*Ni rekodi ya kwanza katika historia
*Awapita Platini na Johan Cruyff
Mpachika mabao wa Barcelona, Lionel Messi ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kwa mara ya nne.
Raia huyo wa Argentina ameweka rekodi mpya, kwani hakuna mcheza kandanda yeyote aliyepata kutwaa tuzo hiyo ya Fifa kama yeye.
Washindani wa Messi mwaka huu walikuwa Mreno Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na mchezaji mwenzake wa Barcelona, Andreas Iniesta anayetoka Hispania.
Kutia fora kwa Messi kunatokana na mkusanyiko wa ubora wa viwango katika mbinu za kuutawala mpira, pasi pamoja na ufungaji.
Hivi karibuni Messi alivunja rekodi ya miaka 40 aliyokuwa anashikilia mwanandinga Mjerumani Gerd Mueller, alipofikisha mabao 91 kwa klabu na nchi yake.
Messi amepata heshima hiyo kubwa zaidi ya soka duniani katika umri mdogo wa miaka 25, na dalili zinaonesha ataendelea kupata tuzo zaidi, kwani anapachika mabao kadiri muda unavyokwenda.
Mwargentina huyo amesaini mkataba mwingine utakaombakisha Nou Camp hadi mwaka 2018, jambo linaloweza kumwongezea kiwango alichopata tuzo huyo inayojulikana kimataifa kama Ballon d’Or.
Wachezaji wengine waliotwaa mara nyingi zaidi tuzo ya dhahabu ya mwanamichezo bora ni Rais wa Uefa, Michael Platini aliyeshinda mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 1983.
Pamoja naye ni Mholanzi Johan Cruyff aliyeshinda mara tatu pia, kati ya mwaka 1971 na 1974. Hata hivyo alikatishwa 1972, kwani tuzo ilikwenda kwa Mjerumani Franz Beckenbauer.
Mjadala unaoendelea pande mbalimbali duniani hivi sasa si juu ya ubora wa Messi nyakati hizi wala wingi wa mabao yake, bali iwapo ndiye bora zaidi katika soka tangu zama.
Mbrazili Edison Arantes do Nascimento ‘Pele’ na Diego Maradona huwa wanarejewa kama watu walioacha alama kubwa kwenye soka kutokana na uwezo wao.
Messi alitangazwa kuwa mfalme katika hafla iliyofanyika Zurich, Uswisi Jumatatu hii.
Kwa upande wa wanawake, Abby Wambach wa Marekani alipewa umalkia wa soka wa dunia. Vicente del Bosque wa Hispania aliibuliwa kocha bora.