*Waungana na Bayern, Real na Dortmund
*Bingwa atatoka Hispania au Ujerumani
Ilibidi mchezaji bora duniani, Lionel Messi aingie uwanjani kuwawasha Barcelona waliokuwa wamezimika mbele ya Paris Saint-Germain.
Japokuwa waliingia uwanjani na mtaji wa mabao mawili ya ugenini, Barca walipelekwa pita na PSG, hivyo kwamba jahazi lao likaelekea kuzama.
Katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya timu hizo mbili zilitoka sare ya mabao 2-2 nchini Ufaransa, hivyo katika marudiano Barca walihitaji sare ya aina yoyote ile.
Kama walivyocheza kipindi cha kwanza kwa akili, PSG walikianza kipindi cha pili kwa kasi, na dakika ya 50 walipata bao zuri kupitia kwa Javier Pastore.
Messi aliyekuwa benchi, akijulikana kwamba ni majeruhi, aliharakisha kubadili nguo kuwa tayari kuingia uwanjani.
Baada ya kuingia dakika ya 62, raia huyo wa Argentina alibadili mchezo, akiwaweka vyema mbele Barca, akitenga vyumba na kugawa mipira, na mwenyewe kujaribu kufunga.
Hazikupita dakika 10, alizaa bao baada ya kutoa pasi safi eneo la hatari ambayo hatimaye ilitua kwa Pedro aliyefunga bao lililowapeleka Barca nusu fainali.
PSG walijaribu kila njia kupata bao la pili ambalo lingewavusha, lakini haikuwa rahisi kwa Barca waliotwaa taji hilo mara nne, wakitafuta la tano sasa.
Juventus Si lolote kwa Bayern
Hadithi ya mcheza kwao hutuzwa haikuwa na maana kwa Juventus wa Italia, kwani wakicheza nyumbani kwao, walichabangwa mabao 2-0 na Bayern Munich, idadi ile ile waliyofungwa Ujerumani.
Kwa ushindi huo, Bayern wamewatoa Wataliano hao kwa jumla ya mabao 4-0 na kuingia nusu fainali hii kwa mara ya tatu katika miaka minne.
Waliowaua Juventus walikuwa Mario Mandzukic aliyekwamisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo wa Bastian Schweinsteiger katika dakika ya 64 kabla ya Claudio Pizarro kukomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza la Juventus dakika ya 90.
Nyota mwingine wa Bayern, Arjen Robben alikosa bao baada ya kiki yake kugonga mwamba wakati Juve walikaribia kufunga kupitia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Andrea Pirlo, huku kiki ya Fabio Quagliarella ikigonga mwamba.
Hitimisho hili la mechi za robo fainali linazipeleka Barcelona, Bayern Munich, Borussia Dortmund na Real Madrid nusu fainali, kwa hiyo kombe litakwenda ama Hispania au Ujerumani, kwani zote zimeingiza timu mbili.