BINAFSI, nikiulizwa ni wizara gani iliyopata bahati mbaya kuanzia mwishoni mwa utawala wa awamu ya tatu na nne, nitasema ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Nakumbuka kabla ya kubadilishwa jina, wizara hii iliitwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, wakati huo ikiwa chini ya Joseph Mungai.
Katika awamu hii ya nne, wizara hii iko chini ya Margaret Sitta.
Sina haja ya kufafanua kazi na wajibu wa wizara hii, kwani inajieleza wazi kama jina lake lilivyo, kuwa ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, hivyo shule zote za msingi na sekondari, ziko chini yake.
Ninasema wizara hii ingali haijapata mtetezi kwa kigezo kimoja cha michezo mashuleni, kwani si Joseph Mungai wala Sitta, aliyeonyesha kujali michezo.
Wakati wa Mungai, aliamua kusitisha mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA), kwa hoja kuwa, yanachangia kufeli kwa wanafunzi.
Hoja yake ilikuwa, muda wanaopoteza katika michezo, unawafanya wanafunzi kutozingatia masomo ipasavyo, hivyo aliamua kupiga stop hadi hapo serikali itakapotoa mwongozo mpya.
Kimsingi, Mungai sijui alidanganywa na nani, kwa sababu, katika ufahamu wa kawaida tu bila kuhitaji hata elimu ya chuo kikuu, kwamba michezo huwezi kuitenganisha na masomo.
Wataalamu mbalimbali wamefanya tafiti zao na kubaini kuwa, kwa mtoto mwenye akili, akiwa anashiriki michezo, huweza kufanya vizuri zaidi darasani kwani akili yake inakuwa na siha njema.
Mifano hili, iko mingi kwa sababu wako wachezaji wa michezo mbalimbali duniani hata nchini, ambao vipaji vyao, vimeanzia shuleni.
Na zaidi ha hapo, wameweza kushiriki kikamilifu, tena kwa mafanikio makubwa kisoka na kimichezo, hivyo taifa kuwa na wanamichezo wasomi.
Kwa bahati mbaya, Mungai iwe kwa kupotoka au kupotoshwa, akasimamisha michezo kwa hoja kuwa, michezo inawafanya wanafunzi washindwe kumudu masomo.
Maana yake, Mungai alichangia kwa kiasi kikubwa, taifa kukosa wachezaji wasomi kwani kwa kuzuia michezo mashuleni, taifa lilikuwa likijiandaa kupata wanamichezo mbumbumbu.
Kitendo cha Mungai kutumia kivuli cha serikali kupiga marufuku michezo, kilimaanisha hata kile kitivo cha P.E kilichoko Chuo Kikuu Mlimani, hakina umuhimu wowote.
Ni hivyo kwa sababu, Kitivo kile hakiko kwa bahati mbaya, bali ni kwa kutambua umuhimu wa elimu ya viungo ambayo ni moja ya taaluma kama zilivyo nyingine.
Suala la michezio mashuleni, limekuwa likipewa umuhimu mkubwa tangu Tanzania kupata uhuru mwaka 1961.
Uwepo wa mashindano ya msingi, sekondari hata ngazi ya vyuo, kulichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana wachezaji waliolisaidia taifa.
Wako wasomi, waliotoa mchango wao katika timu mbalimbali katika ngazi ya klabu hata timu ya taifa.
Kwa umahiri wao, baada ya kuonekana katika mashindano ya shule za sekondari, walitwaliwa na timu mbalimbali za mashirika ya umma na binafsi, chini ya mpango wa elimu sehemu ya kazi.
Wako wengi walioibuka katika enzi hizo kwa mfano, katika soka ni kama akina Leodegar Chilla Tenga, Lawrance Mwalusako, Maulid Dilunga, Leopold Tasso Mukebezi na wengine wengi. Hii ni katika soka.
Kwa upande wa riadha ni kama Mwanjaa Mwinga, Filbert Naayi, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui na wakali wengine ambao, chimbuko lao ni mashindano ya shuleni.
Kwa kutambua umuhimu wa michezo mashuleni, ndiyo maana mawaziri kabla ya Mungai na Sitta, walisisitiza michezo na utamaduni katika mashule.
Mfano hai, ni aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Chediel Yohane Mgonja, ambaye kwa hakika, alionekana kupigania suala la michezo mashuleni.
Katika kipindi chake, utamaduni na michezo vilitumika kama kiungo cha mahusinao baina ya Tanzania na nchi nyingine kama za Ulaya, Asia, Marekani na hata Afrika kwa ujumla.
Nakumbuka miaka ya sitini hadi sabini, vikundi kutoka China, Urusi, Uingereza na Afrika vya michezo ya soka, ngoma na sarakasi, vilitua nchini na tukafurahia ushirikiano huo kwani ilikuwa ni darasa kubwa kwa vijana wetu.
Hata bada ya Waziri Mgonja, akaja waziri mwingine wa elimu, Isaeli Elinawinga ambaye aliamua kupigania pia suala la michezo ingawa si kama alivyokuwa Mgonja.
Baada ya Elinawinga, wakapita wengi akiwemo Thabita Siwale, lakini hakuna aliyethubutu kuvuruga suala la michezo, kwa kujua kuwa michezo ni pacha wa elimu na utamaduni.
Katika awamu ya tatu, ndipo alipokuja huyu Mungai, ambaye kwake michezo ni kikwazo cha wanafunzi kufaulu mitihani yao, kitu ambacho si kweli.
Ni kweli, wanafunzi walikuwa wanashindwa kufaulu, lakini tatizo halikuwa mashindano ya michezo, bali ni kitu kingine kabisa.
Baada ya kuingia Rais Kikwete madarakani, kwa vile ni mpenda michezo, tukadhani hata waziri atakayehusika na elimu, atazingatia suala la elimu ingawa michezo iko katika Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, iliyo chini ya Muhamed Seif Khatib.
Serikali ni moja, hivyo kwa vile Sitta ana wanafunzi na Khatib ana michezo, mawaziri hawa, walipaswa kuketi kuangalia ni kwa jinsi gani wanafunzi watashiriki michezo bila kuathiri muda wa masomo.
Baada ya uteuzi wa Sitta, wengine tuliona suala la michezo mashuleni, halijapata ufumbuzi, kwani aliyekabidhiwa wizara hiyo, si mwanamichezo.
Baada ya michezo kupigwa marufuku kwa muda mrefu, hatimaye serikali ikatangaza kuirejesha, lakini hadi sasa hakuna UMITASHUMTA wala UMISSETA.
Kwa mtazamo wangu, tatizo ninaloliona ni kwamba, Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia kupata rais mpenda michezo, lakini bahati mbaya tuliyo nayo, hatujapata waziri aliye mwanamichezo.
Angalia rais kwa kuipenda michezo, akathubutu kumleta Kocha wa Kibrazil, Marcio Maximo kwa ajili ya kuinoa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars na yule wa vijana wa chini ya miaka 17, Marcos Tinoco.
Pamoja na juhudui hizo, bila kuwako kwa mashindano ya shule za msingi na sekondari, itakuwa ni vigumu kwa Tanzania kupata mafanikio kimichezo.
Vipaji vinatakiwa viibuliwe kuanzia ngazi ya awali, yaani katika shule za msingi, sekondari kupitia mashindano mbalimbali kabla ya kuonekana na kushiriki mashindano ya Copa Coca-Cola na mengineyo.
Bila kufanya hivyo, Tanzania itakuwa vigumu kupata mafanikio ya michezo tunayoyataka kwani, ni wapi vijana watajifunza na kuonekana kama si shuleni?
Kinachosikitisha ni kuwa, tangu serikali iseme imerejesha mashindano mashuleni, hakujawa na juhudi zinazoonekana kwa macho katika hilo, zaidi ya kubaki kama hadithi.
Hii inatokana na ukweli kuwa, hakuna mashindano ya ngazi ya shule za msingi wala sekondari huku serikali ikijinadi kuwa, imerejesha michezo mashuleni. Tunajiuliza michezo hiyo i wapi?
Kutokana na mtiririko wa kimya hiki kuhusu michezo mashuleni, ndiyo maana ninasema, kilio cha michezo mashuleni, hakijapata mwitikiaji kwani Sitta, ameziba masikio.
Awamu hii ya nne, ilipaswa kutilia umuhimu mkubwa michezo, hasa kutokana na mkakati wake wa kupambana na uhaba wa ajira kwa vijana, hivyo kwa vile michezo ni ajira, ilipaswa kuhakikisha inarejeshwa mashuleni.