Serikali imetoa masharti kwa Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) kabla ya kuruhusu kurejea kwa mechi zilizobaki za msimu huu, ikiwa ni pamoja na kuonesha baadhi ya mechi bure.
Serikali pia imeitaka bodi hiyo kutoa fedha zaidi kwa Ligi ya Soka na kwa zile za ngazi za chini kabisa, yakiwa ni masharti ya kurejea tena kwa msimu ambao kwa EPL zimebaki mechi 92 na sasa wanavutana jinsi ya kuzimaliza.
Masharti hayo yametolewa na Waziri wa Utamaduni, Oliver Dowden Alhamisi hii, akitoa ruhusa ya mechi kuanza tena ili mradi iwe salama kufanya hivyo kwa wachezaji na wadau wengine watakaokuwa uwanjani na maeneo ya jirani.
“Serikali inafungua mlango kwa ajili ya soka ya ushindani kurejea kwa usalama Juni. Hii itakuwa ni pamoja na kutanua fursa kwa washabiki kutazama mubashara mechi hizo na fedha zitakazotokana na mechi kurejea zisaidie familia pana zaidi ya soka.
“Sasa ni juu ya mamlaka za soka kukubaliana na kuhitimisha mipango ya kumalizia msimu ili pawepo na nia njema ya pamoja ya kufanya hivyo kwa washabiki wao, jumuiya ya soka na taifa kwa ujumla. Serikali na wataalamu wetu wa afya wataendelea kutoa miongozo na kuunga mkono soka kabla ya uamuzi wowote wa mwisho utakaoweka mipango hiyo kwenye utekelezaji,” akasema Waziri Dowden.
Bodi ya EPL ipo kwenye majadiliano na washirika wake wa utangazaji – Sky na BT juu ya kupata namna ya kuonesha baadhi ya mechi bure msimu utakapoanza. Suluhu inayopendelewa zaidi na serikali ni kwamba mechi 45 ambazo hazijawekwa kwenye mpango wowote miongoni mwa madili yaliyopo ya televisheni zioneshwe kwenye chaneli za bure au kuzitiririsha bure kwenye mitandao ya jamii kama YouTube.
Vyanzo vya Habari kutoka Bodi ya EPL vinadai kwamba wametakiwa pia kuhakikisha wanatoa fedha kwa klabu ndogo ambazo zimekuwa katika mkwamo kiuchumi, huku Sky na BT nao wakitaka fidia iwapo vigezo na masharti waliyowekeana kwenye mikataba yao havitatekelezwa.
Malumbano na mikwaruzano juu ya mapato ya kurusha si jambo jipya kwenye soka ya England huku kukiwapo pia na wasiwasi juu ya mambo mengine kabla ya kurejea kwa mechi zilizosalia.
Kikwazo kilichopo kwa sasa kinachoonekana ni kikubwa, ni jinsi ya kuwezesha wachezaji kurejea kwenye mazoezi na kisha uwanjani, baada ya kuwa nje ya dimba kwa miezi miwili. EPL na EFL wamebuni protokali za kitabibu zinazoenda sambamba na ushauri mpya wa serikali juu ya maozezi kwa wachezaji wa kulipwa. EPL inaamini kwamba itaweza kushawishi wadau wake – klabu zote 20 kuridhia protokali hizo Jumatatu ijayo.
Matokeo ya kura hiyo kuwa chanya kwa EPL si jambo la kuhakikishiwa, kutokana na mkururo wa mikutano baina ya wachezaji, makocha wa klabu na maofisa wengine. Baadhi ya wachezaji, ikiwa ni pamoja na nahodha wa Watford mwenye ushawishi mkubwa – Troy Deeney, wanaaminika waliondoka kwenye mkutano wa mwisho wakiwa na wasiwasi kwamba masuala ya usalama wao hayakuwa yameshughulikiwa ipasavyo.
Baadhi ya makocha, akiwamo Jose Mourinho wa Tottenham Hotspur, wanadaiwa kutaka mazoezi yawe zaidi ya wiki tatu na yagharimiwe na EPL kupitia mpango wa mradi wake unaokwenda kwa jina la ‘Project Restart’. Makocha na wachezaji watashirikishana kwenye ngazi ya klabu kabla ya kura yenyewe.
Ikiwa protokali hizo mpya zitapitishwa, wachezaji wataruhusiwa kufanya mazoezi kwenye makundi lakini watatakiwa kuzingatia kukaa mbalimbali kiasi. Kukaribiana na kugusana wakati wa maandalizi ya mechi, kutaruhusiwa tu kutokana na ushauri zaidi kutoka serikalini.
“Nataka mazoezi yaanze na nina hamu sana kwa EPL kurejea mapema ikiwa tu ni salama kufanya hivyo, hasa kwa kuwa nasi tunaona ligi nyingine zikijiandaa kwa ajili ya kurejea,” anasema huku akiongeza kwamba haiwezi kuwa mapema sana.