SASA ni rasmi mshambuliaji Lionel Messi anaondoka katika klabu ya Barcelona. Taarifa za kuondoka nyota huyo zilielezwa alhamisi jioni kwa na kudhihirisha kuwa Barcelona imeshindwa katika jaribio lake kumshawishi kusaini dili jipya la mkataba wa kuitumikia timu hiyo.
Kwa sasa swali moja tu linalosumbua vichwa vya wengi ni wapi atakakocheza Messi kwa msimu wa ujao wa 2021/2022. Licha ya juhudi kutoka kambi ya rais wa Barcelona Joan Laporta kumshawishi Messi abakie klabuni imeshindikana.
Ikumbukwe kuwa Laporta alitumia jina la Lionel Messi katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Barcelona. Laporta aliahidi kuhakikisha supastaa huyo anabaki Nou Camp, lakini sasa habari ni kinyume chake.
Taarifa ya Messi kuachana na Barcelona ilielezwa na wawakilishi wake mbele ya uongozi wa Barcelona kuwa hana mpango wa kuendelea kucheza katika klabu hiyo.
Suala la uamuzi huo kutolewa sasa ni kitu ambacho kinatarajiwa kujulikana siku chache zijazo. Hata hivyo suala la msingi kwa sasa litakuwa mwelekeo wa Messi, kwamba atajiunga na timu gani ili aitumikie msimu ujao.
Mchezo wa soka ni biashara ya kuchekesha wakati mwingine, timu zinahangaika kusaka fedha katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa corona, lakini ukweli ni kwamba mchezaji mkubwa na hodari zaidi duniani anapatikana bure sokoni na kazi imebaki kwao kumsajili.
Idadi ya klabu zinazoweza kumsajili Messi ni chache mno kwa kuzingatia hali halisi ya nyota huyo, lakini mchezaji huyo atakuwa na uwanja mpana wa kuchagua timu ya kujiunga nayo kati yaz ile ambazo zitawasilisha ofa kwake.
TANZANIA SPORTS inafanya tathmini ya timu ambazo zinaweza kumsajili Lionel Messi na akavaa uzi wao kuanzia msimu ujao.
MATAJIRI WA PSG
Dili la kwenda PSG linawezekana kutokea na nyota huyo akaanza maisha mapya jijini Paris, kwa sababu ndiyo timu inayojipanga na kusajili wachezaji wakali zaidi ili kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Juhudi za kutwaa taji ndizo ziliwafanya wambakize Neymar Junior kwenye klabu hiyo, huku wakiwa kwenye juhudi za kumtaka nyota wao mwingine Kylian Mbappe akubali kusaini mkataba mpya
Endapo Messi ataingia kwenye rada za PSG itakuwa na maana kuwa rais wa timu hiyo Nasser Al-Khelaifi atachukua uamuzi wa kumuuza nyota wake Kylian Mbappe kwenda Real Madrid ili kupunguza gharama za mishahara pamoja na kumudu mshahara wa Messi.
Kwa mchezaji mwenyewe hilo ni jambo linalotakiwa kutuliza kichwa na kutafakari kwa kina. Kwa timu ambayo inapambana kuhakikisha inatamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Mbappe atapata wapi mshahara mnono kama anaolipwa PSG kwa sasa?
Na kwa Messi mwenyewe huu ni wakati wake wa kuvuna fedha nyingi, na hakuna timu yenye uwezo mkubwa kubeba mshahara wake kama PSG, ambako atakuwa na nafasi ya kucheza pamoja na mmoja wa marafiki zake Neymar Junior.
Mtindo wa maisha ya jiji la Paris ni rahisi mno, hata kama ligi ya Ufaransa haionekani kuwa na ubora wa hali ya juu, lakini itanufaika na ujio wa Messi. Pia Messi atapata wasaa wa kupumzika mikikimikiki ya soka aliyokutana nayo kwenye La Liga katika kipindi chake cha kucheza Barcelona.
KWENDA KWA PEP GUAERDIOLA WA MAN CITY
Manchester City imekubali kutoa kiasi cha Euro milioni 118 kumsajili kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Jack Grealish, lakini sasa wanaweza kuangalia uwezekano wa kumsajili Lionel Messi pia, lakini itategemea kama watapata wanunuzi wa mawinga wao wawili Bernardo Silva and Riyad Mahrez.
Kama ataamua kwenda Man City maana yake atakwenda kuungana na kocha wake aliyetamba naye kwenye mashindano mbalimbali barani Ulaya. Watakuwa na uwezekano wa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa mara nyingine. Pia atakuwa na uwezekano wa kutwaa taji la Ligi Kuu England msimu ujao akiwa Man City. Hiyo ni timu yenye kikosi kikubwa cha gharama na chenye vipaji vya daraja la juu.
Guardiola alitwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Messi. Lakini ameshindwa kutwaa mataji hayo bila kuwepo Messi katika kikosi chake, huenda akafanya jaribio la kumsajili nyota wake wa zamani kuwa sehemu ya kikosi chake cha ushindi.
Ikiwa Messi atajiunga Man City utakuwa mwisho wa mradi wa timu hiyo kuifanya kuwa kinara barani Ulaya wakiwa chini ya uongozi wa Ferran Soriano na Txiki Begiristain ambao waliwasili klabuni hapo wakitokea Hispania katika klabu ya Barcelona.
KUFUATA CHANGAMOTO MANCHESTER UNITED
Sera za usajili za Manchester United kwa sasa haziruhusu kusajili mchezaji aina ya Lionel Messi iwe kama mchezaji huru au kununuliwa moja kwa moja. Lakini klabu hiyo ni miongoni mwa zenye uwezo wa kulipa dau la kumsajili Messi na hivyo kuifanya timu hiyo kwua sehemu ambayo mchezaji huyo anaweza kwenda kujiunga nayo.
Ni vigumu kumchagua mchezaji mwenye umri wa miaka 34 kujiunga na Man United au Man City kwa sasa, kwa sababu Man United haitakuwa tayari kugombania ubingwa hadi mwaka 2023, lakini kama wakiamua kumsajili wanaweza kumtumia katika mipango yao ya kurejesha makali yao barani Ulaya kama zilivyokuwa zama za Sir Alex Ferguson.
Messi amewahi kuiadhiri Man United katika fainali mbili za Ligi ya Mabingwa, jijini Rome na London, ambapo kipaji chake kiliwatetemesha mno mashabiki wa timu hiyo. Na sasa kama atasajiliwa wanaweza kujivunia kuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa duniani kucheza katika timu yao.
Lakini hesabu zinaonesha kuwa huenda ikawa vigumu kwa sababu tayari timu hiyo imekwisha kumsajili Jadon Sancho na kushindwa kumpata mnunuzi wa Jesse Lingard.
KIBIBI KIZEE CHA TURIN
Maisha ya Juventus kwa sasa ni kama vile unatazama filamu kutoka nchini Marekani. Juventus iligonga vichwa vya habari baada ya kumsajili mshambuliaji Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid ya Hispania.
Ikumbukwe kwao kusajili ni jambo la kawaida, na uwezo wa kumsajili Messi wanao. Je itakuwaje siku Messi na Ronaldo wakiwa timu moja ya Juventus? Hakika itakuwa kama njozi machoni pa wengi lakini utakuwa mwisho wa kambi mbili za Messi au Ronaldo.
Inawezekana Messi akisajiliwa Juventus huenda asiwe mchezaji wa kikosi cha kwanza, lakini huwezi kumbeza nyota huyo linapofika suala la kipaji na uwezo wa kuibeba timu.
Ronaldo na Messi wamekuwa wapinzani kwa muda mrefu katika mchezo wa kandanda, La Liga Ligi ya Mabingwa na kwenye tuzo binafsi za Ballon d’Or. Kwahiyo kufikiria wawe wachezaji wa timu moja ni jambo ambalo sijui litakuwa na sura gani.
Hakuna mwenye uhakika wa nini kitatokea kama wachezaji hawa watacheza timu moja. Ronaldo amewahi kutamka kuwa anatamani wakati wa kucheza na Messi wakiwa timu moja. Huwezi kujua kwa upande wa Messi, inawwezekana naye anafikiria hivyo.