kuwa wao hawahusiki na suala la miundombinu ya uwanjani hapo, ambapo kazi yao ilikuwa ni kutengeneza sakafu ya uwanja huo.
Mushi alisema kuwa anashangazwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa kampuni yao imeshindwa kuutengeneza uwanja huo, ambapo lawama zote zinapaswa kutupiwa uongozi wa uwanja kwa kuukataa ushauri wao juu ya kutanua mifereji ya uwanjani hapo.
“Nashindwa kuwaelewa tunatupiwa lawama kwa sababu gani, sisi kama EKIKA hatuhusiki na suala la mifereji kazi yetu ilikuwa ni kutengeneza sehemu ya kuweka nyasi bandia na ndio kazi tuliyoitekeleza, hayo mengine hayatuhusu,“alisema Mushi.
Alisema kuwa wakati wanafanya ukarabati wao walijaribu kuushauri uongozi wa uwanja kutanua mifereji yake ili kusafirisha maji kwa urahisi kitu ambacho hakikufanyika na badala yake mifereji iliachwa vile vile.
Mushi aliongeza kuwa watakuwa tayari kuifanya kazi ya kutanua mifereji endapo watapewa tenda upya ya kufanya kazi hiyo kama walivyopewa kazi ya kusawazisha uwanja.
Aidha, alisema katika kuondoa malumbano ni vema uongozi wa uwanja ukakaa pamoja na uongozi wa EKIKA ili kujadiliana jinsi ya kulitatua tatizo hilo kitaalamu.
Kwa upande wake Meneja wa uwanja huo, Charles Masanja, alisema kuwa suala zima la ubovu wa uwanja huo ameliacha mikononi mwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA),ambao ndio waliogharamia ukarabati huo.
Uwanja huo ambao mara baada ya kuwekwa nyasi bandia ulielezwa kuwa utaweza kutumika katika hali zote kitu ambacho ni tofauti kutokana na mara kwa mara kushindwa kutumika kufuatia sehemu kubwa ya uwanja kujaa maji pale mvua inaponyesha.