“Usoni mwake kuna alama au dalili za maisha yake ya nyuma, ambayo hayakuwa mazuri”
Hatimaye kitendawili cha umri wa msakata ndinga wa Lazio, Joseph Minala kimeteguliwa kwa kuhakikishwa kwamba umri wake ni miaka 17 si 42 iliyodaiwa na Tovuti ya Soka ya Afrika.
Kiungo huyo alikuwa akichunguzwa na Chama cha Soka Italia baada ya yeye kudai ana umri wa miaka 17 lakini usoni akaonekana kuwa na makunyanzi kama mtu aliyevuka sana umri huo. Wataalamu wanasema kwamba ‘uzee’ unaonekana usoni mwake kwa sababu ya maisha ya dhiki siku zilizopita.
Minala alizaliwa Cameroon na alijiunga na klabu hiyo ya jijini Roma msimu uliopita wa kiangazi na kuwachezea katika mashindano ya vijana Februari mwaka huu, huku watu wengi wakishangaa ikiwa kweli ni kijana.
Lazio walikuwa wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote aliyekwua akihoji uhalali wa mchezaji wao huyo kushiriki mashindano hayo na pia dhidi ya madai kwamba ana umri wa miaka 42, yaani miaka 25 zaidi ya umri wake halali.
Klabu hiyo imesema kwamba imepata hata cheti chake cha kuzaliwa ambacho walikipeleka kwenye chama cha soka na baada ya hapo watashughulika na yeyote atakayeendeleza propaganda za kumchafua kijana huyo juu ya umri wake.
Mtandao huo ulidai kwamba Minala alikiri kuwa umri wake wakati huo ulikuwa miaka 41 na hivyo sasa amefikisha 42 lakini yeye anakana kuzungumza na watu wa tovuti iliyotoa habari hizo.
“Usoni mwake kuna alama au dalili za maisha yake ya nyuma, ambayo hayakuwa mazuri. Ni hivyo tu. Hakuna kitu kingine chochote kinachoweza kumtonya mtu kwamba eti ana miaka zaidi ya 40. Ukiangalia kichwa chake ni cha kijana.
“Lakini acheza kwa kasi sana hata anapozungukwa na wachezaji wengi, mchezaji wa umri huo hangeweza kuwa na makeke kama huyu,” anasema mwanahabari Max Evangelista ambaye ni Mtaliano.
Minala anaelezwa kwamba ni yatima na aliishi maisha ya tabu sana mitaani nchini mwake kabla ya kupelekwa kituo cha watoto yatima kabla ya kubahatika kucheza soka barabarani kisha akapelekwa kwenye viwanja, akapanda chati hadi kupelekwa Italia.