*England waongoza, Kenya nao watamba
*Mataifa madogo kabisa yaizidi Tanzania
Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyomalizika jijini Glasgow, Uskochi imemalizika kwa England kuibuka kidedea, wakizoa jumla ya medali 174, wakifuatiwa an Australia na Canada.
Baada ya siku 11 zilizokutanisha wanamichezo mbalimbali kwenye michezo tofauti 17, pazia lilishushwa Hampden Park huku wenyeji wakishika nafasi ya nne, ambayo kwa udogo kijiografia si haba.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola, Mike Hooper alisema kwamba michezo hii ndiyo iliyofana zaidi katika miaka 84 ya historia yake. Scotland walipata medali 19 za dhahabu, idadi ambayo hawakupata kutwaa katika mashindano mengine.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 28, England walishika usukani kwa medali 58 za dhahabu, 59 za fedha na 57 za shaba.
Australia walinyakua 49 za dhahabu, 42 za fedha na 46 za shaba huku Canada wakiwa na 32 za dhahabu, 16 za fedha na 34 za shaba.
Nafasi ya tano ilichukuliwa na India, wakifuatiwa na Newzealand, Afrika Kusini, Nigeria, Kenya na Jamaica katika nafasi ya 10, wakifunga eneo la kumi bora.
Wakati Afrika Kusini, Nigeria na Kenya wakiitoa kimasomaso Afrika kwa ujumla wake, wapo Watanzania watakaoegemea kwenye Kenya kufanya vizuri na kuchukulia kwamba ndiyo mafanikio yao.
Hata hivyo, ni vyema ikaeleweka kwamba katika nchi nyingi zilizofanya vyema, Tanzania ina eneo kubwa na watu wengi zaidi pamoja na hata vipaji vingi zaidi ya hizo, tatizo ni jinsi ya kuvikuza tu.
Hata nchi ndogo kama visiwa vya Fiji vinavyokumbwa na misukosuko ya kisiasa imeweza kuwa juu ya Tanzania, pamoja na Barbados, Samoa, St Lucia isiyosikika kabisa, jirani zetu Zambia, Bahama, Kiribati ambayo huwezi kuwa hata na wazo ipo wapi kijiografia zote zimetikisa.
Hata Cyprus, Wales, Grenada, Botswana, Trinidad & Tobago, Ireland Kaskazini, Nauru, Isle of Man zimefanya kweli, wakati Tanzania haikupata hata medali moja, na kilichoelezwa na wahusika ni kusubiri ripoti ya wataalamu na kujipanga upya.