Kocha asiye na mafanikio wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo amemrudisha kikosini Abdi Kassim ‘Babi’ aliyemuacha tangu mwanzoni mwa mwaka, siku chache baada ya kiungo huyo kuifungia Zanzibar Heroes bao lililomtoa nishai Mbrazili huyo kwenye Kombe la Chalenji la Afrika Mashariki.
Babi alitemwa Februari 11 Maximo alipotangaza kikosi cha Stars kilichocheza mechi ya kirafiki na Zimbabwe, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, CHAN, ya nchini Ivory Coast.
Babi alifunga kwa mpira wa adhabu ndogo goli lililoipa Zanzibar Heroes ambayo ilikuwa na wachezaji wawili tu ambao wamewahi kuthaminiwa na Mbrazili huyo, ushindi wa 1-0 dhidi ya Kilimanjaro Stars ya Maximo nchini Kenya mwezi huu.
Mbali na kumrudisha Babi, kocha huyo ambaye hajabeba hata Kombe la Chalenji katika miaka mitatu ya kuwa mwalimu wa kigeni nchini, pia amemrudisha kipa anayelalamikiwa kwa ubovu hata na walimu wa klabu yake na ambaye anapingwa na mashabiki Shabaan Dihile, ambaye alimtema katika kikosi cha Chalenji.
Kocha huyo ambaye mrithi wake ameshaanza kutafutwa baada ya shirikisho la soka, TFF, hatimaye kumchoka, alikiri kuwa mbioni kutafuta timu nyingine mara baada ya mkataba wake kumalizika Julai mwakani.
Kwa rekodi yake Stars, hatahivyo, ni vigumu kupata kazi hivi karibuni.