*UEFA yatazama dili za Qatar na klabu hizo
*Kombe la dunia 2022 Qatar pia lazua jambo
Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) umeanza uchunguzi juu ya harufu ya mlungula kati ya taifa la Qatar na kampuni zake kwa upande mmoja na klabu kubwa za soka.
UEFA ambayo juzi tu ilieleza kuguswa na kutoa ushirikiano kwa polisi wanaochunguza kashfa za upangaji matokeo, inaelekea inataka kufukua kila mahali.
Inasema inaangalia uwezekano wa kukiukwa kwa kanuni yake ya haki kwa kuwianisha na thamani katika mikataba ya udhamini.
Jicho lake linatua katika klabu za Manchester City na Paris-Saint Germain (PSG) ya Ufaransa zilizofunga mkataba mnono na mashirika yanayomilikiwa na serikali ya Qatar, kutokana na kujuana kwingi.
Mashirika hayo ya umma yapo nchini Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, na kadiri muda unavyokwenda, wapo wanaodhani kwamba kuna harufu ya kutembea rushwa.
Uchunguzi wa UEFA pia unakuja wakati utata unakolezwa juu ya taifa la Qatar kushinda uandaaji wa mashindano ya Kombe la Dunia 2022.
Hata hivyo masuala yote hayo kwa pamoja, yanajenga picha kwamba itakuwa vigumu mno kuchimbua mzizi wa rushwa, kama ilitumika, kwa sababu ya jinsi Qatar ilivyojitandaza kwenye soka.
Mpelelezi wa masuala ya maadili wa FIFA, Michael J. Garcia alinukuliwa mwezi uliopita akisema alikuwa anapitia upya tuhuma za Qatar kupindisha taratibu hadi kupata uenyeji wa michuano hiyo mikubwa zaidi.
Kwa upande wa UEFA, uchunguzi unalenga kwenye mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mkataba wa pauni milioni 200 kwa mwaka ulioingiwa na PSG na Mamlaka ya Utalii ya Qatar.
Manchester City wenyewe wameingia mkataba wa pauni milioni 625 kwa ajili ya uwanja wa Etihad, ambalo ni shirika la ndege lililopo Abu Dhabi.
PSG inamilikiwa na Qatar Sports Investments (QSI), ambalo ni shirika la serikali wakati Manchester City ilichukuliwa na mwanafamilia ya kifalme ya Emirates.
Sheria ya UEFA inayotaka haki katika uwekezaji na biashara kwenye soka inalenga pia kuzuia wamiliki wa klabu kukwepa kanuni zake kwa kutumbukiza fedha kupitia kampuni na mashirika wanayomiliki.
Suala linalohusika hapa ni ukweli kwamba umiliki wa klabu hizo na mashirika yanayozidhamini yanahusiana kupita kiasi.
Katibu Mkuu wa UEFA, Gianni Infantino anasema kwamba kanuni zinazungumzia wazi haja ya wadau wa klabu kutotumbukiza fedha tu kwenye klabu moja kwa moja au vinginevyo.
Moja ya tuhuma, ambazo bado hazijathibitishwa ni kwamba Qatar ilipanga kuitwaa PSG kisha kuongeza uwekezaji wake nchini Ufaransa.
Michel Platini ambaye ni kigogo wa UEFA na mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA ana mtoto aliyeajiriwa kuwa mwanasheria wa QSI.
Inadaiwa ilikubaliwa kwamba ipigwe kura kuivusha Qatar kuwa mwenyeji wa kombe hilo la dunia 2022, kisha kituo cha televisheni cha Al Jazeera cha Qatar kinunue haki ya kurusha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Inadaiwa kwamba yote hayo yalijadiliwa Ikulu ya Elysee wakati wa urais wa Francois Sarkozy, aliyependa sana mawazo hayo, kubwa kwake likiwa watu watawekeza nchini mwake, na yeye mwenyewe ni shabiki wa PSG.
Ni suala la kusubiri kuona, iwapo kweli uchunguzi utafanyika, na kama mkono ‘mrefu’ wa sheria utafikia hata wale wasiotarajiwa katika hili, au itaishia kuelezwa kwamba ni tuhuma zisizo na msingi wowote.