*Ni Kerr aliyecheza Leeds na Sheffield Wednesday
*Mzaliwa wa Malta aliyesafiri sana kwa ajili ya soka
Simba wamedhamiria kurejesha heshima iliyopotea kwa miaka mitatu Mtaa wa Msimbazi, kwa kusuka upya benchi la ufundi litakalokuwa chini ya Dylan Kerr atakayesaidiwa na yule wa viungo kutoka Serbia, Dusan Momcilovic.
Kerr (48), aliyezaliwa Malta kabla ya kuwa Mwingereza, ameingia mkataba wa kuwanoa Simba kwa mwaka mmoja, ambapo Rais wa Simba, Evans Aveva anasema wana imani kubwa na kocha huyo kutokana na wasifu wake, uwezo na mafanikio aliyopata kwenye timu alizopita kabla ya kutua Tanzania.
Wasifu wa Kerr unaonesha kwamba alizaliwa Januari 14, 1967 huko Valetta, Malta na amecheza mpira wa kulipwa akiwa mlinzi, ambapo alibobea kwenye beki ya kushoto. Anaingia Simba akitoka klabu ya Hải Phòng alikoenda kuanza kazi Januari mwaka jana.
Alianzia soka yake Sheffield Wednesday 1984 lakini hakucheza hata mechi moja ya ligi katika miaka mine aliyokaa Hillsborough, ndipo akaondoka na kwenda Afrika Kusini alikojiunga na klabu ya Arcadia Shepherds 1988.
Mwaka mmoja baadaye, Kerr alirejea England na kujiunga na Leeds United ambako alicheza mechi 13 tu a ligi katika miaka minne aliyokaa Elland Road chini ya kocha Howard Wilkinson. Leeds waliamua kumtoa kwa mkopo kwa klabu mbili; kwanza Doncaster Rovers alikoweka rekodi kwa kufunga bao lake la kwanza katika ligi.
Baada ya hapo alipelekwa Blackpool, ambapo katika miezi yake mitatu hapo alifunga moja ya mabao ya timu yake pale walipowanyuka watani wao wa jadi katika eneo la Lancashire – Burnley kwenye dimba la Bloomfield Road.
Mwaka 1993 alikwenda Mortimer Common na kujiunga na klabu ya Reading, iliyo katika eneo lenye Watanzania wengi na watu wa Afrika Mashariki kwa ujumla na huko ndiko alipata fursa ya kucheza mechi nyingi zaidi katika soka yake – 89, akifunga mabao matano.
Alikuwa kwenye kikosi cha Reading kilichotwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili (Championships) lakini pia alikuwamo waliposhina nafasi ya pili katika Ligi Daraja la Kwanza msimu uliofuata.
Kocha huyu wa sasa wa Simba, ilipofika mwaka 1996 alisajiliwa na klabu ya Kilmarnock iliyoko Uskochi ambako alicheza mechi 61 za ligi katika miaka minne. Katika msimu wake wa kwanza huko, alitwaa pamoja na timu hiyo ubingwa wa Scotland.
Kerr alikuwa na matatizo ya kujirudia rudia majeraha yaliyomfanya kuwa nje ya dimba kwa zaidi ya mwaka. Ni kwa sababu hiyo Kilmarnock waliamua kumwacha baada ya kuwa wamempeleka kwa mkopo Carlisle United.
Septemba 2000 alijiunga kwa muda na Kidderminster Harriers kwa mazoezi lakini mkataba wake wa mwezi mmoja ulikatizwa kwa maelezo kwamba alikwenda kinyume na kanuni za nidhamu za klabu, ndipo akarudi Uskochi na kusajiliwa na Hamilton Academical Januari 2001.
Katika miaka mitatu iliyofuata alichezea klabu za Exeter City (kwa mkataba wa miezi mitatu), Greenock Morton, Harrogate Town, East Stirlingshire na Hamilton Academical tena kabla ya kuhitimisha soka yake dimbani akiwa Uskochi na klabu ya Kilwinning Rangers 2003.
Baada ya kustaafu, Kerr alikwenda kufundisha nchini Marekani, kwa namna ya pekee Phoenix, Arizona kwa muda. Kwa kuwa hakupata visa ya kubaki nchini Marekani, alirudi Uskochi na kufanya kazi kama Ofisa wa Maendeleo ya Soka katika Halmashauri ya Argyll & Bute kati ya 2005 na 2009.
Septemba mwaka huo huo alisaini mkataba wa kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini alikodumu hadi Juni 2010. Mwaka 2012, Kerr alisaini mkataba wa kuwa kocha wa viungo wa Timu ya Taifa ya Soka ya Vietnam kabla ya kwenda Hải Phòng mwaka jana.
Kwa upande wa Momcilovic, klabu inasema kwamba amebobea katika kutoa mafunzo kwa mazoezi ya viungo na amefundisha klabu mbalimbali nchini Malaysia, Indonesia na Georgia alikokuwa kocha wa mazoezi ya viungo wa klabu ya FC Dinamo iliyocheza mechi za awali za Uefa, lakini pia amefanya kazi, Bosnia n& Herzegovina, Oman na Serbia.
Barani Afrika amefanya kazi na timu ya Sogor –Tobruk ya Libya. Amehitimu shahada ya mazoezi ya viungo Belgrade akiwa amejikita kwenye mazoezi ya viungo na kujenga mwili.
” Klabu ya Simba inafuraha kubwa kuingia mkataba na kocha Dušan Momčilović mwenye uzoefu na weledi wa kutosha, tunaamini atakuwa chachu ya mafanikio pia kunoa vipaji vya wachezaji wa Simba,” imeandika tovuti ya Simba.
Simba wanashiriki michuano ya ndani tu msimu ujao, kwani wameshindwa kupata ubingwa au ushindi wa pili, hivyo wanatakiwa kujipanga upya, ili waweze kuanza tena safari za nje ya nchi.
Kwa miaka mitatu sasa hawajapata kupambana kwenye michuano kama ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Shirikisho la Klabu Bingwa Afrika, nafasi zinazokamatwa na Yanga ambao ni mabingwa na washindi wa pili, Azam