Menu
in , , , ,

Mikel Arteta anafundisha soka lake

Mikel Arteta bado anadaiwa na Arsene Wenger

Mikel Arteta bado anadaiwa na Arsene Wenger

UNAWEZA kutumia maneno yote kumkosoa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta na benchi lake la ufundi, lakini kamwe huwezi kukikiri kuwa dunia ya makocha imeishiwa ubunifu ndiyo maana kila mmoja anataka kucheza soka la Pep Guardiola. Kabla hujamlaumu kocha wa Arsenal hebu tazama ya aina soka linalochezwa kwenye vilabu vingi kama vile Man City, Chelsea, Man United, Girona, Barcelona na hata Lille utaona kila kocha anataka kucheza kama Pep Guardiola. 

Kama ambavyo amewahi kusema nyota wa zamani wa Man United, Patrice Evra kwamba Pep Guardiola anaua soka la dunia, kila kona hakuna ubunifu wowote unaofanyika badala yake makocha wengi wanataka kucheza mifumo wa Mhispania huyo. Kwanza tukiri kuwa Pep Guardiola ni kocha mzuri na amefanikiwa kuendeleza falsafa ya soka toka kwa Johan Cruyff aliyotoka nayo Ajax Amsterdam na kuipeleka Barcelona. 

Makocha wanatamani kucheza kama Pep na kuwafanya wakose ubunifu. Hicho ndiyo ambacho kiinawafanya makocha wengine kutafuta kila aina ya ubunifu kuhakikisha wanaweka alama kwenye soka. Katika hali ya kukosa ubinifu hata nyota wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel amekosa uelewa juu ya kile anachokifanya Mikel Arteta na kikosi chake cha Arsenal. 

Je kuna tofauti ya Arsenal katika utawala wa Arteta?

Jibu ni ndiyo. Mikel Arteta amefanya mambo mawili kabla ya kuja na la tatu. Jambo la kwanza liahitaji kuunda timu yenye ushindani dhidi ya Man City. Jitihada hizo zilimfanya aambulie vichapo mara nyingi kutoka kwa bosi wake wa zamani. Arsenal ilikuwa inatandaza soka kama Man City, ukaibuka upinzani mkali baina ya vilabu hivi. Bahati mbaya Mikel Arteta alikuwa anashuhudia kikosi chake kikiruhusu mabao mengi. 

Timu inaweza kushinda 3-2 au 4-3 au kutoka sare 3-3 na kulifanya lango lake likose ulinzi. Aliamua kubadilisha aina ya golikipa kwa kumwondoa Aaron Ramsdale, kisha akaimarisha safu ya ulinzi ili kupunguza mabao ya kufungwa. Tofauti na mwanzoni alikokuwa na mipango ya kushambulia pekee, bali awamu ya pili aliweka mkakati wa kuzuia magoli kuingia langoni mwake.

Ujio wa mpango wa pili

Arteta hakuishia tu kupunguza mabao, bali kutazama namna mpya ya uchezaji wa mechi ngumu ambazo zinahitaji akili ya ziada. Kwanza alisuka safu ya ulinzi kucheza mbinu nyingi za gizani (Dark arts) ambazo ni maarufu kwa safu ya ulinzi ya Real Madrid kwa miaka mingi sana. safu ya ulinzi ya Arsenal ilibadilika kutoka kuwa legelege hadi ngome imara zaidi. 

Mabeki wake walionekana kucheza soka la shoka na ile roho ngumu nay a kikatili ilionekana wazi wazi machoni pa Gabriel na mwenzake William Saliba. Angalau William Saliba anaonekana kama ‘Mr.Nice Guy’, lakini kwa siri anacheza kihuni mno. Gabriel akawa beki wa fujo, aliweza kupambana mipira ya juu, alipiga tackle nyingi na baadaye wakaifanya ngome ya Arsenal kuwa imara. Ni sababu hiyo Arsenal wamejikuta wakikosa ubingwa kwa tofauti ya pointi chache tu.

Ubunifu wa kufundisha makocha duniani

Benchi la ufundi la Arsenal kwa sasa linalaumiwa kwa kuwafundisha wachezaji wake kusaka mabao kwa njia ya kona. Mabao mengi ya Arsenal msimu huu katika mechi ngumu au za kawaida yanapatikana katika kona. Kwa mfano kuna timu unapaswa kuhakikisha unazuia kila uwezavyo ili zisipate faulo karibu na lango lako. 

Uholanzi kwa miaka mingi walikuwa mahiri katika eneo hili, kwao mipira ya adhabu ndogo au kona ilikuwa mwanya wa kupachika mabao. Katika ngazi ya klabu AC Milan, Inter Milan ni miongoni mwa vilabu ambavyo vina historia nzuri katika mabao ya kona. Katika eneo hili, timu nyingi zina makocha wenye jukumu la kufundisha namna bora ya kupiga mipira ya faulo na kona ili kupata mabao. 

Kwa aliyetazama Arsenal msimu huu atagundua kuna wachezaji wanafanya mambo makubwa ya kiufundi wakiwa kwenye lango la adui wakati wa upigaji kona. Wachezaji wanne wa Arsenal wanajipanga mstari mmoja wakiwa nyuma ya mabeki wa timu pinzani. Kama kona inapigwa upande wa kushoto, basi wachezaji wanne wa Arsenal wanajipanga upande wa kulia kwenye eneo la hatari. Mpira wa kona unapopigwa upande wa kulia, pia wachezaji wanne wanajipanga mstari upande wa kushoto eneo la hatari na mchezaji mwingine anakwenda kusimama mbele ya golikipa wa timu pinzani. 

Mpira unapopigwa kuelekea eneo la hatari wachezaji wanne hao wanakimbilia eneo la hatari wakiwa wameongozana kisha wawili wanaeleka upande mwingine na wawili wanabaki mita chache toka anaposimama golikipa na kuwa watatu na yule anayesimama mwanzoni. Kiujumla utaona kuna wachezaji watano katika eneo la golikipa na mpira unatua hapo kisha huruka kwa vichwa au piga nikupige nyingi zimewapatia mabao. Mara nyingi timu pinzani zinajisahau katika hili na hawajui namna ya kuwazuia. Hapo ndipo Mikel Arteta anapowafundisha makocha mbinu mpya za kuipa ushindi timu yake. Mikel anataka kutumia kila nafasi ya kona na faulo kuhakikisha wanapata bao. Kwa hili anastahili kupongeza sio kukejeliwa.

Arteta ameachana na dhana mbovu za Pep Guardiola

Timu ya Pep Guardiola ina udhaifu wa kufunga mabao ya faulo. Hata kabla ya ujio wa mshambuliaji Erlin Haaland ambaye mara kadhaa amejitahidi kufunga kwa vichwa lakini kama angelipata timu inayothamini mipira ya adhabu hiyo bila shaka angekuwa mbali kirekodi. Pep Guardiola mara nyingi timu yake ina udhaifu wa kutumia vizuri mipira ya kona. 

Tuseme katika eneo la kona timu za Guardiola hazina ubunifu wowote, kwahiyo Arteta amepita njia yake na kufichua kuwa inawezekana kutumia na kuipa ushindi timu yake. Pep kila mara anataka zipigwe pasi nyingi mno na wakati mwingine hazina uhuni ambao unaweza kumletea ushindi. Kifupi hawezi kutafuta ushindi katika mazingira ya kihuni au kimtaa. Sasa, Arteta amekuja na kitu kipya na ambacho muda si mrefu kitampa sifa nzuri kuliko lawama anazopewa sasa. 

Makocha wamebweteka mno

Tatizo dunia imeishiwa makocha wabunifu ndiyo maana wengi wanaiga kila anachofanya Pep Guardiola na kukiona ndicho kitu kizuri zaidi. Kifupi makocha wamebweteka mno kiasi kwamba ubunifu mpya wa Arteta unalalamikiwa utadhani wao wanao wa kwao. Ni vizuri kuelewa kuwa kocha huyu amekuja kivyake, na kuonesha kuwa anaweza kubuni na kuleta kuleta kitu kipya katika mchezo wa soka.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version