Kulikoni, na ana mamlaka gani?
WAKATI muhimu katika soka ya Uingereza uliwadia Jumanne, pale muswada wa mdhibiti wa kusimamia soka ulipowasilishwa kwenye Bunge la Uingereza, kwa minajili ya kuanzisha mratibu huru wa soka.
Novemba 2021, mapitio yalitoa mwito wa kuanzishwa kwa mratibu huyo, huku serikali ikitangaza mipango ya kuanzisha hilo Februari 2023.
Mdhibiti husika atakuwa huru dhidi ya serikali na mamlaka za soka. Kadhalika atakuwa na uwezo wa kuzuia mianya mipya, ikiwamo mashindano kama European Super League, na kuwa na mamlaka juu ya mgawanyo wa fedha na kuwachunguza kabla ya kuwaidhinisha wamiliki na wakurugenzi wa klabu.
Hapa, Matt Slater na Peter Rutzler wanafafanua juu ya lini mdhibiti huyo ataanza kazi yake, kazi hiyo itagharimu kiasi gani – na ni vipi dunia ya soka itakavyopokea jambo hilo jipya.
Mdhibiti ataanza kazi lini hasa?
Mdhibiti husika ni kitovu cha Muswada wa Kusimamia Soka, uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza Jumanne.
Muswada huo lazima usomwe tena mara mbili zaidi bungeni (House of Commons), upitiwe na kamati ya bunge kisha upelekwe kwenye bunge (House of Lords), kabla ya kuridhiwa na Mfalme na kuwa sheria, tayari kuanza kutumika.
Hata hivyo, kwa kuwa jambo hili linaungwa mkono na zaidi ya chama kimoja, inatarajiwa kwamba muswada utapita bila tabu. Mkwamo pekee unaowezekana ni iwapo muda wa bunge hautamalizika kabla ya kupitia, ikizingatiwa kwamba uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Ingawa hivyo, kuna uwezekano kwamba muswada huo utakuwa umefika mbali kiasi cha kukubaliwa juu kwa juu kimchakato kabla ya uchaguzi. Hii inamaanisha kwamba, mambo yote yakienda sawa, mdhibiti huyo huru wa soka atakuwa tayari kazini mapema 2025.
Ama juu ya nani ataendesha chombo hicho na makao yatakuwa wapi ni mambo ambayo bado hayajaamuliwa, japokuwa mchakato wa kumpata mwenyekiti umeshaanza, ambapo mtu husika atawajibika kuteua timu ya utendaji.
Mdhibiti atagharimu kiasi gani nani atamlipa?
Inavyoelekea chombo hiki kitakuwa kikubwa, kwani kimepewa bajeti pendekezwa ya pauni milioni 10, zitakazotokana na fedha zitakazotozwa klabu zitakazokuwa chini ya utawala wa udhibiti. Hizo ni klabu 116 za Ligi Kuu (EPL), English Football League (EFL) na National League (NL).
EPL ndio watabeba mazigo mkubwa zaidi kwa kutoa kiwango kikubwa zaidi cha fedha hizo, kitu kinachokaribia asilimia 80 ya bajeti yote na asilimia zake zitagawanywa sawasawa kwa mapato ya EPL yatokanayo na urushwaji matangazo, ambapo klabu zilizofanikiwa zaidi zitalipa takriban £600,000 kwa mwaka.
Akizungumza kwenye mkutano wa vyama vyote bungeni, mmoja wa wadau wakubwa wa uanzishwaji wa mdhibiti huyo, Tracey Crouch, Waziri wa zamani wa michezo ambaye pia ndiye aliyeandika ripoti juu ya kuanzishwa kwa mdhibiti husika 2021, alisema soka itakuwa ikijilipa yenyewe.
Mdhibiti atakuwa na mamlaka gani?
Jambo muhimu zaidi ni kwamba mdhibiti atatazama kuhakikisha kwamba utoaji leseni kwa klabu utahakikisha wahusika kuendana na matakwa ya kanuni za fedha, ushirikishwaji wa washabiki na kulinda urithi wa klabu.
Mdhibiti huyo atakuwa na wajibu wa kuchunguza na kuidhinisha wamiliki na wakurugenzi wa klabu, na pia kuhakikisha viongozi husika wanakidhi viwango vilivyowekwa.
Mdhibiti atakuwa pia na mamlaka ya kutoza faini ya hadi ya asilimia 10 ya mapato ya mwaka ya klabu, ikitokea kwamba klabu zimekiuka kwa kiasi kikubwa matakwa ya leseni zao.
Lini mdhibiti anaweza kusimamia utatuzi wa masuala ya kifedha?
Kwamba ni linin a kwa vipi mdhibiti anaweza kutumia mamlaka yake yamekuwa masuala mazito ya mjadala na Mawazo ytofauti katika miezi ya karibuni, ambapo klabu za EPL zilishindwa kufikia muafaka juu ya mfumo wa usambazaji fedha, kiasi wanachoweza kuwapa EFL.
Serikali ilikuwa ikitarajia kwamba ‘dili jipya kwa soka’ lingefikiwa na kukubaliwa na ligi za hapa kabla ya mdhibiti kuchukua nafasi yake, lakini haijawa hivyo. Hata hivyo, hilo huenda likakamilishwa, madhali kila mtu ameshajua kwamba ‘sherifu’ mpya yupo njiani.
Kulikoni mdhibiti kuletwa?
Inawezekana kwamba mapitio, hasa ya washabiki yamechangia kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa chombo hiki, japo kuna masuala mawili kwenye soka ya Uingereza yamechangia.
Kwanza ni kuanguka kwa klabu ya kihistoria ya Bury mwaka 2019, kulikopelekea ahadi kutolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Conservative mwaka huo huo. Mapitia yalisogezwa mbele, kutokana na majaribio ya klabu sita— Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur — kuungana na kutaka kuunda European Super League. Miongoni mwa mapendekezo 10 ya kimkakati yalikuwa kuanzishwa kwa mdhibiti huyo.
EPL ilipokea vipi suala la mdhibiti?
Wakati EFL, Chama cha Soka, Chama cha Washabiki wa Soka na mawaziri serikalini, akiwamo Waziri Mkuu Rishi Sunak, walionesha matumaini kwamba mdhibiti huyo angeweza kuanza kazi mapema iwezekanavyo, EPL walionesha kutoridhishwa na uanzishaji huo.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye mkesha wa kusomwa kwa muswada huo, Bodi ya Ligi Kuu ilieleza kwamba ilikuwa na kutofurahishwa kwani yangeweza kuwapo matokeo mabaya, hata kama si ya kudhamiriwa na sheria husika, na kwamba ingeweza kudhoofisha ushindani na mvuto wa soka ya England.
Vipi kuhusu EFL?
Alipoulizwa juu ya hili, Mwenyekiti wa EFL, Rick Parry alisema: “Hakuna kitakachobadilisha ushindani kwenye Ligi Kuu. Ukitazama nyuma mwaka 2009 pale Ligi Kuu ilipowekwa kuwa namba moja katika ligi barani Ulaya- tulikuwa na timu zenye kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, nusu fainali mara tatu kati ya nne katika miaka mitatu katika kipindi cha miaka mitano – ilikuwa ikilipa £600 milioni kwa mwaka katika mishahara zaidi ya ligi iliyofuata.
“Kufikia 2019, pengo lilizidi kuwa kubwa kufikia pauni bilioni 1.6, ikimaanisha lilitanuka kwa pauni bilioni 1. Wakati tukiendelea na mjadala, pengo likaongezeka tena hadi kufikia pauni bilioni 2.
Pengo hilo linazidi kuwa kubwa, hivyo wazo la kwamba Ligi Kuu inaenda kukumbana na vikwazo na haitakuwa na ushindani, siwezi kabisa kuona. Sioni msingi wa mjadala huo hata kidogo.”