WAJERUMANI wameumizwa kwa kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa vijana wa Blue Samurai. Ni kipigo kilichowakumbusha Ujerumani kwenye michezo ya fainali za Kombe la Dunia mnamo Desemba mwaka 2022 ambako walitupwa nje ya mashindano na vijana hawa wa Bule Sumarai. Ni vijana wa Japan, ambayo ilikuwa mwenye wa fainali za kombe la dunia mwaka 2002 ikishirikiana na Korea kusini. Kipigo cha mabao 4-1 kililiamsha shirikisho la soka la Ujerumani, DFB na kuchukua uamuzi wa kumfukuza kocha wao Hans Flick. Ni kocha ambaye aliwahi kuwaongoza Bayern Munich kuwachakaza mabingwa wa Hispania, Barcelona kwa mabao 8-2 kwenye Ligi ya Mabingwa. Alikuwa na mafanikio akiwa klabu ya Bayern Munich. Kila klabu hiyo ilipopata ushindi mnono kwenye Bundesliga lakini hakuonekana kutabasamu.
Hata Bayern Munich ishinde mabao matano, lakini uso wake ulibaki vilevile. Hans Flick alikuwa kocha wa aina yake. Ameacha alama ya uso mkavu hata pale timu yake ilipokuwa inafanya vizuri. Lakini alipohamia katika ngazi ya Timu ya Taifa mambo yamekwenda shelabela. Sasa Mkurugenzi wa Ufundi wa chama cha soka cha Ujerumani, DFB Ruud Voller amekabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho kuelekea kwenye mchezo wao dhidi ya Ufaransa.
Sababu zipi zimetumiwa na DFB?
Hansi Flick amefukuzwa kazi ya ukocha nchini Ujerumani akiwa kocha wa kwanza kutimuliwa. Historia inasema ndiye kocha wa kwanza wa Timu ya Taifa kufukuzwa katika kiti hicho. Aliongoza Ujerumani katika michezo 25, ameshinda michezo 12. Timu za mwisho kuzifunga ni Oman, Costa Rica, Peru ndizo zilizofungwa na Ujerumani katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Wastani unaonesha kuwa hana mafanikio katika kikosi cha Ujerumani hali ambayo inawatia hofu viongozi wa DFB pamoja na wadau. Kabla ya mechi dhidi ya Japan, kocha huyo alipewa mechi mbili kuamua mustakabali wake kwenye kiti cha ukocha wa Ujerumani. hata hivyo DFB imeshindwa kuvumilia na hivyo kufuta ajira yake.
Miezi 9 kabla
Ujerumani ndiye mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya au maarufu kwa jina la Euro (Euro 2024). Ikiwa kama mwenyeji wa fainali hizo, Ujerumani imekuwa kwenye mawindo ya kutengeneza kikosi cha kuibuka na ushindi ikiwemo kunyakua kombe hilo. Miezi 9 kwa maandalizi na mipango ya timu hiyo imekuwa ya kusuasua licha ya kuzungukwa na wachezaji wengi wenye vipaji. Katika kipindi hiki Ujerumani inaonekana kuhofia nini kitatokea kwenye michuano ikiwa wangeendelea na kocha Hans Flick.
Kumekuwa na tetesi kwamba Ujerumani wanatamani kumpata Jurgen Klopp wa Liverpool lakini upo ugumu kumng’oa kocha huyo. Kwa upande mwingine Ujerumani wanatama kuwa na kocha wa muda mrefu, ambaye atakuwa na mipango ya kuimarisha kikosi zaidi ya fainali za Euro 2024. Kwahiyo DFB wanataka kombe la Euro lakini wakati huo wanataka kocha wa muda mrefu, huku wakitamani huduma ya gwiji Jurgen Klopp ambaye kuondoka Liverpool ni kama kitu kisichowezekana. Suluhisho ambalo wanaweza kulipata ni kumpa kandarasi ya muda mfupi, nayo itategemea kama Liverpool watakubaliana nao.
Wachezaji wapo?
Hili ndilo swali wanalotakiwa kujibu Wajerumani. Je wanacho kizazi chenye uwezo wa kulinyakua kombe la Euro? Ikiwa hivi leo Ujerumani wanategemea huduma ya wachezaji ambao wanaonekana dhahiri wapo chini ya ubora au kutokuwa na kiwango ni vigumu kulipigania kombe. Nahodha wa Ujerumani Ilkay Gundogan, ni mchezaji mkongwe, halafu ukitazama sura nyingine kikosini ni Kai Harvetz, Jamal Musiala na wengine ambao hawana umahiri kama ilivyozoelekea kwa Ujerumani. Umwamba wa Ujerumani katika Timu ya Taifa unaelekea kuondoka na Joachim Loew aliyepokea kibarua kutoka kwa Jurgen Klinsmann mwaka 2006.
Ni kipindi cha mpito?
Ujerumani kama walivyo Italia, Ureno na Hispania wapo katika kipindi cha mpito kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Wapo wachezaji waliokuwa mahiri miaka kadhaa iliyopita, lakini hivi leo hawaonekani kuwa imara. Ujerumani inahangaika kurudisha makali yake, kama ilivyo kwa Ureno ambao walichapwa na Morocco kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la dunia, huku Hispania nao wakifungasha virago katika mazingira ya ajabu. Kufika hapo unaona ni kipindi cha mpito ambacho makocha watafukuzwa maradufu.