Menu
in ,

MIKONO YA KABWILI INAPINGANA NA HUKUMU YETU KWAKE

Tanzania Sports

Nilikuwa naangalia marudio ya mechi ya Saint Louis na Yanga
iliyochezwa Usherisheri.

Katikati ya mechi nilibaki naangalia umbo la golikipa wa Yanga, Youthe
Rostand. Umbo ambalo linamfaa golikipa yoyote kuwa nalo.

Kimo chake kizuri , kimo kinachompa sifa ya ziada kama golikipa. Kuwa
na umbo zuri hakutoshi kukufanya kuwa golikipa bora.

Kuna vitu vingi vya ziada ambavyo unatakiwa upigane kuvipata kwa
kufanya mazoezi ili uweze kuwa golikipa bora kwenye mpira wa miguu.

Inawezekana msimu jana alionesha kiwango kilichovutia akiwa Africa
Lyon, lakini ni ukweli usiopingika kuwa msimu huu amekuwa na kiwango
ambacho siyo kizuri ukilinganisha na ƙkiwango alichokionesha akiwa na
African Lyon msimu jana.

Youthe Rostand anakosa mtu wa kushindana naye kwenye kusaka namba
katika timu ya Yanga ndiyo maana hana uchungu wa kuona kila siku
anatembea kurudi nyuma.

Amekuwa na madhaifu mengi sana kwenye baadhi ya michezo ambayo
amefanikiwa kukaa langoni.

Kwake yeye hata mipira ya chini imekuwa tatizo ndiyo maana mechi dhidi
ya Ihefu Fc alisababisha iwe ngumu kwa Yanga na kusubiri mpaka mikwaju
ya penati kuwatoa Ihefu FC.

Habib Kiyombo alijaribu kuwaonesha Yanga madhaifu ya Youthe Rostand
pale CCM Kirumba, lakini benchi la Yanga halikushtuka likazidi
kumwamini.

Kumwamini kwao kunatokana na sababu moja tu nayo ni uzoefu , ana
uzoefu katika udakaji lakini mikono yake haijakua.

Mikono yake ina umri mdogo ukilinganisha na umri wake halisi ndiyo
maana siyo mwepesi hata anapokuwa anaamua kudaka mipira ya juu.

Kuna wakati maamuzi yake huwa mazito, huchukua muda mrefu mpaka
kufanya maamuzi kitu ambacho kinadhihirisha siyo mkomavu kwenye akili
yake na mikono yake.

Kuwa na umri mkubwa haimanisha waweza kufanya maamuzi yaliyokomaa,
kuna wakati mtu mzima hufanya maamuzi yasiyo na ukomavu na mtu mwenye
umri mdogo akafanya maamuzi yaliyokomaa

Ndiyo maana pale Yanga kuna watu Ramadhani Kabwili mwenye umri mdogo
na Youthe Rostand mwenye umri mkubwa lakini maamuzi yao
yanatofautiana.

Pamoja na kwamba tunamhukumu Ramadhani Kabwili kama mchezaji asiye na
uzoefu kutokana na umri wake lakini mikono yake inatupa majibu tofauti
na hukumu yetu.

Mikono yake inaonesha ukomavu mkubwa ambao tunaukosa kwa Youthe Rostand.

Jicho lako likiwa linashuhudia namna Youthe Rostand anavyoadhibiwa kwa
magoli ya mbali, hadithi huwa tofauti kwa Ramadhani Kabwili ambaye
kwake yeye mipira ya mbali ndiyo mipira ya kuonesha umwamba wake.

Umwamba ambao huufanya hata kwenye maamuzi yenye uharaka wa kudaka
mipira ya juu inayotokana na ƙkona pamoja na mipira ya krosi.

Kuna wakati timu huzidiwa, wachezaji wa ndani wanaweza wakawa wamekata
tamaa lakini mtu pekee ambaye hastahili kukata tamaa ni golikipa,
golikipa ndiye mtu pekee ambaye anaweza rudisha morali ya wachezaji
wenzake au kushusha morali ya wachezaji wenzake.

Pamoja na umri wake wa miaka 18 Ramadhani Kabwili ameonekana kuwa
kiongozi mbele ya wachezaji viongozi tena wakongwe kama kina Kelvin
Yondani.

Amekuwa akiwapanga vizuri kipindi timu inaposhambulia au kipindi
ambacho timu inaposhambuliwa, ni ngumu kuona timu ikifungwa kutokana
na mabeki kutojipanga vizuri kama goli ambalo Majimaji walifunga
kwenye mchezo wa FA katika hatua ya kumi na sita bora 2017/2018.

Ni kawaida kwa mchezaji kutoka nje ya mchezo kwa dakika kadhaa, lakini
ni kwa namna gani anaweza kurudi kwa wepesi kwenye mchezo.

Kabwili anapotoka mchezoni uwahi kurudi haraka na kuendelea kuiweka
akili yake ndani ya mchezo.

Ni mdogo kiumri lakini ana akili ya kuitunza na kuilea familia,
Donnarruma kaanza kudaka akiwa na miaka 15 mpaka leo hii ni baba wa Ac
Milan, ni wakati sahihi kwa Kabwili kupewa jukumu la kuitunza rasmi
Yanga

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version