Menu
in

Mipango ya Burundi iwe somo kwa sekta ya michezo Tanzania

Mike Tresor Ndayishimiye

Sekta ya michezo ni eneo lingine la biashara,utalii na chanzo kikubwa cha mapato  ya serikali mbaliimbali duniani. Kodi hukusanywa kupitia wachezaji,makocha,haki  za televisheni na maeneo mengine. 

Michezo ya aina mbalimbali kwenye mashindano huwa chachu ya kuinua hali ya  maisha ya wachezaji, walimu,wadau na watalaamu. Kusema hivyo ndiyo maana  baadhi ya nchi zimekuwa zikiwekeza kwa kiwango kikubwa.  

Mashindano kama Olimpiki, riadha ya Diamond League, IAAF, Ligi za soka, mbio  za magari na mengineyo yamekuwa chachu ya kiuchumi kwa nchi tofauti. Hii  ndiyo maana baadhi ya serikali zinaingia gharama kuhakikisha zinawezesha  upatikanaji wa huduma fulani ama baadhi ya raia kupewa kipaumbele kupiia  michezo na kadhalika.  

Ndiyo sababu serikali ya awamu ya nne nchini iliamua kulipa mishahara ya  makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo Marcio Maximo. Hata hivyo  juhudi za kuboresha sekta ya michezo zimekuwa hafifu na inaelekea haijatiliwa  mkazo ili kuleta matokeo chanya. 

Tanzania inao wachezaji wengi katika ngazi tofauti wanaocheza michezo  mbalimbali kuanzia soka, riadha, floor ball na mingine mingi lakini wanashindwa  kuiwakilisha Tanzania kwa vile hakuna ruhusa ya uraia pacha. Kizazi chenye asili  ya Tanzania hakijapewa nafasi kurudi na kuimarisha sekta ya michezo. 

Tanzania Sports
Gael Bigirimana

Kwa mfano, wapo raia wa Tanzania ambao wanaishi nchi za Ulaya, Asia na  Amerika, ambao wana watoto wenye vipaji vya michezo mbalimbali. kizazi hicho  ambacho kingeweza kutumika kuleta mafanikio kwa nchi yetu kimejikuta kikiwa  nje ya mfumo wa sekta ya michezo kutokana nan chi yetu kushindwa kutengeneza  utaratibu wa kuwatumia.  

Wapo wanasoka ambao wamezaliwa kwa wazazi kutoka Tanzania katika nchi za  Ulaya na wamekuwa wakichagua mataifa kuwakilisha mataifa kama vile Denmark,  Sweden Finland, Uswisi, Ujerumani, Uingereza kwenye michezo badala ya 

Tanzania. kukosekana utaratibu huo ndio sababu inayoleta swali ni kwa namna  gani Tanzania inaweza kujifunza kwa jirani zao Burundi? 

Utaratibu wa sekta ya michezo nchini Burundi ni kuhakikisha kocha wao wa timu  ya taifa anakuwa na rasilimali zote iwenye timu hiyo ili kuleta mafanikio katika  kandanda. Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka Burundi amepewa fursa ya  kutekeleza mipango ya soka nchini humo kwa kuzunguka nchi za Ulaya na nje ya  Ulaya akitafuta watoto wenye asili ya Burundi waje kusaidia timu ya taifa ya  Burundi. 

Kocha wa Burundi amefanikiwa kuwashawishi mastaa kama Saido Berahino na  Gael Bigirimana ambao wote walikuwa wameshachezea timu za taifa za Uingereza katika ngazi tofauti.  

Kocha wa Burundi amefanikiwa pia kumleta Marco Waymans ambaye alikuwa  ameshachezea timu ya taifa ya Ubelgiji ya Vijana, naye kama walivyo mastaa  wengine akakubali kuichezea timu ya taifa ya Burundi. 

Aidha, kocha huyo amezidi kutanua mipango kwa kufanikiwa kumleta Thilo  Kehrer anayekipiga katika klabu ya PSG ya Ufaransa kwenda kuchezea timu ya  taifa ya Burundi, bahati mbaya kabla ya kuanza utekelezaji wa zoezi hilo serikali  ya Ujerumani ikamshawishi kijana huyo achezee nchi yao, naye akageuza mawazo  na kuiacha Burundi. Ingawa jaribio la kumpata Thilo halijafanikiwa lakini Burundi  wameonesha wazi mikakati yao kwenye michezo na kwamba wanataka kuleta  mafanikio ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo. 

Hivi karibuni kocha huyo pia amefanikiwa kumleta kijana mwingine Mike Tresor  Ndayishimiye ambaye amewahi kuchezea timu ya taifa ya vijana ya Ubelgiji, naye  tayari ameshakubali kusaidia Burundi nchi walikotoka wazazi wake.  

Shirikisho la soka la Burundi wana mipango ya kuwaita vijana wote wenye vipaji  vya soka wenye asili ya nchi hiyo kuchezea timu ya taifa. Vijana wote wanaocheza  vilabu vya Ulaya wanatakiwa kuwekwa kambini ili wachague wachezaji wazuri  waingizwe kwenye timu ya taifa. Malengo ya Burundi ni kuhakikisha wanacheza  fainali za Kombe la dunia mwaka 2026 na wameanza kuandaa vijana. 

Unapoona mikakati ya namna hiyo maana yake imebarikiwa na serikali. Kwamba  serikali imeamua kwa kauli moja na utashi kuwa ni wakati wa kuwarudisha kizazi  chenye asili ya Burundi kuleta manafaniko. 

Nikitazama nchi yetu namna tunavyoendesha soka letu, sioni dalili za kuchukua  mkondo kama huu kuhakikisha wachezaji wenye vipaji ambao wanataokana na  kizazi cha watanzania wanaoishi nje ya nchi. Sioni mipango ya kuwafuatilia ama  kuwa na mpango wa kuwachukua vijana wenye vipaji ili waje kutumikia Taifa  Stars.  

Sioni hayo, lakini taifa dogo la Burundi ambalo tumewazidi mambo mengi  kisoka, kiuchumi,ulinzi na kadhalika wanachukua hatua madhubuti na kutekeleza  mipango yao. Ni lini serikali ya Tanzania itakuwa na utashi kuhakikisha inaweka  utaratibu ambao unawezesha kuwachukua vijana wenye vipaji kuchezea timu zetu  za taifa? 

Ni lini shirikisho la soka TFF litakuwa na mpango wa kuhakikisha linajikita  kuwaibua na kuwachukua wachezaji wenye asili ya Tanzania kuchezea nchi ya  wazazi wao ama wao wenyewe?

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version