Menu
in

Mbio za kuwania uongozi TFF zaanza kimyakimya

ZIKIWA zimesalia siku 90 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, tayari kampeni za chini chini zimeanza huku Katibu Mkuu wa zamani wa FAT kabla ya kuwa TFF, Michael Wambura akionekana kujipanga mapema.

Uchaguzi Mkuu wa TFF ulifanyika Desemba 27 na kumalizika Desemba 28, 2004 kwenye Hoteli ya Golden Tulip kwa Leodegar Tenga kutangazwa kuwa Rais wa kwanza wa TFF baada ya kurekebisha katiba.

Mwenyekiti wa zamani wa FAT na TFF, Muhidin Ndolanga na Katibu wake, Michael Wambura walishindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Uchunguzi uliofanywa jijini Dar es salaam, umebaini kuwa baadhi ya wajumbe wanaanza kujipanga akiwemo Michael Wambura ambaye katika mahojiano katikati ya jiji la Dar es Salaam, alisema kuwa hana nia hiyo.

Wachunguzi wa duru za kispoti wanasema kuwa kati ya watu ambao hawajakata tamaa ni Wambura ambaye alidiriki kwenda shule ili kutimiza vigezo kwa kiongozi wa juu wa TFF lazima we mwenye shahada.

Pia baadhi ya watu kadhaa wanaonekana kusita kujitokeza mapema kwani wamekuwa wakitengeneza misingi na wamekuwa wakitajwa kutaka kuchukua nafasi mbalimbali za uongozi.

Katibu Mkuu wa zamani wa FAT, Kanali Mstaafu, Ali Hassan Mwanakatwe ni kati ya watu wanaotajwa kufiti katika nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais ambayo anayeishikilia kwa sasa, Crescentius Magori tayari ameshatangaza kuwa hatoiwania nafasi hiyo.

Katibu wa FAT, Ismail Aden Rage pia amekuwa akitajwa kutaka kurejea kwenye nafasi yake baada ya kusafishwa na mahakama.

Rage alipoteza nafasi yake ya Makamu wa Pili baada ya kukosa sifa kwa kutohudhuria vikao vitatu mfululizo kutokana na kufungwa kwa ubadhirifu wa fedha za iliyokuwa FAT. Hata hivyo aliachiwa huru kwa msamaha wa rais mwaka juzi.

Mpaka sasa, TFF imekuwa katika sifa za kukubalika kutokana na uongozi uimara wa Tenga ambao hauruhusu lepe la migogoro tofauti na iliyokuwa FAT. Tenga imeelezwa kuwa hataki tena kuongeza muhula katika TFF.

Pamoja na hayo, uongozi wa Tenga umekuwa na bahati kuwepo kwa mkono wa serikali katika suala la malipo ya kocha wa timu ya taifa, kitu ambacho katika miaka ya nyuma, lilikuwa tatizo kubwa.

Pia TFF chini ya Tenga imeweza kupata wadhamini wa uhakika kwa timu ya taifa ambao ni Kampuni ya Bia ya Serengeti, SBL na Benki ya NMB ambao kwa vipindi tofauti wameingia mikataba ya kuihudumia timu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Uchaguzi Mkuu wa TFF umepangwa kufanyika mwisho wa mwaka huu baada ya kumalizika kwa kipindi cha miaka minne cha uongozi wa Tenga.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version