Tarehe 5 mwezi wa 2 mwaka 1992 ardhi ya Sao Paulo ilipokea kiumbe kipya. Kiumbe ambacho wakati kinatoka ilikuwa ngumu kujua kitakuja kufanya nini duniani.
Tabasamu kubwa pekee lilifunika uso wa mama yake, lakini mama yule ambaye muda mchache alitoka kusikia uchungu wa kuzaa alikuwa bado hajui mwanaye atakuja kuwa nani kwa baadaye.
Inawezekana kama ilivyo matamanio ya Wabrazil wengi, pasina shaka mama yule asilimia kubwa ya matamanio yake alikuwa anatamani mwanaye aje awe mwanasoka bora duniani.
Kama ilivyo kwa desturi ya Wabrazil mpira kwao ni utamaduni. Kila nyumba kuna mchezaji wa mpira wa miguu awe wa ligi ya kulipwa au ya kutolipwa.
Mpira kwao ni utamaduni, utamaduni ambao waliubatiza kwa jina la Samba, ndiyo maana nina amini kwa asilimia kubwa matamanio ya mama yule aliyekuwa ameshikilia kichanga alikuwa anatamani kichanga kile kicheze mpira.
Dunia ilikuja kumfunua Neymar rasmi, ilimfunua kama mchezaji mpira wa miguu. Tena mchezaji ambaye alikuwa anafananishwa na watu ambao walikuwa kama nembo ya mpira kwa muda mrefu.
Kabla ya ujio wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Diego Maradona pamoja na Pele walisimama kama nembo halisi ya mpira wa miguu.
Yani ilikuwa ukiwataja wao unakuwa unaonesha maana halisi ya neno ya mpira wa miguu. Kwa kifupi tafasri halisi ya neno mpira wa miguu ilikuwa kwenye picha ya hawa magwiji.
Magwiji ambao walikuwa na vipaji vya pekee. Vipaji ambavyo viliifanya dunia iwaimbe sana. Nyimbo za kusifu na kuabudu vipaji vyao zilitungwa nyingi sana.
Kwa sababu tu walikuwa na vipaji vya kipekee. Upekee ambao wengi waliuona katika miguu ya Neymar. Macho ya walio wengi yaliamini Neymar ndiye atakayekuja kuwa Pele mpya.
Tulimpa muda , na yeye akatuonesha kwanini anastahili kuwa Pele mpya. Aliitumikisha sana miguu yake kiasi kwamba akiwa na umri mdogo wa miaka 17 alienda na timu ya taifa kushiriki michuano ya Olympic.
Michuano ambayo ilimfanya afunge hat trick yake ya kwanza. Hat-trick ambayo ilikuwa kama mlio wa tahadhari kuwa kuna mdudu mpya kwenye soka anakuja.
Tulimsubiri sana aje, tulikuwa na hamu pamoja na bashasha kubwa sana. Na yeye alikuwa anakimbia kwa kasi kutufikia karibu na matamanio yetu.
Akiwa na miaka 20 pekee alifanikiwa kuwa mchezaji bora wa bara la America. Hapo ndipo ukawa mwanzo wa vingi kutokea.
Hapo ndipo ukawa mwanzo wa vita kuu ya usajili kuanza. Vita ambayo ilihusisha vilabu ambavyo kila mwanadamu anayecheza mpira wa miguu anatamani kwenda kucheza.
Vilabu ambavyo ni Hija ya soka, kila mchezaji anatamani kufanya ibada ya kuhiji, Realmadrid na Barcelona.
Lakini mwisho wa siku Barcelona ilifanikiwa kuifanya miguu ya Neymar kukanyaga nyasi za Camp Nou kwa muda mrefu.
Akawa anasogea karibu na ndoto zake, akawa anasogea karibu na matamanio yake. Kusogea kwenye sayari halisi ya mpira wa miguu (Barcelona) kulitoa matumaini ya yeye kubeba Ballon D’or.
Kitu ambacho amekuwa akikiota kwa muda mrefu. Hiki ndicho kitu anachokitamani sana. Unaweza ukaona labda yeye kupigania kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa Brazil ndicho kitu ambacho anakitaka.
Ana magoli 60 mpaka sasa hivi nyuma ya Pelle na Ronaldo De Lima. Lakini hii hata haimuumizi kichwa. Kichwa chake kinawaka moto kila anapofukiria neno Ballon D’or.
Alikaribia kuichukua mwaka 2015 alipoingia tatu bora, lakini mwisho wa siku kikwazo kilikuwa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.
Hawa wameitawala hii tunzo kwa muongo mmoja. Tangu Kaka ambaye ndiye Mbrazil wa mwisho kushinda Ballon D’or mwaka 2007 hakuna mchezaji yeyote zaidi ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambaye alishinda tunzo hii.
Luka Modric ndiye amekuja kuvunja utawala huu, ameshinda akiwa katika siku zake za mwishoni katika soka. Miaka 32 na kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kushinda Ballon D’or.
Hana maisha marefu tena. Inawezekana kwa kiasi kikubwa ikawa Ballon D’or yake ya kwanza na ya mwisho.
Na pia hii inawezekana ikawa kengele ya kumwamsha Neymar usingizini kuwa anaweza akatimiza ndoto yake ya siku nyingi.
Kuna uwezekano wa kushinda Ballon D’or mbele ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Natumaini kuna matumaini mapya ambayo yamezaliwa ndani ya moyo wa Neymar baada ya Luka Modric kushinda Ballon D’or.
Dani Alves aliwahi kusema kuwa kocha pekee ambaye anaweza kumsaidia Neymar kushinda Ballon D’or ni Pep Guardiola.
Mimi naamini, kwa Neymar kwenda PSG amejiweka mbali na uso wa Ballon D’or. Anatakiwa kurudi kwenye sayari halisi ya mpira wa miguu. Sayari ambayo itamwezesha kushinda kitu ambacho kinamuumiza usingizi kila uchwao.